Friday, July 19, 2019

Fahamu chimbuko la hifadhi ya jamii, umuhimu wake


Wanachama na wadau wa mfuko wa PSSSF kwa watumishi wa umma wakielekezwa kuhusu hifadhi ya jamii kwa wote. (Na Mpigapicha Wetu).

Na Christian  Gaya. Majira Ijumaa 19.Julai.2019
 Hifadhi ya jamii ni mfumo wa jamii ambao umekuwapo tangu mwanzo wa mwanadamu. Tangu enzi za kale, jamii zote zimekuwa na taratibu mbali mbali za kuhakikisha ya kwamba kila mtu anakuwa na uhakika wa kuishi maisha yake katika mazingira yoyote yanayoweza...
kumkwaza kuishi kama vile  majanga ya maradhi,  ulemavu na ya uzee.
 Hifadhi ya jamii ina maana ni aina ya hatua madhubuti au shughuli zilizobuniwa za kuhakikisha kuwa wananchi wa jamii hiyo wanapata mahitaji yao ya lazima na ya msingi  na wanapewa kinga ya hifadhi ya kutokana na majanga ili kuwawezesha kuwa na kiwango cha maisha ya kuishi kulingana na mila na desturi za jamii.
 Malengo ya hifadhi ya jamii ni kumwezesha mwananchi kuishi maisha yenye staha kwa kuwawezesha kupata huduma za msingi pale wanapokuwa hawana kipato kutokana na sababu mbalimbali zinatokana na uzee, kifo, ugonjwa, uzazi na kadhalika
 Wazee, watoto, yatima, wajane, na wagonjwa ambao kutokana na hali zao hawawezi kujikimu ni baadhi ya makundi ambayo yamekuwa yakipata kinga maalumu tangu enzi hizo hadi sasa, kama sehemu ya mfumo wa jamii ya mwanadamu duniani kote.
 Jamii ilikuwa inahakikisha kuwa vikundi hivyo vya watu wasiojiweza wanapata hifadhi ya jamii kwa maana ya msaada wa chakula, malazi na matibabu.
 Ili kuweza kutoa hifadhi hiyo jamii ilijiwekea taratibu na kanuni ambazo ilibidi zifuatwe kabla ya mtu hajapewa hifadhi kwa nia ya kuhakikisha kuwa ni wale tu wanaohitaji msaada ndiyo wanaopata. Na utaratibu mpaka leo unafanyika ndani ya jamii za Kitanzania na penginepo pale hapa Afrika na hata Ulaya.
 Hifadhi ya jamii ni haki ya msingi ambayo kila mtu anastahili kupata kutoka katika jamii. Jamii zilijiwekea utaratibu na sheria ambazo hutumika kuhakikisha jamii inapoondokana na utegemezi.
 Sheria ya kwanza kabisa kutungwa na kuandikwa kuhusu hifadhi ya jamii ilikuwa in ile sheria ya kusaidia maskini huko uingereza iliyotungwa karne ya 16. Sheria hiyo ilifuatiwa na nyingine iliyotungwa mwaka 1883 kwa ajili ya matibabu.
 Baadaye nchi nyingi hasa za ulaya zilianza kutunga sheria mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha mifumo ya hifadhi ya jamii. Na hiyo ilitokana na mapinduzi ya viwanda yaliyo tokea ulaya wakati huo, ambapo watu wengi walikimbilia mijini kutoka mashambani kwa kazi ya kuajiriwa viwandani.
 Hivyo misingi ya kusaidiana kifamilia kwa watu wa mashambani, kifamilia kwa watu wa mashambani ikaanza kupotea. Kwa sababu nguvukazi yote iliyokuwa ukitoa huduma katika koo mbalimbali iliishia kwenda mijini kwenda kufanya kazi. 
Lakini ikumbukwe kuwa hifadhi ya jamii ilitolewa na mpaka sasa bado inatolewa ndani ya jamii mbalimbali za kiafrika ingawa kiwango chake kila siku kinakwenda kikipungua hasa kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii duniani.
 Na ndiyo maana wazee wengi wana imani hata ya kuzaa watoto wengi zaidi kama hifadhi yao ya jamii ya sasa na ya baadaye ingawa lengo kubwa ni kuendeleza ukoo na kufanya kuwa ni wajibu kuwa na watoto.
 Watu wanateuliwa kubaki na wazee na wale wengine wasiojiweza ili kuwapa hifadhi ya jamii. Hata wakunga wa jadi tunao mpaka sasa ambao hutoa huduma za hifadhi ya jamii kwa akina mama wajawazito na wanapojifungua.
 Watoto waliofiwa na wazazi wao wana ukoo waligawana na kuwapa hifadhi ya jamii mpaka wanapofikia umri wa kujitegemewa na yule anayesoma anapewa hifadhi mpaka anapomaliza elimu ya juu. Huo ni utaratibu ambao unawekwa na wanajamii hasa ndani ya koo mbalimbali. Na tumeona aina hii ya hifadhi ya jamii inaendelea kufanyiwa kazi na baadhi ya jamii.
Tumeona mara nyingi karibu mikoa yote hapa nchini huduma ya kupatiwa msaada wa mazishi unapotolewa ndani ya vikundi mbalimbali. Na watu sasa wamegundua kuwa njia nzuri ya hifadhi ya jamii ni kwa ile isiyokuwa rasmi ambapo kuna vikundi mbalimbali vya kufa na kuzikana, kuweka na kukopa, ambapo wanachama wake hutokana na mkoa au wilaya anakotoka.
 Na hata viongozi wakuu wa mashirika ya umma, mashirika yasiyo ya kiserikari, na wa serikali wamekuwa wanachama wachagiaji wakubwa kwenye mifuko hii isiyo rasmi.
Na hii imeleta changamoto kubwa kwa hifadhi za jamii zilizo rasmi kama vile mashirika ya hifadhi ya jamii yaliyopo hapa nchini na sehemu zingine za kiafrika. 
 Kwa kawaida anayetakiwa kuwajibika kutoa hifadhi ya jamii kwa wazee, walemavu, wategemezi, na kwa watu wasio na kazi ni serikali na jamii ya kitanzania kwa ujumla.
Hifadhi ya jamii ina maana ni aina ya hatua madhubuti au mfuko uliobuniwa kama vile wa PSSSF wa  kuhakikisha kuwa wananchi wa jamii hiyo wanapata mahitaji yao ya lazima na ya msingi  na wanapewa kinga ya hifadhi ya kutokana na majanga ili kuwawezesha kuwa na kiwango cha maisha ya kuishi kulingana na mila na desturi za jamii.
 Serikali kupitia sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma namba 2 ya mwaka 2018 ilifuta mifuko ya hifadhi ya jamii ya PPF, PSPF, LAPF, na GEPF na kuanzisha mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wote wa umma yaani PSSSF.
Inaendelea wiki ijayo

No comments :

Post a Comment