Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiagana na
Afisa Mfawidhi wa Maabara ya Taifa ya Udhibiti Samaki na
Mazao ya Uvuvi Emanuel Mundoko wakati wa
oporesheni ya kufuatilia madeni ya kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa
Mawanza mwishoni mwa wiki.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akihakiki deni la kodi ya pango la ardhi la kampuni ya Jesse and Company
Ltd wakati wa oporesheni ya kufuatilia madeni ya kodi ya pango la ardhi
katika mkoa wa Mawanza mwishoni mwa wiki. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi
wa Jesse and Company ltd Sundeep Bachu.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akimpa maelekezo Meneja Rasilimali Watu wa kapmuni ya Synergy Tanzania
Ltd ( wa kwanza kulia) wakati wa oporesheni ya kufuatilia wadaiwa sugu
wa kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Mawanza mwishoni mwa wiki. Wa
kwanza kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizarani Denis Masami.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi
Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo (wa tatu kulia) akifafanua jambo kwa Meneja wa
Kampuni ya Ideal Development Ltd Burnanuddin Rajbhai (wa kwanza kushoto) wakati
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipoitembelea
kampuni ya Ideal Development Limited katika operesheni ya kufuatilia wadaiwa
sugu wa kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Mwanza mwishoni mwa wiki. Wa pili
kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Dorothy Mwanyika na wa pili kushoto ni
Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizarani Denis Masami.
Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amezidi kuzibana Taasisi
na Makampuni yenye madeni makubwa ya kodi ya pango la ardhi ambapo
ametua mkoani Mwanza na kuyabana makampuni na taasisi nane ambazo kwa
ujumla wake zinadaiwa zaidi ya milioni 900.
Kampuni
na taasisi alizotembelea Dkt Mabula ni Synergy Tanzania Ltd, Ideal
Development Ltd, Birchard Oil Ltd, Shule za Musabe, Taasisi ya Taifa ya
Utafiti Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Ndamavyo Auto Spares, Jesse &
Company Ltd na Maabara ya Taifa ya Udhibiti Samaki na Mazao ya Uvuvi.
Akizungumza
katika ziara yake hiyo ya kufuatilia madeni ya kodi ya pango la ardhi
mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
alisema ziara hiyo anayoifanya ya kuwafikia wale wenye madeni makubwa
inafuatia baadhi ya kampuni na taasisi zinazodaiwa kushindwa kulipa ama
kurekebisha madeni yao baada ya kikao cha Juni 11, 2019
kilichowakutanisha wadaiwa zaidi ya 200 jijini Dodoma
katika mwanzo wa ziara yake kwenye shule za Musabe, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alimueleza
mmiliki wa shule hizo Daniel Musabe kulipa deni lake la kodi ya pango
la ardhi linalofikia milioni 57.4 katika viwanja vyake vinne
anavyomiliki kufikia tarehe 31 Julai 2019 ili kuepuka kufikishwa katika
Baraza la Ardhi na Nyumba.
Hata
hivyo, Mmiliki wa Shule hizo ambazo ni za Chekechea, Msingi na
Sekondari alimueleza Dkt Mabula kuwa yuko tayari kulipa deni la kodi ya
pango la ardhi lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na changamoto za
kibiashara ambapo hata hivyo aliahidi kulipa kiasi anachodaiwa kuanzia
Agosti 2019 na kumaliza deni lote ifikapo Desemba 2019.
Akiwa
katika Kampuni ya Birchard Oil Limited, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula ambaye aliambatana na Mkuu wa Kitengo
cha Kodi Wizarani Denis Masami aliitaka kampuni hiyo kulipa kiasi
inachodaiwa cha kodi ya pango la ardhi inayofikia milioni 85,235,050
ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya kodi za miaka ya nyuma.
Meneja
uhusiano wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na uzalishaji Mafuta na
Marobota ya Pamba Arshad Jetha alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa
kampuni yake pamoja na kudaiwa kodi ya pango la ardhi kwa baadhi ya
viwanja inavyomiliki lakini baadhi yake alishalipia hivyo aliomba
kuhakikiwa madeni yake ili kupata deni halisi.
Ideal
Development Ltd kupitia Meneja wake Burnanuddin Rajbhai alikiri deni la
kodi ya pango la ardhi linalofikia milioni 79 na kuomba kupewa muda wa
kulipa katika awamu tatu tofauti. Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi
alizitaka kampuni na Taasisi zilizokubali kulipa madeni kuandika
barua ya kueleza namna zitakavyolipa na muda wa mwisho wa kulipa madeni
yao katika ofisi za ardhi za halmashauri husika na nakala za barua hizo
ziende ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda ya Ziwa.
Kamishna
Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo aliionya kampuni ya
Ideal Development Ltd kwa kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyofikia
ya kulipa deni lake na kuieleza kuwa hatua itakayofuata kwa kampuni hiyo
ni kufikishwa katika Baraza la Ardhi na suala la kuingia makubaliano ya
malipo haliwezi kufanyika kwa mara ya pili.
Kampuni
ya Synergy Tanzania Ltd Kupitia kwa Meneja Utawala wake Florence
Kivamba iliahidi kuandika barua ya makubaliano ya kulipa deni la milioni
43 inayodaiwa ingawa alioamba kufanya mawasiliano na uongozi wa juu kwa
kuwa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi ilikuwa ya kushtukiza na uongozi
haukuwepo.
Akiwa
katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Naibu
Waziri wa Ardhi Dkt Mabula aliueleza uongozi wa Taasisi hiyo kuwa
inadaiwa jumla ya shilingi milioni 515,713,900 ya kodi ya pango la ardhi
na taasisi hiyo haijawahi kulipa kodi hiyo tangu mwaka 1996.
Mkurugenzi
wa NIMR mkoa wa Mwanza Safari Kinuhi alijitetea kwa kueleza kuwa
taasisi yake inapaswa kusamehewa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa
haiko kibiashara bali inatoa huduma kwa wananchi na kuboresha afya
ingawa aliahidi kuwasiliana na uongozi wa juu kuhusiana na suala hilo.
Hata
hivyo, Dkt Mabula alimueleza kuwa Taasisi yake inapaswa kufuata sheria
wakati wa kuomba kusamehewa kodi ya pango la ardhi huku Mkuu wa Kitengo
cha Kodi Wizarani Denis Masami akisisitiza kuwa hata kama Taasisi hiyo
itasamehewa kulipa kodi hiyo lakini deni la nyuma lazima lilipwe kwa
kuwa sheria ya msamaha itaanza pale tamko la msamaha lilipotoka.
Maabara
ya Taifa ya Udhibiti Samaki na Mazao ya Uvuvi iliyopo eneo la Nyegezi
ilionekana kutokuwa na hati ya eneo inalomiliki ingawa Afisa Mfawidhi wa
Taasisi hiyo Emanuel Mundoko alijitetea kwa kueleza kuwa awali Taasisi
hiyo ilikuwa sehemu ya chuo cha Uvuvi na sasa inajitegemea hivyo hawajui
madeni halisi wanayodaiwa.
No comments :
Post a Comment