Monday, June 3, 2019

Vyama vya Upinzani Vyatangaza Kususia Uchaguzi wa Marudio


Tokeo la picha la vyama upinzani
Vyama  nane vya upinzani vimesema havitashiriki uchaguzi wa marudio katika kata 32 unaotarajia kufanyika Juni 15, mwaka huu, endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haitatekeleza agizo la Mahakama la kuwataka wakurugenzi wa halmashauri kutosimamia uchaguzi.

Vyama vilivyosusia ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi,Chauma, UPDP, NLD,CCK na DP.

Wakizungumza kwa niaba ya vyama hivyo nane, viongozi wa vyama vinne vya ACT-Wazalendo, Chauma, UPDP na NLD walisema kitendo cha NEC kuwaruhusu wakurugenzi kuendelea kusimamia uchaguzi huo ni kuidharau mahakama na kwamba hata vyama vyao haviwezi kushiriki kwa kuwa kufanya hivyo ni kushirikiki katika dharau dhidi ya hukumu ya mahakama.

Akisoma tamko la vyama hivyo mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salam, Mwenyekiti wa Taifa wa UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema pamoja na kwamba mahakama ilitoa hukumu ya kufuta vifungu vya sheria vinavyowapa wakurugenzi mamlaka ya kusimamia uchaguzi, lakini vyama hivyo vimekuwa vikipokea barua ya mchakato wa uchukuaji na urudishaji wa fomu kutoka kwa wakurugenzi hao.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa marudio katika kata 32, Juni 15, mwaka huu na baada ya tangazo hilo, wakurugenzi wamekuwa wakiviandikia vyama vya siasa juu ya mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu na kutia saini kama wasimamizi wa uchaguzi huo,” alisema Dovutwa.

Aliongeza: “Itakumbukwa kuwa Mei 10, mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam ilitoa uamuzi wa kuvifuta vifungu vya sheria ya uchaguzi ambavyo vilikuwa vinawapa mamlaka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwa wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao. Mara baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema serikali itawasilisha kusudio lake la kukata rufani kupinga uamuzi huo, lakini mpaka tunavyozungumza hivi, hakuna rufani iliyowasilishwa wala ombi la kisheria la kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo.”

Dovutwa alisema vyama hivyo vinaitaka NEC kupitia mamlaka yake iliyopewa, kuteua wasimamizi wa uchaguzi huo wa marudio mara moja na kama itaendelea na msimamo wake wa kudharau amri ya mahakama, vyama hivyo vitachukua hatua ya kutoshiriki uchaguzi huo na vitawasiliana na wanaharakati waliofungua kesi hiyo kupeleka shauri mahakamani la kukazia hukumu hiyo na kuitaka mahakama iichukulie hatua NEC kwa kudharau amri hiyo ya mahakama.

Pia alisema vitaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika madai ya kuhakikisha wanapata tume huru ya uchaguzi ambayo itakuwa na uwezo kamili na mamlaka ya kuandaa na kusimamia uchaguzi huru na haki ikiwa ni pamoja na kuwa na watendaji na wasimamizi wake wasiofungamana na chama chochote cha siasa.

Vyama hivyo vilitumia nafasi hiyo pia, kuikumbusha NEC kutangaza utaratibu wa kuanza kuandikisha wananchi katika daftari la kudumu la wapigakura katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.

No comments :

Post a Comment