
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
SHEREHE
za wakulima maarufu kama Nane Nane zimetajwa kuwa ni darasa huru kwa
wakulima, wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla kwani zinatoa nafasi
kwao kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo kilimo chenye tija, Ufugaji wa
kisasa na Uvuvi wenye tija pasina kuharibu rasilimali za serikali.
Hayo
yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Methew J.
Mtigumwe wakati akizungumza na mtandao wa Wazo Huru Blog mara baada ya
kutembelea mabanda mbalimbali ya Maonesho ya Wakulima (Nanenane) Kitaifa
yanayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi kwenye Halmashauri ya Mji
wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Alisema
kuwa serikali inatambua kadhia inayowakabili wakulima nchini ikiwemo
pembejeo feki ambazo wakulima wanauziwa, hivyo kupata hasara ikiwamo
mazao kidogo na hafifu tofauti na kusudio lao la kujipatia mazao mengi
ya biashara na chakula jambo ambalo inalifanyia kazi ili kukabiliana
nalo kwa haraka.
Maonyesho
haya Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu
yatawasaidia wakulima kupata elimu juu ya pembejeo halisi ikiwamo mbegu,
dawa (viuatilifu), mbolea kutoka kwa mashirika husika yanayozalisha
pembejeo mbali mbali, ili kuwasaidia kuepuka kununua pembejeo feki
ambazo huwasababishia hasara na kuwakatisha tamaa.
Sherehe
hizi huambatana na maonyesho ya bidhaa za kilimo yanayofanywa na
wakulima na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya kilimo,
lengo likiwa ni kujitangaza shughuli zao, kubadilishana uzoefu na
wataalamu wa kilimo.
Pia
wakulima wadogo ambao ni wengi ukilinganisha na wakulima wakubwa
watajifunza mbinu mpya za kitaalamu za kilimo zinazoendana na wakati
uliopo kwa maana ya mabadiliko ya kiteknolojia na tabia nchi ili
wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa na kunufaika kiuchumi.
Mhandisi
Mtigumwe alisema kuwa Kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakilima kilimo
cha mazoea ambacho hakizingatii kanuni za kitaalamu, jambo
lililowasababisha kukata tamaa na kuona kuwa kilimo hakilipi kutokana na
mbinu duni walizozitumia.
Alisema
kuwa Wizara ya Kilimo inajipambanua zaidi kumkwamua mkulima ili
Wakulima nchini waondokane na kilimo cha kubahatisha cha kutegemea mvua
na badala yake wajikite katika kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha
uhakika, kinachoweza kuyabadilisha maisha yao kiuchumi kutokana na mazao
mengi watakayopata.
"Natambua
kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanategemea sekta ya kilimo
kama ajira yao Sehemu kubwa ya kilimo ni cha wakulima wadogo wadogo
ambao mashamba yao yana ukubwa wa hekta 0.9 na hekta 3.0 kwa kila moja,
Karibu asilimia 70 ya ardhi ya kilimo na mazao inalimwa kwa kutumia
jembe la mkono, asilimia 20 hutumia maksai na asilimia 10 hutumia trekta
Hivyo kama wizara tutajitahidi kadri iwezekanavyo kuwakwamua wananchi
ili kuondokana na uduni katika mavuno" Alisema Mtigumwe
Mbali
na hayo, kilimo cha Tanzania ni cha kutegemea mvua, uzalishaji wa mazao
ya chakula ndio unaongoza katika uchumi wa kilimo. Hekta milioni 5.1
zinalimwa nchi nzima kila mwaka, kati ya hizo asilimia 85 ni kwa ajili
ya mazao ya chakula tu, na wanawake ndio wafanyakazi wakubwa mashambani.
Mhandisi
Mtigumwe anasema katika maonesho hayo anatarajia wakulima watajifunza
mbinu bora na za kisasa za kilimo zitakazowawezesha kupata mazao mengi
na kuinua kipato chao.
Aidha
ametoa wito kwa wakulima na mashirika kujitokeza katika maonesho hayo
kwa sababu watapata fursa ya kujifunza mambo mengi na kubadilishana
uzoefu na wataalamu mbalimbali wa kilimo.
No comments :
Post a Comment