Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Mhe. Seleman Jafo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.
Adolf Ndunguru na Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Rora
Madete wakifuatilia kwa karibu maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tasisi ya
Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii, Dkt. Tausi Kida katika hafla ya uzinduzi wa
Mpango Kazi wa Uendelezaji Miji Tanzania, Dodoma.
Meza
kuu wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Mhe. Seleman Jafo, wakiwa katika picha ya pamoja baadhi ya washiriki
hafla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Uendelezaji Miji
Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dodoma.
Na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali
imezindua rasmi Mpango Kazi wa Uendelezaji Miji Tanzania ili
kuhakikisha nchi inakuwa na miji iliyopangwa na makazi yenye huduma zote
za kijamii ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa pili wa Taifa wa Maendeleo
wa miaka mitano 2016/17-2020/21.
Mpango
huo umezinduliwa Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo, katika ukumbi wa
Wizara ya Fedha na Mipango.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa Mpango kazi huo, Waziri Jafo alisema kuwa
Serikali imejidhatiti kuandaa mipango miji madhubuti ambayo imezingatiwa
katika miongozo ya kuandaa mipango ya taifa.
“Serikali
inazindua rasmi Mpango huo ili kuleta mpangilio mzuri wa Miji wenye
manufaa kwa Taifa na kufanya ukuaji wa miji kuwa mchakato wenye manufaa
ya kiuchumi na kijamii kwa nchi”, alisema Waziri Jafo.
Waziri
Jafo alisema kuwa mpango huo umejikita katika maeneo manne ambayo ni
matumizi ya lugha ya mpango kazi, suala la utawala na kanuni, mkakati wa
fedha pamoja na kuchunguza njia za kukuza uchumi kwa kutambua njia
ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi katika viwango vya juu.
Alisema
kuwa maeneo hayo manne ni muhimu kufanya ukuaji wa miji kuwa mchakato
wenye manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa kuwa unatoa mapendekezo ya
msingi kwa wakati ambayo ni muhimu kwa upangaji wa maendeleo ya miji
nchini.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.
Dkt. Angeline Mabula, alisema kuwa ukuaji wa miji ni suala pana ambalo
linahitaji wadau wengi kuunganisha juhudi ili kuhakikisha ukuaji wa miji
inayosimamiwa kikamilifu.
Dkt.
Mabula amesema kuwa, wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano katika
kuleta pamoja jitihada za kila taasisi ili kuepuka jambo moja kufanywa
na wadau zaidi ya mmoja, lengo likiwa kufanikisha malengo ya nchi
iliyojiwekea.
Naye
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolph Ndunguru,
aliwashukuru viongozi na wote waliohudhuria katika hafla hiyo muhimu kwa
Taifa na kueleza kuwa mpango huo utasaidia kutatua changamoto za
upangaji miji kwa maendeleo ya uchumi na Taifa kwa ujumla.
Vilevile
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa kiuchumi na Kijamii, Dkt.
Tausi Kida, amesema Mpango huo utasaidia katika uandaaji wa mipango ya
kitaifa ya uendelezaji miji pamoja na uandaaji wa sera kwa kuwa
uliotokana na utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii kwa
kuwa uliofanywa kwa kufuata kanuni za kisayansi za ufanyaji tafiti.
No comments :
Post a Comment