UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kutokana na
taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, naomba kutoa hoja kwamba, sasa
Bunge lako lipokee na kujadili mapitio ya utekelezaji wa Mpango na
Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2018/19 pamoja na
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/20. Aidha,
naomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi zilizo chini yake
pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa mwaka 2019/20.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia uhai na afya njema
na kutuwezesha kukutana tena kushiriki mkutano huu wa Bunge unaojadili
Bajeti ya mwaka 2019/20, ambayo ni ya Nne tangu Serikali ya Awamu ya
Tano ilipoingia madarakani.
3. Mheshimiwa Spika, kwa
namna ya pekee, napenda nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa
Viongozi Wakuu wa Serikali, nikianza na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kwa miongozo yao iliyojaa hekima na uzalendo. Ni dhahiri
kwamba, katika kipindi cha takriban miaka mitatu na nusu ya uongozi wao,
tumepata mafanikio mengi ambayo kila mmoja wetu anapaswa kujivunia.
Naomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwajalia afya njema ili dhamira zao za
dhati za kuwaletea watanzania maendeleo ziendelee kuleta manufaa kwetu
na kwa vizazi vijavyo.
4. Mheshimiwa Spika, napenda
pia nitumie fursa hii, kuwapongeza sana Mhe. Balozi Dkt. Augustine
Philip Mahiga (Mb.), kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria,
pamoja na Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Kabudi (Mb.), kwa kuteuliwa
kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Nawaahidi ushirikiano wa hali ya juukatika kutekeleza majukumu yetu ya kumsaidia Mhe. Rais ili shughuli za Serikali ziendelee kufanyika kwa ufanisi zaidi.
5. Mheshimiwa Spika, napenda
kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa
kuendesha vizuri majadiliano ya Bajeti za Wizara mbalimbali. Aidha, napenda
kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe.
George Boniface Simbachawene (Mb) na Makamu Mwenyekiti Mhe. Mashimba
Mashauri Ndaki (Mb) kwa kuongoza vizuri majadiliano ya Kamati. Vilevile,
nawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti kwa michango yao mizuri
ambayo inatusaidia sana katika kutekeleza majukumu ya Wizara kwa
ufanisi. Aidha, Wizara inaahidi kuendelea kuzingatia maoni na ushauri
kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wote wakati wa kujadili taarifa hii ya
utekelezaji wa Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2018/19 na Mpango na
Bajeti ya mwaka 2019/20.
6. Mheshimiwa Spika, napenda
kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba
Kijaji (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, kwa msaada mkubwa na
ushirikiano anaonipatia katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya
Wizara. Aidha, nawashukuru Bw.
Doto M. James, Katibu Mkuu HAZINA na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Naibu
Makatibu Wakuu Bi. Amina Kh. Shaaban, Dkt. Khatibu M. Kazungu na Bw.
Adolf H. Ndunguru kwa kusimamia shughuli za kiutendaji za Wizara kwa
ufanisi. Vilevile, nawashukuru Makamishna, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi
zilizoko chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wakuu wa Vitengo na wafanyakazi wote wa Wizara, kwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
7. Mheshimiwa Spika, baada
ya maneno haya ya shukrani, naomba nijielekeze katika hoja yangu yenye
maeneo makuu mawili ambayo ni: mapitio ya utekelezaji wa Mpango na
Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2018/19 na Mpango na Bajeti kwa mwaka
2019/20.
8. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2018/19, bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango
inatekelezwa katika mafungu nane ya kibajeti ambayo ni: - Fungu 50 -
Wizara ya Fedha na Mipango; Fungu 21 - HAZINA; Fungu 22 - Deni la Taifa;
Fungu 23 - Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 7 - Ofisi ya Msajili wa
HAZINA; Fungu 10 - Tume ya Pamoja ya Fedha; Fungu 13 - Kitengo cha
Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 45 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2018/19
9. Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa
viwanda na kuwaletea Watanzania maendeleo inafikiwa, Wizara iliandaa
Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/19 kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya
kitaifa, kikanda na kimataifa ambayo ni pamoja na: Dira ya Maendeleo ya
Taifa ya 2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17-
2020/21, Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti 2018/19, Sheria ya Bajeti
Na.11 ya Mwaka 2015, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015,
Agenda ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika 2063 na Malengo ya Maendeleo
Endelevu ya mwaka 2030. Aidha, Mpango na Bajeti ulizingatia ahadi na
maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya uzinduzi
wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ushauri na maoni ya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja na Sera mbalimbali za
Serikali.
Mapatona Matumizi ya Wizara kwa Mwaka 2018/19
10. Mheshimiwa Spika, Muhtasari
wa mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2018/19 ni kama
inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 6 hadi ukurasa wa 9.
UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU
11. Mheshimiwa Spika, napenda
sasa nitumie fursa hii kulieleza Bunge lako tukufu kuhusu majukumu
yaliyotekelezwa na Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake kwa
kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi kufikia Aprili 2019 ambayo yameainishwa katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 9 hadi ukurasa wa 124.
Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla
12. Mheshimiwa Spika, malengo
ya uchumi jumla kwa mwaka 2018/19 yalikuwa: kuhakikisha Pato la Taifa
linakua kwa asilimia 7.2 mwaka 2018; mfumuko wa bei unabaki katika wigo
wa tarakimu moja; mapato ya ndani yanafikia asilimia
15.8 ya pato la Taifa; na mapato ya kodi yanafikia asilimia 13.6 ya
Pato la Taifa na nakisi ya bajeti inafikia asilimia 3.2.
13. Mheshimiwa Spika, uchumi
wa nchi yetu umeendelea kuimarika ambapo mwaka 2018, Pato la Taifa kwa
kutumia bei ya kizio ya mwaka 2015 lilikua kwa asilimia 7.0
ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2017. Sekta zilizokua kwa kasi
kubwa ni pamoja na Sanaa na Burudani (asilimia 13.7), ujenzi (asilimia
12.9), usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 11.8) na habari na
mawasiliano (asilimia 9.1). Ukuaji
huu wa uchumi umeenda sambamba na utolewaji wa huduma bora kwa wananchi
zikiwemo maji, afya, umeme, elimu na ujenzi wa miundombinu ya reli,
bandari, viwanja vya ndege, madaraja na barabara pamoja na kuimarisha
usafiri wa anga.
14. Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei umeendelea kushuka na kubakia katika
kiwango cha tarakimu moja. Kwa mwezi Aprili 2019, mfumuko wa bei
ulikuwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na asilimia 3.8 kwa kipindi kama
hicho mwaka 2018. Hali
hii imetokana na kuimarika kwa upatikanaji wa chakula katika masoko ya
ndani na nchi jirani, kutengamaa kwa bei za mafuta katika soko la dunia,
usimamizi madhubuti wa Sera za bajeti na fedha na utulivu wa thamani ya
shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine. Utulivu
huu wa bei umesaidia wazalishaji, wanunuzi na walaji kuweka mipango na
mikakati ya muda mrefu bila kuhofia mabadiliko ya mara kwa mara ya bei
ya malighafi na bidhaa.
Uandaaji na Ufuatiliaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa
15. Mheshimiwa Spika, Wizara
imefanikiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi 102 ya maendeleo kati ya
179. Miradi iliyofuatiliwa ilijumuisha sekta za Viwanda, Maji, Kilimo,
Nishati, Uvuvi, Afya, Elimu, Madini, Sheria, Ujenzi na Uchukuzi.
Ufuatiliaji huo umesaidia kurekebisha upungufu uliojitokeza katika
utekelezaji na kuainisha hatua za kuzingatiwa katika kutayarisha mpango
wa mwaka 2019/20.
Kusimamia Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali
Mapato ya Kodi na Yasiyo ya Kodi
16. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2018/19, Wizara ilipanga kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani
yakijumuisha mapato ya Halmashauri ya jumla ya shilingi trilioni 20.89.
Kati ya hizo, mapato ya kodi yalikuwa shilingi trilioni 18.0,
Halmashauri shilingi bilioni 735.6 na mapato yasiyo ya kodi shilingi
trilioni 2.16. Hadi
kufikia Aprili 2019, mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri
yalifikia shilingi trilioni 15.46. Kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi
yalikuwa shilingi trilioni 12.9, sawa na asilimia 87.4, mapato yasiyo ya
kodi shilingi trilioni 2.04, sawa na asilimia 122 na mapato ya
Halmashauri shilingi bilioni 529.25, sawa na asilimia 72 ya lengo la
kipindi hicho.
17. Mheshimiwa Spika, kati ya mapato yasiyo ya kodi ya kiasi cha shilingi trilioni 2.04 yaliyopatikana hadi kufikia Aprili 2019, jumla ya shilingi bilioni 600.45 zimekusanywa na Wizara ya fedha na Mipango, sawa na asilimia 100.44
ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 597.81. Mafanikio haya
yametokana na kuimarishwa kwa ufuatiliaji na usimamizi wa mashirika,
kampuni na taasisi za umma ambazo Serikali imewekeza.
18. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuleta uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, Wizara ilipanga kuunganisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali 300 kwenye Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli (Government e- Payment Gateway - GePG). Hadi kufikia Aprili 2019, jumla ya Taasisi 210 zimeunganishwa kwenye mfumo wa GePG ikiwa ni asilimia 70 ya lengo. Aidha, hadi sasa jumla ya taasisi 410 kati ya taasisi 667 zimeunganishwa na zinakusanya mapato kupitia mfumo huu. Mfumo
huu unaiwezesha Serikali kuona moja kwa moja miamala ya ukusanyaji wa
mapato na kujua kiwango cha mapato kinachokusanywa kwa siku.
