Sunday, July 14, 2019

JENGO LA TATU LA ABIRIA (TBIII) KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA JULIUS NYERERE DAR ES SALAAM KUANZA KUTUMIKA MWEZI UJAO: NDITIYE


Naibu Waziri  wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi) Mhandisi  Atashasta Nditiye, amesema Ujenzi wa Jengo la  tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha  Julius Nyerere (JNIA) umekamilika,  na Jengo linatarajiwa kuanza uendashaji  mwanzoni mwa mwezi  Agosti  mwaka huu.
Pia amesema amefurahishwa  kwa  kukamilika kwa jengo hilo  ambapo  ni la  kisasa na huduma zake zake ni nzuri.
Akizungumza mara  baada ya Ziara ya kukagua Jengo hilo , amesema katika idadi ya miruko ya ndege Barani Afrika  JNIA inachukua nafasi ya tano  na nafasi ya sita kwa idadi ya abiria.
‘’ Nimefurahishwa kwa kukamilika kwa Ujenzi wa jengo la tatu la abiria wa  Kiwanja cha Ndege ambapo utakapoanza kuhudumia abiria natarajia tutachukua nafasi nzuri zaidi Barani Afrika kwani ni Jengo la kisasa na litatoa huduma nzuri,’’ alisema.
Nae Mkurugenzi  wa Kiwanja cha Ndege cha  Kimataifa cha Julius Nyerere( JNIA),  Paul  Rwegasha akitoa ufafanuzi wa Kiwanja hicho, alisema  mara baada ya kukamilika kwa jengo la tatu itakuwa jumla ya majengo matatu  yanaweza kuhudumia abiria milioni nane kwa mwaka.
Rwegesha alisema  ujenzi wa jengo la kwanza lina uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka na ujenzi wa jengo la  pili abiria  milioni 1.5
Alisema kukamilika kwa jengo hilo la tatu kutaongeza idadi ya Ndege, abiria pamoja na Watalii baada ya kuwa na Miundombinu  bora na ya kisasa.
Vile vile alisema Ujenzi wa jengo  la  tatu ni kwa ajili ya abiria wa safari za Kimataifa ambapo kwa sasa yako mashirika  23 na  jengo la   pili kwa ajili ya abiria wa safari za   ndani ya nchi   huku jengo la  kwanza  safari za ndani pia. .
Alisema ujenzi wa jengo la tatu la abiria  litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 2,800, kwa saa na maegesho ya magari mchanganyiko yasiopungua 2,075 kwa wakati mmoja.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama, alisema kwasasa kuna  katika maandalizi ya Wakuu wa Nchi na Serikali watakaohudhuria mkutano wa 39 wa SADC  ambapo maadalizi yameambatana na ukarabati wa maboresho ya miundombinu  na samani.
Ndyamukama, alisema wageni hao wanatarajia kuingia hapa nchini Agosti mwaka huu ambapo  watapata   huduma bora zaidi  na yenye uhakika.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Viwanja vya Ndege Tanzania Mhandisi Julius Ndyamukama (mwenye koti jeusi)akisoma Taarifa ya Mradi wa Jengo la III la abiria kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye alipofanya ziara katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye akihoji jambo katika Ukumbi wa Watu mashuhuri alipotembelea jengo la III la abiria.


Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere Bw, Paul Rwegasha ( mwenye koti kijivu) Akitoa maelezo ya jengo la mizigo linalokarabatiwa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye wakati alipofanya ziara katika Kiwanja hicho.

No comments :

Post a Comment