Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa akiwa katika mzungumzo na Kamishna
Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo
Grandi. Mazungumzo hayo yamefanyika kando na mkutano wa TICAD7
Yokohoma,Japan.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi
akifuatilia mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la
Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi(hayupo pichani)
Yokohama, Japan.
Mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa na Kamishna Mkuu
wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi
kuhusu wakimbizi waliopo Tanzania yakiendelea. Yokohama, Japan.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa akiagana na Kamishna Mkuu wa
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi mara
baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina yao kuhusu wakimbizi waliopo
Tanzania. Mazungumzo hayo yamefanyika Yokohama, Japan.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi
akisalimiana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani
(UNHCR) Bw Filippo Grandimara baada ya kumaliza kufanya mazungumzo na
Waziri Mkuu mhe. Kassim M. Majaliwa. Yokohama, Japan.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiteta
jambo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR)
Bw Filippo Grandi mara baada ya kumalizika mazungumzo ya Waziri Mkuu
mhe. Kassim M. Majaliwa. Yokohama, Japan.
……………….
Tanzania imetoa rai kwa Jumuiya ya
Kimataifa na Japan kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwenye
changamoto mbalimbalii ambazo bado zinajitokeza kwenye baadhi ya nchi za
Afrika ikiwemo ugaidi wa kimataifa, uhalifu, mabadiliko ya tabianchi,
ukame, njaa na
magonjwa sambamba na kujitolea kuchangia na kuwekeza
kwenye miradi iliyobuniwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuboresha
mazingira yaliyoharibiwa kutokana na uwepo wa kambi za Wakimbizi kwenye
maeneo mbalimbali nchini.
Rai hiyo imetolewa na Waziri
Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Serikali kuhusu kuimarisha amani na usalama barani Afrika uliofanyika
wakati wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya
Afrika (TICAD 7) uliomalizika leo tarehe 30 Agosti 2019 jijiji Yokohama,
Japan.
Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa,
miradi hiyo ambayo ni pamoja na kubadilishana teknolojia hususan kwenye
maeneo ya mipakani na mifumo ya kutoa taarifa mapema kwa ajili ya
kujikinga na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza itasaidia
kuboresha mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameharibiwa na wakimbizi
na watu wanaotafuta makazi.
“Uwepo wa wakimbizi na watu
wanaotafuta makazi kwa namna moja au nyingine huathiri mazingira, jamii
usalama na uchumi wan chi inayowapokea. Hivyo ni ombi letu kwenu
kushirikiana nasi kwenye miradi mbalimbali katika kuboresha mazingira”
alisema Mhe. Waziri Mkuu.
Aliongeza kusema kuwa, kwa
miaka mingi Tanzania imekuwa kimbilio kwa wakimbizi kutoka nchi jirani
wanaokimbia nchi zao kutokana na migogoro ya kisisasa, kikabila na
kuibuka kwa vikundi vya uasi. Alieleza kuwa hadi kufikia tarehe 1 Agosti
2019, Tanzania inahifadhi wakimbizi wapatao 305,983.
Vilevile, Mhe. Waziri Mkuu
aliongeza kuwa, katika kuhakikisha amani inapatikana pote dunaiani,
Tanzania ina mchango mkubwa katika amani, utulivu na utatuzi wa migogoro
barani Afrika na kwamba ni miongoni mwa nchi zinazochangia misheni za
ulinzi wa amani katika nchini mbalimbali Afrika na duniani.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri
Mkuu amefanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kimataifa la
Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Bw. Fillipo Grandi walipokutana pembezoni
mwa Mkutano wa Saba wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika.
Wakati wa mazungumzo hayo,
Mhe. Waziri Mkuu na Bw. Grandi wamekubaliana kuimarisha ushirikiano
katika kuhakikisha usalama kwenye makambi ya wakimbizi, kuimarisha
mipaka pamoja na kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira
unaofanywa na Wakimbizi.
Akizungumzia Mkutano wa Saba
wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwa siku
tatu jijini Yokohama, Japan. Mhe. Waziri Mkuu amesema Mkutano huo
umemalizika kwa mafanikio huku Wakuu wa Nchi a Serikali wakikubaliana
kuteleleza Azimio la Yokohama linalolenga kuleta mapinduzi barani Afrika
kwa kuimarisha masuala ya usalama, elimu, sayansi na teknolojia na
kukuza sekta binafsi.
Amesema kuwa, Tanzania
itajipanga kikamilifu kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano
huo ambayo ni ya manufaa makubwa kwa nchi za Afrika.
Mhe. Waziri Mkuu alieleza kuwa,
maazimio hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamegusa sekta zote muhimu
zikiwemo afya, elimu, maendeleo ya miundombinu, sayansi na teknolojia na
amani na usalama yanalenga kuzikwamua kiuchumi nchi za Afrika kupitia
ushirikiano na Serikali ya Japan.
“Tumemaliza kikao cha TICAD
leo ambacho kimejadili mambo mengi yakiwemo ya usalama, maendeleo ya
elimu, sayansi na teknolojia na namna nzuri ya kuendesha nchi zetu
kupitia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa miundombinu. Kikao hiki kwetu
Tanzania ni chachu ya kuendeleza jitihada zetu za kufikia uchumi wa
kati na mapinduzi ya viwanda ifikapo mwaka 2025” alifafanua Waziri
Mkuu.
Mhe. Waziri Mkuu aliongeza
kuwa, Japan imetenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za
Afrika kupitia fursa ya mikopo na ufadhili. Aliongeza kuwa, Tanzania
itajipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kuandaa maandiko mazuri ya miradi
ya kipaumbele ili kupata fedha hizo.
Amesema kuwa, nchi za Afrika
ambazo kwa kiasi kikubwa zimejaliwa kuwa na maliasili na malighafi za
kutosha kwa ajili ya kujenga uchumi, zimesisitizwa kuimarisha mahusiano
na sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa nchi hizo.
No comments :
Post a Comment