Misaada na Mikopo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo
19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara ilipanga kuratibu upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu ya kiasi cha shilingi trilioni 2.67
kutoka kwa washirika wa Maendeleo ili kugharamia miradi mbalimbali ya
maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili 2019, misaada na mikopo ilifikia
shilingi trilioni 1.70, sawa na asilimia 86 ya lengo la kipindi hicho.
Mikopo ya Ndani na Nje yenye Masharti ya Kibiashara
20. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2018/19, Wizara ilitarajia kuratibu upatikanaji wa mikopo ya
ndani na nje yenye masharti ya kibiashara ya jumla ya shilingi trilioni
8.90. Kati ya hizo, shilingi trilioni 3.11 ni mikopo ya nje, shilingi
trilioni 1.19 ni mikopo ya ndani na shilingi trilioni 4.60 ni mikopo ya
ndani ya kulipia hatifungani zilizoiva (rollover). Hadi kufikia Aprili,
2019 kiasi cha shilingi bilioni 692.30 kilikopwa kutoka nje na shilingi
trilioni 3.3 zilikopwa kutoka soko la ndani zikijumuisha malipo ya
dhamana za Serikali zilizoiva (rollover).
Usimamizi wa Deni la Serikali
21. Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia Aprili, 2019 Deni la Serikali liliongezeka na kufikia shilingi
trilioni 51.03 kutoka shilingi trilioni 49.86 Aprili 2018. Ongezeko hilo
ni sawa na asilimia 2.35. Kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilikuwa
shilingi trilioni 13.25 na deni la nje lilikuwa shilingi trilioni 37.78.
Ongezeko la Deni la Serikali linatokana na kupokelewa kwa mikopo mipya
kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa
Jengo la tatu la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa, Ujenzi wa miradi ya umeme na Ujenzi wa barabara na madaraja makubwa.
22. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kufanya tathmini ya Deni la Taifa kila mwaka ili kupima
uhimilivu wake. Matokeo ya tathmini iliyofanyika Desemba, 2018 inaonesha
kuwa, Deni la Taifa ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati
na mrefu. Tathmini hiyo ilionesha kuwa: uwiano wa thamani ya sasa ya
Deni la Taifa (Present Value of Total Public Debt) kwa Pato la Taifa ni
asilimia 27.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70; thamani ya sasa ya
Deni la nje pekee (Present Value of External Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 22.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; thamani ya sasa ya
deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 157.3 ikilinganishwa na ukomo
wa asilimia 240; na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa
nje ni asilimia 15.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23.
23. Mheshimiwa Spika,
Serikali ilitenga kiasi cha shilingi trilioni 1.41 kwa ajili ya kulipa
riba ya deni la ndani. Hadi kufikia Aprili, 2019 kiasi cha shilingi trilioni 1.06
kimelipwa sawa na asilimia 75.18 ya lengo. Aidha, Serikali ilitenga
shilingi bilioni 689.67 kwa ajili ya kulipa riba ya deni la nje. Hadi
kufikia Aprili, 2019 shilingi bilioni 588.30 zimelipwa sawa na asilimia
85.30 ya lengo. Vilevile, Serikali ilitenga shilingi trilioni 1.66 kwa
ajili ya kulipia mtaji wa deni la nje, ambapo hadi kufikia Aprili, 2019
shilingi trilioni 1.23 zimelipwa sawa na asilimia 74.10 ya lengo. Wizara
itaendelea kusimamia Deni la Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo,
Dhamana na Misaada SURA 134 pamoja na Mkakati wa Muda wa kati wa
Kusimamia Madeni.
Malipo ya Pensheni na Michango ya Mwajiri kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
24. Mheshimiwa Spika, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi trilioni 1.19 kwa ajili ya kulipia mchango wa mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hadi kufikiaAprili,
2019 kiasi cha shilingi bilioni 797.29 sawa na asilimia 67.0 ya lengo
kililipwa ikiwa ni uwasilishaji wa michango ya mwajiri kwa watumishi
wote wa Umma walio kwenye “Payroll” ya Serikali na kwa wakati.
25. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2018/19, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 424.74 kwa
ajili ya kulipa mafao ya Kustaafu na mirathi kwa wastaafu wanaolipwa na
HAZINA. Hadi kufikia Aprili 2019, kiasi cha shilingi bilioni 314.92 sawa
na asilimia 74.14 kilitumika kulipa Wastaafu 4,016, Mirathi ililipwa
kwa Warithi 854 na Pensheni kwa kila mwezi kwa Wastaafu 57,055. Katika
kurahisisha ulipaji wa mafao ya wastaafu, Serikali imetengeneza mfumo wa
ukokotoaji wa Mafao, uhifadhi wa kumbukumbu pamoja na utoaji wa
Vitambulisho vya kielektroniki kwa kutumia mfumo wa TPPS (Treasury
Pensioners Payment System).
