Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola
(kulia), akifurahia jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi nchini,
Sudi Mwakibasi, wakati walipokua wametembelea Kituo cha Shirika la Kuwahudumia
Wahamiaji (IOM), kilichopo Makere, Wilayani Kasulu, Mkoani Kigoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola,
akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma. Lugola alisema Serikali
Tanzania na Burundi imesaini hati ya makubalinao ya kuwarejesha wakimbizi 2000
kwa kila wiki nchini mwao. (Picha na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi).NA
FELIX MWAGARA, KIGOMA
Wakimbizi hao waliopo katika Kambi
ya Nduta na Mtendeli wanatarajiwa kusafirishwa kuelekea katika nchi yao ya
asili kutokana na amani iliyopo katika nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola, na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchini Burundi, Pascal Barandagiye
tayari wamesaini makubaliano hayo ambayo watahakikisha wakimbizi wote waliopo
katika kambi hizo wanartejeshwa nchini mwao bila kukwamishwa na mtu au shirika
lolote.
Akizungumza na waandishi wa habari,
mjini Kigoma jana, Waziri Lugola alisema makubaliano hayo yataanza rasmi Oktoba
mosi na wakimbizi hao watakuwa wanarejeshwa nchini mwao na kupata mapokezi
makubwa na Serikali ya Burundi.
“Tunataarifa wapo baadhi ya watu,
mashirika ya kimataifa wanawarubani wakimbizi wakiowatangazia kuwa Burundi
haina amani, jambo ambalo si la kweli, nchi hiyo ina amani na wakimbizi
wanapaswa kurejea nchini mwao,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa,
atawachukulia hatua kwa watakaokwamisha zoezi hilo la kuwasafirisha wakimbizi
hao, kwa kuwa Serikali ya Wakimbizi inataka watu wao na Tanzania imeamua kuwapa
watu wao ili waende wakaijenge nchi.
“Natoa kauli hii sio kuwatisha au
kutishia nyau, bali nasema, Serikali ya Magufuli haiwezi kuchezewa na mtu
yeyote, hivyo tutawakamata wanaowarubani, wanaowashawishi wakimbizi wasiende
nchini mwao,” alisema Lugola.
Wiki iliyopita, katika mkutano wa
hadhara katika Kambi ya Nduta, baadhi ya Wakimbizi walisema wanawekewa vikwazo
na kucheleweshwa na baadhi ya watendaji wa mashirika ya wakimbizi kambini humo
wakati wanapoomba kujiandikisha kurejeshwa kwao.
Mkimbizi
wa kambi hiyo, Nzoisa Bhainoje, alisema yupo tayari kurejea nchini Burundi
lakini amefanya juhudi za kwenda eneo la kujiandikisha kambini hapo lakini
hakufanikiwa kutokana na kusumbuliwa akiambiwa kuwa idadi wanaotakiwa kuondoka
imekamilika.
“Nakumbuka
nilifika eneo la kuondoka siku ya Jumanne lakini ilishindikana kujiandikisha kutokana
na kukwamishwa, wengi tunataka kuondoka lakini tunashindwa kuondoka kwasababu tunakwamishwa,”
alisema Bhainoje.
Bhainoje
aliongeza kuwa, wanaomba watendaji hao wawaruhusu kwa wale wanaotaka kurejea
nchini mwao kwa hiari, lakini kwa wale ambao hawataki kuondoka wanaweza kubaki
kwa mipango yao.
Baada
ya wakimbizi hao kutoa kero zao kwa Waziri Lugola na Waziri Barandagiye, ndipo
Lugola aliagiza kufanyika uchunguzi katika kambi hiyo kuwakamata wale wote
ambao wanakwamisha wakimbizi hao kurejea nchini kwao kwa hiari.
“Naagiza
uchunguzi ufanyike haraka iwezekanavyo kwa yeyote atakayehusika anakwamisha
zoezi hili la kuwarejesha wakimbizi hawa ambao wapo tayari kuondoka nchini kwao
kutokana na amani iliyopo, awe Afisa kutoka Wizarani, awe afisa wa shirika
lolote, awe yupo hapa kambini, lazima tutamkamata na kumpeleka mahakamani,”
alisema Lugola.
Aliongeza
kuwa, muda umefika kwa
wakimbizi wa Burundi kurudi nchini mwao, kwasababu zile sababu ambazo zilikuwa
zinazuia zoezi la kuwarudisha kwao wakimbizi hao kwa sasa havipo tena kwasababu
nchi hiyo ina amani.
Alisema Serikali ya Tanzania chini
ya Rais John Magufuli imejiridhisha sababu kubwa iliyowaleta wakimbizi hao wa Burundi
nchini ya kutowepo kwa amani haipo tena na kwamba kwa sasa Burundi ipo salama
kiulinzi na kiusalama pia kisiasa hivyo wakimbizi hao wanapaswa kurudi nchi
mwao wote bila kuwepo kikwazo chochote.
"Wanaosema Burundi haina amani
wanaipaka matope nchi hiyo kwani jambo hilo halina ukweli wowote na Tanzania
imefanya uchunguzi wa kutosha na kujiridhisha kuwa amani ya kudumu ipo nchini
humo, Oktoba Mosi tutaanza kutekeleza mkataba wa pande tatu wa kurudishwa kwa
wakimbizi 2000 kila wiki wa Burundi kwenda nchini mwao," alisema Lugola.
Naye Waziri Barandagiye, kwa upande wake alisema Burundi iko tayari kutekelezwa kwa
makubaliano ya pande tatu ya kuhakikisha wakimbizi wote wa Burundi wanaohifadhiwa
kwenye makambi mbalimbali ya wakimbizi mkoani nchini wanarudi Burundi lakini
wanashangazwa na namna Shirika la Kuhudumia Wakimbizi linavyoendesha zoezi hilo
kwa kasi ndogo.
Waziri
Lugola na Barandagiye walitembelea Kambi ya Nduta, Wiliyani Kibondo na Mtendeli
iliyopo Wilayani Kakonko mkoani humo, kwa lengo la kuhamasisha wakimbizi katika
kambi hizo kurejea nchini kwao kwa hiari.
No comments :
Post a Comment