Wajumbe
wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya baraza la wawakilishi la Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar wakiwa katika ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali
ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yao ya
kuangalia huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi
hiyo leo jijini Dar es Salaam.Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wa wodi ya watoto Theresia Tarimo akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya baraza la wawakilishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar jinsi wanavyowahudumia watoto wanaolazwa katika wodi hiyo. Kushoto kwa Theresia ni Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman ambaye aliambatana na wajumbe hao ili kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wa chumba cha Cathlab Rogers Kibula akiwaelezea wajumbe wa kamati ya Ustawi wa Jamiii ya baraza la wawakilishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar jinsi upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua pamoja na uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo unavyofanyika katika kwa kutumia mtamo wa Cathlab wakati wa ziara ya wajume wa baraza hilo ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar
Harusi Said Suleiman akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi, Wajumbe
wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya baraza la wawakilishi Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na wafanyakazi wa JKCI mara baada ya wajumbe hao
kumaliza ziara yao ya kutembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma
za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Picha na JKCI
…………………..
Na Ales Mbilinyi – JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) imeiahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inatoa
elimu kwa wataalamu wa magonjwa ya moyo waliopo Hospitali ya Mnazi
mmoja ili wananchi wanaotibiwa katika Hospitali hiyo wapate huduma za
kisasa na za
utaalamu wa hali ya juu .
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alipokutana na wajumbe
wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la wawakilishi la Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar walipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona
huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa.
Prof. Janabi alisema Taasisi hiyo
imekuwa ikipokea wataalamu kutoka Hospitali mbalimbali hapa nchini
zikiwemo za Benjamini Mkapa, Bugando na KCMC ambao walijifunza jinsi ya
kuwatibu wagonjwa wa moyo kwa njia za kisasa na utaalamu wa hali ya juu
na baaada ya kumaliza mafunzo yao walikwenda kuyafanyia kazi katika
maeneo yao waliyotoka kitu ambacho kimesaidia wananchi kupata matibabu
ya moyo yanayoendana na wakati uliopo.
“Umefika wakati sasa uzoefu
walionao wataalamu wa afya wa JKCI ukatumika kuwafundisha wataalamu
wengine wa afya wakiwemo wa kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja. Kama
mtakuwa tayari watumeni wataalamu wenu waje kujifunza kwetu japo kwa
kipindi cha miezi mitatu nasi tutawafundisha utaalamu wote tulionao”.
“Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
iko tayari kushirikiana na Hospitali ya Mnazi mmoja kwa kutuma wataalamu
wake na kufanya matibabu ya pamoja kwa wagonjwa wa moyo wanaotiiwa
katika Hospitali ya Mnazi Mmoja”, alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye
pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema tangu kusainiwa kwa
mkataba wa kupokea wagonjwa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
jumla ya wagonjwa 26 wameshatibiwa katika Taasisi hiyo na hali zao
zinaendelea vizuri.
“Baada ya kusaini mkataba na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwishoni mwa mwaka jana tulianza
kuwapokea wagonjwa wa moyo kutoka Zanzibar. Hadi sasa wagonjwa 26
wamepata matibabu ya upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na bila
kufungua kifua, miaka ya nyuma wagonjwa hawa walikuwa wanapelekwa nje
ya nchi lakini hivi sasa wanatibiwa hapa nchini na wataalamu wetu”,
alisisitiza Prof. Janabi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo
mwenyekiti wa kamati ya Ustawi wa Jamii ya baraza la wawakilishi Mhe.
Mwanaasha Juma amesema kupitia ziara waliyoifanya katika Taasisi hiyo
wameweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatawasaidia katika
kuhakikisha huduma bora za matibabu ya moyo zinapatikana Zanzibar.
“Ujio wetu hapa utatuwezesha
kuendelea kutoa rufaa kwa wagonjwa wa moyo walipo Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kuja kutibiwa hapa JKCI badala ya kuwapeleka nje ya nchi
kupatiwa matibabu ambayo yanapatikana hapa hapa Tanzania. Kama kamati
tumeridhika na huduma zinazotolewa kwani tumejionea kwa macho yetu na ni
furaha kuwa wagonjwa wetu kutibiwa katika nchi yao kwa mazingira
waliyoyazoea,” alisema Mhe. Mwanaasha
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Afya Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman aliishukuru Taasisi hiyo kwa
mapokezi mazuri waliyowapatia na kuahidi wataendelea kushirikiana zaidi
katika kuhakikisha wananchi wanapata matibabu mazuri ili watoke hapo
walipo na kusonga mbele zaidi katika huduma za matibabu ya moyo.
Mhe. Harusi aliuomba uongozi wa
JKCI kuwapeleka mara kwa mara wataalamu wake katika hospitali ya Mnazi
Mmoja kwa ajili ya kufanya matibabu ya pamoja bila kuchoka ili mafunzo
yatakayotolewa yawe na tija kwa wataalamu hao na kwa wananchi waweze
kupata matibabu ya kibingwa.



No comments :
Post a Comment