Kubuni na Kusimamia Mifumo ya Taarifa za Fedha
26. Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kubuni mfumo wa ufuatiliaji wa Mali za Serikali ujulikanao kama Government Asset Management Information System-GAMIS kwa ajili ya kurahisisha usimamizi na udhibiti wa Mali za Serikali. Aidha, Wizara imebuni na kuanza kutengeneza mfumo wa usimamizi wa fedha za miradi ya Maendeleo kutoka kwa washirika wa maendeleo zinazopelekwa moja kwa moja kwa
watekelezaji (Direct to Projects Funds) ambao unatarajiwa kuanza
kutumika Julai, 2019. Lengo ni kutambua miradi yote na kuweka uwazi
kuhusu fedha zinazotolewa na Washirika wa Maendeleo bila kupitia Mfuko
Mkuu wa Serikali.
27. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa chini ya usimamizi wa mifumo ya taarifa za fedha ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 24 hadi ukurasa wa 28.
Kuandaa na kufuatilia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali
28. Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatoa huduma bora kwa
Wananchi, Wizara imeendelea kuzijengea uwezo kwa kuzipatia fedha za
kutekeleza miradi ya kimkakati ili ziweze kujitegemea kimapato na
kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali Kuu.
Katika mwaka 2018/19, Wizara imefanya uchambuzi wa Miradi ya Kimkakati
111 yenye thamani ya shilingi bilioni 749.63 kutoka kwenye Halmashauri
67 kwa ajili ya kuzingatiwa katika bajeti ya 2019/20. Matokeo ya
uchambuzi huo ni kuwa jumla ya miradi 15 yenye thamani ya shilingi
bilioni 137.38 kutoka kwenye Halmashauri 12 ilikidhi vigezo na mikataba
kusainiwa. Orodha ya Halmashauri na idadi ya Miradi ni kama ifuatavyo:
Halmashauri ya Jiji la Tanga mradi mmoja na Halmashauri ya Jiji la
Mwanza miradi miwili; Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni miradi
miwili, Kigamboni mradi mmoja, Iringa mradi mmoja, Ilemela miradi
miwili; Halmashauri ya Mji wa Tarime mradi mmoja; Halmashauri ya Wilaya
ya Bagamoyo mradi mmoja, Biharamuro mradi mmoja, Kibaha mradi mmoja na
Hanang mradi mmoja.
29. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu kuandaa na kufuatilia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 28 hadi ukurasa wa 32.
Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Fedha za Umma
30. Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, imefanya uhakiki wa madeni
ya malimbikizo ya mishahara katika Wizara, Idara zinazojitegemea na
Wakala wa Serikali 142; Sekretarieti za Mikoa 24 na Mamlaka ya Serikali
za Mitaa 185. Aidha, Wizara imeendelea kuhakikisha
usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma zinazotolewa kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kufanya
ukaguzi maalum katika Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Hospitali ya
Taaluma na
Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Kampasi ya
Mloganzila, ambapo mapendekezo ya ukaguzi yaliwasilishwa kwa taasisi
husika kwa ajili ya kuyafanyia kazi ili kuleta ufanisi katika
utekelezaji wa miradi.
31. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika kusimamia na kudhibiti Matumizi ya Fedha za Umma ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 33 hadi ukurasa wa 35.
Usimamizi wa Mali za Serikali
32. Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya
uhakiki wa mali na madeni katika taasisi zilizounganishwa ambazo ni
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (PSPF, GEPF, PPF na LAPF) na mamlaka za maji
Dar es Salaam (DAWASA na DAWASCO). Baada ya utambuzi wa mali na madeni
ya taasisi hizo, Serikali itahakikisha kuwa inachukua hatua stahiki
kulingana na matokeo ya uhakiki. Wizara pia imefanya uhakiki wa majengo
yaliyobaki wazi Jijini Dar es Salaam baada ya Serikali kuhamishia shughuli zake
Jijini Dodoma kwa lengo la kuandaa utaratibu wa kugawa majengo hayo kwa
baadhi ya Taasisi za Serikali ambazo zina uhitaji wa majengo hayo.
33. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika Usimamizi wa Mali za Serikali ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 35 hadi ukurasa wa 37.
Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi
34. Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu (FIU) imeendelea kusimamia
utekelezaji wa Sheria za Udhibiti wa Fedha Haramu kwa kutekeleza
majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kupokea na kuchambua taarifa 1,305 za miamala shuku kutoka kwa watoa taarifa na kuwasilisha taarifa fiche 32 kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji
wa sheria kwa ajili ya uchunguzi; kupokea taarifa 5,536 zinazohusu
usafirishaji fedha taslimu na hati za malipo mipakani; kuratibu na
kusimamia zoezi linaloendeshwa na ESAAMLG la tathmini ya mifumo ya
udhibiti wa fedha haramu (AML/CFT Mutual Evaluation); kuimarisha
ushirikiano na FIU za nchi za
Djibouti, Sudan, Ethiopia, Somalia, China (Taiwan) na Mauritius na pia
kufanya majadiliano ya kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na FIU
za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamaica, Japan, Trinidad and
Tobago, Botswana, Canada, Jamhuri ya Kongo na Kazakhstan. Aidha, Kitengo
cha Kudhibiti Fedha Haramu imekagua benki nne ili kujiridhisha na
utekelezaji wa Sheria za Udhibiti wa Fedha Haramu.
35. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 37 hadi ukurasa wa 39.
Tume ya Pamoja ya Fedha
36. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Pamoja ya Fedha umeoneshwa kuanzia ukurasa wa 39 hadi ukurasa wa 40.
Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19,
Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali imefanya Ukaguzi Maalum katika Kampuni 34 ambazo
Serikali ina umiliki wa hisa chache. Aidha, Ofisi ya Msajili wa Hazina
imeandaa Mpango Kazi wa kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa katika
ripoti ya ukaguzi na utekelezaji unaendelea. Utekelezaji wa Mpango Kazi
unajumuisha kupitia mikataba ya ubia, uendeshaji na utaalam kwa kampuni
husika. Lengo kuu la zoezi hili ni kubaini sababu za Serikali kupata
kiwango kidogo cha gawio au kutopata kabisa na kuchukua hatua stahiki
ili kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, ufuatiliaji wa madeni kwa
wawekezaji waliobainika kutomaliza kulipa bei ya ununuzi wa kampuni hizo
unaendelea.
38. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 40 hadi ukurasa wa 47.
Uratibu wa Mikakati ya Kupunguza Umaskini
39. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2018/19, Wizara imefanya uchambuzi wa awali wa Utafiti wa
Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi 2017/18 ambao, unaonesha kuwa
umaskini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka
2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18. Kiwango cha umaskini wa
chakula kimepungua kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 na kufikia asilimia
8.0 mwaka 2017/18.
40. Mheshimiwa Spika, tathmini ya viashiria vya umaskini usio wa kipato inaonesha
tumefanya vizuri katika kuboresha hali ya makazi, umeme, huduma ya maji
safi na salama, vyoo, umiliki wa vyombo vya usafiri na mawasiliano.
Viashiria vinaonesha kuwa makazi yaliyojengwa kwa kutumia zege, mawe, saruji na vyuma yameongezeka. Vilevile, kaya zinazoishi katika nyumba zenye paa la kisasa zimeongezeka kutoka asilimia 68.0 mwaka 2011/12 hadi asilimia 84.1 mwaka 2017/18. Aidha, asilimia
78.8 ya kaya zinaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa kuta imara mwaka
2017/18 ikilinganishwa na asilimia 46.0 mwaka 2011/12.
Vilevile, asilimia 50.1 ya kaya zinaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa
sakafu imara mwaka 2017/18 ikilinganishwa na asilimia 40.0 mwaka
2011/12.
41. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika kuratibu Mikakati ya Kupunguza Umaskini ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 48 hadi ukurasa wa 52.
Ununuzi wa Umma
42. Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kufanya marekebisho ya Kanuni ya 164 ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kumpa mzabuni haki ya kupata taarifa ya ukamilishwaji wa mchakato wa ununuzi. Aidha, Kanuni ya 226 ilirekebishwa kumpa
mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kutoa idhini kwa Maafisa Masuuli
kuongeza idadi ya wajumbe wa timu za majadiliano kwenye miradi mikubwa
yenye maslahi kwa Taifa. Marekebisho hayo yamezingatia maoni ya wadau juu ya changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410.
43. Mheshimiwa Spika,
majukumu mengine yaliyotekelezwa katika kusimamia Ununuzi wa Umma ni
kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 52 hadi ukurasa wa 60
Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi - PPP
44. Mheshimiwa Spika, Wizara imepokea mapendekezo ya miradi ya ubia ipatayo 33, kati ya hiyo miradi sita imekidhi vigezo na kufanyiwa kazi. Miradi hiyo ni: Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Usafiri jijini Dar es Salaam Awamu ya kwanza (Dar- Rapid Transit Project- Phase1); Mradi wa Viwanda Vitatu vya Uzalishaji wa Dawa muhimu na Vifaa Tiba; mradi wa Usambazaji wa Gesi asilia katika Jiji la Dar es Salaam, Lindi na Mtwara; Mradi ya
Ujenzi ya Hoteli ya Nyota Nne; Kituo cha Biashara katika Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; na Mradi wa ujenzi wa hosteli ya
wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE). Aidha, Wizara
imekamilisha uchambuzi wa mawasilisho ya awali ya miradi 22 ya Mamlaka
za Serikali za Mitaa na wahusika watajulishwa kuhusu maeneo ya kufanyia
kazi kwa mujibu wa Sheria, mwongozo na taratibu za PPP.
45. Mheshimiwa Spika, majukumu mengine yaliyotekelezwa katika eneo la Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 60 hadi ukurasa wa 65.
Utekelezaji wa Majukumu ya Mashirika na Taasisi za Umma
46. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Wizara kwa mwaka 2018/19 ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 65 hadi ukurasa wa 114.
