
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio (kushoto)
akikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia
kuwaunganishia wateja wa viwanda maeneo ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, hivi
karibuni.
……………………………………………..
Na Veronica Simba – Dodoma
Serikali imebainisha kuwa
matumizi ya gesi asilia katika magari nchini yamezidi kukua
ambapo kwa
sasa idadi imefikia 210 kutoka 65 yaliyokuwa yakitumia nishati hiyo,
mwaka 2017.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James
Mataragio, jijini Dodoma, leo Agosti 21, 2019 wakati akiwasilisha
taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kuhusu hatua
zilizofikiwa katika kuandaa moduli ya miradi ya bei ya gesi asilia,
uuzaji na usambazaji wake majumbani na viwandani.
Akieleza zaidi, Dkt. Mataragio
amesema kuwa kutokana na ongezeko hilo, kituo cha majaribio kilichopo
Ubungo Dar es Salaam, kinashindwa kuhimili matakwa ya matumizi hivyo
shirika limejipanga kujenga kituo kikubwa eneo la Sam Nuyoma jijini
humo, ili kuondoa changamoto husika.
“Kituo hicho kinachotarajiwa
kukamilika Oktoba 2020, kitatumika kujazia gesi katika magari pamoja na
kupeleka gesi maeneo ambayo miundombinu ya mabomba ya gesi bado
haijafika, yakiwemo maeneo ya viwanda Kigamboni na Kibaha pamoja na
maeneo ya Feri na Muhimbili.”
Aidha, ameeleza kuwa, sambamba na
ujenzi wa kituo husika, shirika limetangaza fursa kwa kampuni binafsi
kuuza gesi kwa rejareja kwa watumiaji wa nishati hiyo katika magari
nchini.
Ameongeza kuwa, jumla ya shilingi
bilioni 16.6 zimetengwa kwa ajili ya vituo vya kuongeza mgandamizo wa
gesi (CNG) na kujazia gesi katika magari.
Ikiwa ni mwendelezo wa jitihada
za uwezeshaji matumizi ya gesi katika magari nchini, Dkt. Mataragio
amesema TPDC inalenga kuupatia gesi asilia mradi wa mabasi ya mwendokasi
(DART), ambapo kwa kuanzia, kituo cha kujazia gesi kwenye magari
kitajengwa eneo la DART, depoti ya Ubungo na kinatarajiwa kukamilika
Oktoba, mwakani.
Amesema, shirika limekubaliana na
DART kuwezesha kuweka vituo maalumu vya gesi katika depoti ya Gongo la
Mboto na Mbagala ili kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi ya DART
na kuongeza matumizi ya gesi asilia.
“Miundombinu hii pia itakuwa na
matoleo ya kuwezesha usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya viwanda
na majumbani katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam,” amesema.
Akizungumzia kuhusu mikakati
mingine inayofanywa na shirika hilo katika kuwezesha ongezeko la
matumizi ya gesi asilia nchini, Dkt. Mataragio amesema TPDC imepanga
kuendeleza miundombinu ya usafirishaji gesi asilia ikiwemo kujenga bomba
la gesi kutoka Tegeta hadi Bagamoyo katika eneo la viwanda.
Aidha, amesema shirika limepanga
kujenga bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Tanga ambalo litakuwa na
matoleo ya kwenda mikoa mingine pamoja na nchi za jirani kulingana na
Mpango kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Nchini (NGUMP).
Katika uwasilishaji huo wa
taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ujumbe wa
serikali uliongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
Wengine walioshiriki ni viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, TPDC na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara.
No comments :
Post a Comment