Thursday, August 1, 2019

MAREKANI YAMUWEKEA VIKWAZO WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA IRAN



Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema leo kuwa uamuzi wa Marekani kumuekea vikwazo Mohammed Javad Zarif inaonyesha kuwa Marekani inamuogopa mwanadiplomasia huyo mkuu.
Katika hotuba ya moja kwa moja ya televisheni, Rouhani amesema Marekani wanaogopa mahojiano yanayofanywa na waziri wa Iran wa mambo ya nchi za kigeni. Akimaanisha mahojiano ya karibuni aliyoyafanya Zarif na vyombo vya habari vya kigeni mjini New York.
Rouhani amesema wakati akiwa ziarani katika mji wa kaskazini magharibi wa Tabriz kuwa uamuzi huo wa Marekani ni wa "kitoto” na kizuizi kwa diplomasia. Utawala wa Trump umemuwekea vikwazo Javad Zarif, na hivyo kumfungia kabisa mlango mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.
Vikwazo hivyo vinazuia mali zozote za Zarif nchini Marekani au zinazodhibitiwa na makampuni ya Marekani. Serikali ya Washington imesema hatua hiyo itadhibiti safari zake za kimataifa.
Taarifa ya Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin imesema kuwa Zarif anatekeleza ajenda hatari ya kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, na yeye ndiye msemaji mkuu wa utawala wa Iran kote duniani. Marekani inatuma ujumbe wa wazi kwa utawala wa Iran kuwa tabia yake ya karibuni haikubaliki kamwe.
Zarif alijibu maramoja akiandika kwenye Twitter kuwa Marekani inajaribu kumyanyamazisha kwenye jukwaa la kimataifa. Akasema vikwazo alivyowekewa havitakuwa na athari yoyote kwake wala familia yake kwa sababu hana mali wala maslahi yoyote nje ya Iran.
Lakini katika ujumbe mwingine wa kukanganya kwa Tehran, Marekani imerefusha kwa siku 90, msamaha wake kwa miradi mitatu ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia ili kuepuka kuzikasirisha nchi nyingine zilizosaini makubaliano ya nyuklia ya 2015, ambazo ni China, Urusi, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.
Akizungumza jana, Zarif alisema Iran iko tayari kupunguza ahadi zake za mkataba wa nyuklia, kama washirika wa Ulaya hawatoilinda dhidi ya vikwazo vya Marekani kwa kuhakikisha kuwa inaweza kuuza mafuta na kupokea mapato.
Mbali na kujaribu kutwaa mali zake, Marekani pia itauminya uwezo wa Zarif kusafiri kimataifa kama mwanadiplomasia. Anatarajiwa kuendelea kuzuru Umoja wa Mataifa mjini New York, ijapokuwa chini ya udhibiti mkali.

No comments :

Post a Comment