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
47. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2018/19, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imefanya
ukaguzi wa hesabu za: Wizara na Idara za Serikali 65; Vyama vya Siasa
14; Sekretariati za Mikoa 26; Wakala za Serikali 33; Mifuko Maalum 16;
Taasisi nyingine za Serikali 42; na Balozi za Tanzania 41. Aidha,
ukaguzi ulifanyika kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa 185 na Mashirika
ya Umma 176. Vilevile, Ofisi imefanya ukaguzi maalum
kwenye taasisi zifuatazo: Shirika la Usafiri Dar-es-Salaam (UDA); Mfuko
wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF); Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA);
Taasisi ya Elimu Tanzania; Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC); Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA); Jeshi la Polisi; na Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege.
48. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi pia ilifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo 469 na ripoti za ukaguzi zimetolewa. Aidha, katika ukaguzi wa
ufanisi, jumla ya taarifa 10 zimetolewa katika kipindi kilichoishia
Machi, 2019. Vilevile, hadi kufikia Aprili, 2019 Ofisi imetoa ripoti kuu
tano. Taarifa hizo ni muhtasari wa jumla ya taarifa 1,042 za ukaguzi
zilizotolewa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18.
Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
49. Mheshimiwa Spika, maelezo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyo chini ya Wizara kwa mwaka 2018/19 ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 117 hadi ukurasa wa 121.
CHANGAMOTO NA MIKAKATI YA KUKABILIANA NAZO
Changamoto
50. Mheshimiwa Spika, pamoja
na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya Wizara,
changamoto zifuatazo zilijitokeza katika mwaka huu wa fedha ambazo ni:
(i) Masharti yasiyo rafiki ya mikopo kwenye masoko ya fedha duniani;
(ii) Kupungua
na kutopatikana kwa wakati kwa fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo
katika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo; na
(iii) Mwamko mdogo wa kulipa kodi kwa hiari, kudai au kutoa risiti za kielektroniki.
Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto
51. Mheshimiwa Spika, katika
kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa bajeti kama
zilivyobainishwa hapo juu, Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali
zikiwemo:
(i) Kuhakikisha
kuwa Wizara na Taasisi zote za umma zinatumia Mfumo wa Serikali wa
Kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli (Government e-
Payment Gateway - GePG);
(ii) Kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kupunguza utegemezi;
(iii) Kuboresha
mfumo wa usimamizi wa mashine za kielektroniki za kutolea risiti ili
ziweze kutumika kwa kila muamala unaofanywa. Uboreshaji huu utaondoa
uwezekano wa kughushi risiti na kupunguza mianya ya ukwepaji wa kodi;
(iv) Kudhibiti
biashara ya magendo kupitia bahari, maziwa, mipaka, na njia zisizo
rasmi kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali kama TANROADS,
Mamlaka ya Bandari, Jeshi la Polisi, Jeshi la Wanamaji na Usalama wa
Taifa;
(v) Kuongeza
jitihada za ukusanyaji wa kodi za majengo kwa kushirikisha wadau muhimu
wakiwemo Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, OR-TAMISEMI,
Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Ofisi ya Taifa
ya Takwimu;
(vi) Kuendelea kusimamia utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015;
(vii) Kuendelea
kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo kwa kutekeleza
Mwongozo wa Ushirikiano (DCF) ili kuhakikisha fedha zilizoahidiwa
zinatolewa kwa wakati; na
(viii) Kuendelea
na majadiliano na taasisi za fedha za kimataifa ili kuhakikisha kuwa
fedha zinazotokana na mikopo ya kibiashara zinapatikana kwa kipindi
kilichobaki.
MALENGO YA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2019/20
52. Mheshimiwa Spika, naomba sasa nieleze kuhusu malengo ya mpango na bajeti ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka 2019/20;
MPANGO WA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA
53. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2019/20, Wizara itaendelea kusimamia majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na yafuatayo:
(i) Kubuni na Kusimamia utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla zinazolenga kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi;
(ii) Kuratibu uandaaji na ufuatiliaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa;
(iii) Kusimamia hatua mbalimbali za ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwezesha utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa ufanisi;
(iv) Kuratibu upatikanaji wa Misaada na Mikopo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na
kuhakikisha kuwa inaendelea kutolewa kama ilivyoahidiwa na kwa wakati
ili kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo;
(v) Kusimamia Deni la Serikali kwa kuhakikisha inakopa kwenye vyanzo vyenye riba nafuu;
(vi) Kufanya
ufuatiliaji na tathmini ya mikopo iliyodhaminiwa na Serikali ili
kuhakikisha wadaiwa wanalipa madeni husika kwa wakati kuepusha uwezekano
wa kuongeza mzigo kwa Serikali wa kulipa mikopo hiyo;
(vii) Kusimamia
mfumo wa udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na
kufanya maboresho ya mfumo wa Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury Single
Account) kwa lengo la kuboresha mfumo wa matumizi ya umma ili
kuiongezea Serikali uwezo wa kugharamia shughuli zake kwa wakati;
(ix) Kusimamia na kudhibiti matumizi ya fedha za umma ili kupata thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
(x) Kuratibu zoezi la uthamini wa mali katika taasisi za Serikali ili kuwa na taarifa sahihi za mali pamoja na kuendelea kuondosha mali chakavu, sinzia (dormant) na zilizokwisha muda wake;
(xi) Kusimamia
utekelezaji wa Sheria za Udhibiti wa Fedha Haramu kwa kupokea na
kuchambua taarifa za miamala shuku zinazohusu utakasishaji wa fedha
haramu na ufadhili wa ugaidi;
(xii) Kusimamia
zoezi linaloendelea la tathmini ya kitaifa ya mifumo ya kudhibiti
utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi (Mutual evaluation).
