Na WAJMW-Brazzaville
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amekutana na Waziri wa
Afya wa Marekani Amiral Brett Giroir na kufanya mazungumzo na kuona
namna gani nchi hizo mbili zinavyoweza kushirikiana katika kupambana na
ugonjwa wa Sickle Cell (Seli Mundu) hasa kwa watoto wachanga na wale
walio chini ya miaka mitano.
Waziri Ummy amemueleza Waziri huyo
kuwa watoto wapatao 11,000 wanazaliwa na ugonjwa huo Tanzania na wengi
hupoteza maisha kwa sababu ya kuchelewa kufanyiwa vipimo na kugundulika
mapema.
Waziri Ummy amemueleza kuwa
muelekeo wa nchi sasa ni kuhakikisha kuwa kila mtoto anayezaliwa
anapimwa Sickle Cell na watakaogundulika matibabu yaanze mapema ili
kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Mawaziri hao wamekubaliana kwa
pamoja kushirikiana katika kudhibiti vifo vinavyoweza kutokea kwa sababu
ya ugonjwa huo huku Waziri Amiral akiahidi kuimarisha upatikanaji wa
vipimo, pamoja na matibabu kwa watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo kuanzia
ngazi ya zahanati na vituo vyote vya kutoa huduma za afya ya msingi
nchini.
“Ni muhimu huduma hizi zikatolewa
katika ngazi ya afya ya msingi mpaka taifa ili kuwapa huduma stahiki
wananchi, hii ikiwa ni utekelezaji wa afya kwa wote. Suala la upimaji wa
Seli Mundu, elimu kwa jamii na pia suala la matibabu katika ngazi zote
za utoaji huduma ni muhimu vikapewa kipaumbele”. Aliongeza Waziri Ummy.

Hivi sasa huduma hii hapa nchini
inapatikana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufa za
Mikoa za Amana na Temeke pekee kwa nchi nzima.
Kwa upande wake Waziri Brett
amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kujenga
viwanda vya dawa nchini ikiwa ni pamoja na za Sickle Cell. Pia ameahidi
kutembelea Tanzania kuona na kujadiliana zaidi namna nchi hizi mbili
zitavyoshirikiana katika kushughulikia ugonjwa huu nchini.
Mawaziri hao wanahudhuria mkutano
wa 69 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaojumuisha Mawaziri wa Afya
toka nchi mbalimbali za Afrika unaoendelea jijini Brazzaville nchini
Jamhuri ya Kongo.
No comments :
Post a Comment