Tathmini hiyo itaijengea nchi sifa na uwezo wa kushirikiana na nchi
nyingine duniani kwa kubadilishana taarifa zinazohusu udhibiti wa
utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi;
(xiii) Kusimamia Mashirika na Taasisi za Umma kwa kuimarisha
ukusanyaji wa maduhuli kutoka katika Taasisi na Mashirika ya Umma na
Kampuni ambazo Serikali ina hisa, kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa
vinafanya kazi kwa ufanisi, kurejesha viwanda vilivyoshindwa kutekeleza
majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano na kuwapatia wawekezaji wengine
wenye uwezo na nia ya kuviendeleza;
(xiv) Kuratibu Mikakati ya Kupunguza Umaskini;
(xvi) Kuratibu shughuli za PPP nchini; na
54. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Mpango wa Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 125 hadi ukurasa wa 145.
Usimamizi na Uratibu wa Taasisi na Mashirika ya Umma Chini ya Wizara
55. Mheshimiwa Spika, mipango
kwa mwaka 2019/20 kwa upande wa Mashirika na Taasisi za Umma zilizo
chini ya Wizara ni kama inavyooneshwa kwenye kitabu cha hotuba yangu
kuanzia ukurasa wa 147 hadi ukurasa wa 167.
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
56. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imepanga
kutekeleza vipaumbele nane ikiwa ni pamoja na: kufanya ukaguzi wa
mafungu ya Bajeti ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala
na Taasisi za Serikali, Sekretariati za Mikoa, Mamlaka za Serikali za
Mitaa katika Mikoa yote nchini, Mashirika ya Umma; kufanya ukaguzi wa
miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Wahisani; kufanya kaguzi za
kiufundi katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa wa rasilimali za Umma kama
vile ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege, reli za kisasa, na Miradi ya umeme; kufanya maboresho ya mfumo wa ukaguzi kwa kutumia TEHAMA; na kukagua ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi; ukaguzi
wa ufanisi, kaguzi maalum, na kaguzi za kiuchunguzi (forensic audits)
katika maeneo yatakayoainishwa; na kuwajengea Wakaguzi uwezo wa kufanya
ukaguzi katika maeneo mapya ya ukaguzi pamoja na ukaguzi katika uhalifu
wa kifedha kwa kutumia mtandao (financial crimes auditing).
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/20
Makadirio ya Mapato
57. Mheshimwa Spika, katika mwaka 2019/20, Wizara inakadiria kukusanya maduhuli kiasi cha shilingi 967,042,379,000 (bilioni 967.04)
kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na gawio, kodi za
pango, marejesho ya mikopo, michango kutoka katika taasisi na mashirika
ya umma, mauzo ya leseni za udalali na mauzo ya nyaraka za zabuni.
Mchanganuo wa maduhuli yanayokadiriwa kukusanywa kwa mafungu ni kama
inavyoonekana kwenye Jedwali Na. 6 ukurasa wa 181 wa kitabu cha Hotuba
yangu.
Makadirio ya Matumizi kwa Mwaka 2019/20
58. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2019/20 Wizara ya Fedha na Mipango, Taasisi zake pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inakadiria kutumia kiasi cha shilingi 11,942,986,578,719 (trilioni 11.94). Kati ya fedha hizo, shilingi 11,212,404,636,988 (trilioni 11.21) ni kwa ajili matumizi ya kawaida na shilingi 730,581,941,731 (bilioni 730.58) ni matumizi ya maendeleo. Matumizi ya kawaida yanajumuisha shilingi 608,371,517,988 (bilioni 608.37) kwa ajili ya mishahara na shilingi 10,604,033,119,000 (trilioni 10.60) kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, matumizi ya maendeleo yanajumuisha shilingi 677,000,000,000 (bilioni 677.00) fedha za ndani na shilingi 53,581,941,731 (bilioni 53.58) ni fedha za nje.
MAOMBI YA FEDHA KWA MAFUNGU
Fungu 50 – Wizara ya Fedha na Mipango
59. Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi ya kawaida - shilingi 65,713,430,000 (bilioni 65.71). Kati ya hizo:
(i) Mishahara - shilingi 37,920,916,000 (bilioni 37.92); na
(ii) Matumizi mengineyo – shilingi 27,792,514,000 (bilioni 27.79).
(b) Miradi ya Maendeleo – shilingi 34,763,757,000 (bilioni 34.76). Kati ya hizo:
(i) Fedha za Ndani – shilingi 13,000,000,000 (bilioni 13.00); na
(ii) Fedha za Nje - shilingi 21,763,757,000 (bilioni 21.76).
Fungu 21 – HAZINA
60. Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaombakuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)Matumizi ya Kawaida – shilingi 1,272,801,249,988 (trilioni 1.27). Kati ya hizo:
(i) Mishahara - shilingi 536,520,631,988 (bilioni 536.52); na
(ii) Matumizi mengineyo – shilingi 736,280,618,000 (bilioni 736.28) ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya idara, taasisi zilizo chini ya Fungu hili, pamoja na matumizi maalum.
(b) Miradi ya maendeleo – shilingi 683,717,888,733 (bilioni 683.71). Kati ya hizo:
(i) Fedha za Ndani - shilingi 656,000,000,000(bilioni 656.00); na
(ii) Fedha za Nje - shilingi 27,717,888,733 (bilioni 27.71).
Fungu 22- Deni la Taifa
61. Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
Matumizi ya kawaida – shilingi 9,730,012,708,000 (trilioni 9.73). Kati ya hizo:
(i) Mishahara - shilingi 8,885,708,000 (bilioni 8.88); na
(ii) Matumizi mengineyo - shilingi 9,721,127,000,000 (trilioni 9.72)
Fungu 23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali
62. Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)Matumizi ya kawaida - shilingi 44,066,048,000 (bilioni 44.07). Kati ya hizo:
(i) Mishahara – shilingi 7,029,314,000 (bilioni 7.03); na
(ii) Matumizi mengineyo - shilingi 37,036,734,000 (bilioni 37.04).
(b)Miradi ya Maendeleo – shilingi 3,300,000,000 (bilioni 3.30). Kati ya hizo:
(i) Fedha za ndani – shilingi 2,000,000,000 (bilioni 2.00);na
(ii) Fedha za Nje - shilingi 1,300,000,000 (bilioni 1.30)
Fungu 7 – Ofisi ya Msajili wa HAZINA
63. Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi ya kawaida – shilingi 40,510,802,000 (bilioni 40.51). Kati ya hizo:
(i) Mishahara – shilingi 3,281,016,000(bilioni 3.28); na
(ii) Matumizi mengineyo – shilingi 37,229,786,000 (bilioni 37.23).
(b) Miradi ya Maendeleo – shilingi 2,300,000,000 (bilioni 2.30). Kati ya hizo:
(i) Fedha za ndani – shilingi 1,000,000,000 (bilioni 1.00); na
(ii) Fedha za Nje - shilingi 1,300,000,000 (bilioni 1.30).
Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha
64. Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
Matumizi ya Kawaida - shilingi 2,207,935,000 (bilioni 2.20)
Kati ya hizo:
(i) Mishahara - shilingi 649,793,000 (milioni 649.79); na
(ii) Matumizi mengineyo - shilingi 1,558,142,000 (bilioni 1.55).
Fungu 13 – Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu
65. Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(i) Matumizi ya mengineyo - shilingi 2,015,586,000 (bilioni 2.01); na
(ii) Matumizi ya Maendeleo – shilingi 200,295,998 (milioni 200.29) ambazo ni fedha za nje.
Fungu 45 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
66. Mheshimiwa Spika, katika Fungu hili kwa mwaka 2019/20, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)Matumizi ya kawaida – shilingi 55,076,878,000 (bilioni 55.07). Kati ya hizo:
(iii) Mishahara – shilingi 14,084,139,000(bilioni 14.08); na
(iv) Matumizi mengineyo – shilingi 40,992,739,000 (bilioni 40.99)
(b)Miradi ya Maendeleo – shilingi 6,300,000,000 (bilioni 6.30). Kati ya hizo:
(iii) Fedha za ndani – shilingi 5,000,000,000 (bilioni 5.00); na
(iv) Fedha za Nje - shilingi 1,300,000,000 (bilioni 1.30).
SHUKRANI
67. Mheshimiwa Spika, napenda nirudie tena kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha hotuba hii mbele ya Bunge lako Tukufu.
Aidha, kwa namna ya pekee kabisa naomba nitumie fursa hii kuwashukuru
Washirika wa Maendeleo wote wakiwemo nchi na mashirika ya kimataifa
ambao wamekuwa wakisaidia kwa namna mbalimbali katika utekelezaji wa
majukumu ya Wizara. Vilevile, napenda kuwashukuru Watanzania wote wenye
mapenzi mema na uzalendo kwa nchi yao ambao wamekuwa wakilipa kodi
stahiki na kwa hiari. Naomba nitumie fursa hii kuwaambia kuwa, mchango
wao katika ujenzi wa Taifa letu unathaminiwa sana na utaendelea
kukumbukwa hata kwa vizazi vijavyo.
68. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, napenda nikushukuru tena wewe binafsi, kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja hii pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara kwa anuani ya www.mof.go.tz
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments :
Post a Comment