WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameagizahalmashauri zote za majiji na miji
zihakikishe kuwa kuanzia sasazinatenga maeneo ya michezo na burudani
kila zinapopima viwanja.
“Naagiza
kuanzia sasa, maeneo yote yanayopimwa na halmashauri na miji yote
nchini, lazima yazingatie uwepo wa maeneo ya michezo na burudani,”
amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 10, 2019)wakati akifungua
mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za msingi na
sekondari Tanzania, katika Uwanja waNangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Zaidi ya wanafunzi 5,400 wanashiriki mashindano hayo.
Pia,
amezitaka Halmashauri ziweke mpango madhubuti wa kuyaendeleza maeneo ya
michezo na burudani sambamba na miundombinu inayozingatia mahitaji ya
wote bila kubagua.
Amesema
katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na uhaba wa viwanja vya michezo kwa
sababu ya mipango miji isiyozingatia mipango endelevu ya sekta
mbalimbali.
Hivyo,
Waziri Mkuu ameagiza yafanyike marekebisho na hatua za haraka ili kutoa
fursa ya ukuaji wa michezo na kusaidia wananchi kushiriki michezo,
mazoezi na kupata burudani.
Amesema
ifikapo Septemba 30, 2019, kila halmashauri iwe imefanya mapitio ya
maeneo yote yaliyokuwa yamepimwa kwa matumizi ya huduma maalum ikiwemo
michezo, burudani, shule na ibada na kutoa taarifa kama yanatumika kwa
ajili hiyo au vinginevyo.
Wakati
huo huo,Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
irudishe na iimarishe mchepuo wa Elimu kwa Michezo Chuo cha Ualimu
Butimba ili kupata wataalam zaidi.
“Halmashauri
ziendelee kuwaruhusu walimu mbalimbali nchini kuhudhuria mafunzo ya
michezo katika chuo cha Mendeleo ya Michezo Malya ili kupunguza uhaba wa
watalaam wa michezo katika shule mbalimbali na nchini kwa ujumla.”
Waziri
Mkuu amesema michezo ni muhimu kwa wanafunzi kwa kuwa itawaepusha
vijana na makundi yasiyofaa yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya na
vitendo vingine visivyoendana na maadili ya Kitanzania.
Amesema
michezo itawawezesha vijana kuwa na afya bora na kufanya vema katika
masomo yao kwa kuwa ili waweze kusoma vema ni sharti afya zao ziwe
njema. Pia sanaa itasaidia katika kuutambulisha utamaduni wetu ndani na
nje ya mipaka ya nchi yetu.
“Kwa
hiyo, ni vema tukatambua kuwa michezo na sanaa ni sehemu ya elimu bora.
Hivyo, ni muhimu kutekeleza dhana ya elimu ya michezo ili tuweze
kufikia maendeleo tarajiwa.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema sambamba na michezo iliyozoeleka, pia wanaweza
kuibua michezo yao ya asili ambayo itautambulisha utamaduni wetu. “Nitoe
wito kwa shule zetu, ziendeleze ubunifu wa kuibua vipaji vya sanaa na
michezo ya asili katika maeneo yetu kwa lengo la kuenzi utamaduni wetu.”
Akizungumzia
kuhusu mashindano ya mwaka huu ambayo yameshirikisha wanafunzi wengi
zaidi wenye mahitaji maalumu, Waziri Mkuu amesema waendelee kuwahusisha
wanafunzi wote katika michezo, sanaa na burudani bila kujali aina ya
ulemavu walionao.
Amesema jambo hilo ni muhimu kwa kuwa vipaji vipo kwa wote na fursa ndizo zitakazowawezesha kuonesha vipaji hivyo na kuvikuza.
Waziri
Mkuu amewasisitiza wadau wote wa shule za msingi, sekondari, vyuo,
sehemu za kazi na wizara, waweke mipango ya kudumu ya kuwashirikisha
watu wenye mahitaji maalumu katika shughuli mbalimbali za kijamii na
kiuchumi bila ubaguzi wowote.
“Hakikisheni
baadhi ya vikwazo katika kushirikisha watu wenye mahitaji maalumu
kwenye michezo vinaondolewa. Vikwazo hivyo ni pamoja na kutokuwepo kwa
mipango endelevu katika maeneo mbalimbali na uwepo wa mitazamo hasi ya
baadhi ya walimu, wazazi na viongozi katika maeneo yao dhidi ya uwezo wa
wanafunzi wenye mahitaji maalum.”
Aidha,
Waziri Mkuu ametuamia fursa hiyo kuupongeza Mkoa wa Simiyu kwa kuwa
mmoja kati ya Mikoa ya mfano katika kutekeleza agizo lake la mwaka jana
alilolitoa kupitia michezo hiyo la kuanzishwa kwa shule maalumu za
michezo.
Mkoa
wa Simiyu umejenga Shule ya Sekondari itakayokuwa kituo cha kukuza
vipaji vya wanafunzi katika michezo. “Naagiza mwakani wanafunzi wote
walioonesha vipaji katika michezo watakaofaulu Mtihani wa Elimu ya
Msingi wapangwe katika shule hiyo ili wakakuze vipaji vyao.”
Amesema
bila ya kuwa na mipango ya kulea na kukuza vipaji kutoka ngazi za chini
Taifa haliwezi kupata mafanikio katika michezo nchini. Kwani katika
kipindi ambapo michezo hiyo ilisitishwa kiwango cha michezo ya aina
mbalimbali kilikuwa chini sana.
“Tangu
tumerejesha shughuli za michezo katika shule zetu tumekuwa na mafanikio
makubwa sana ikiwemo kupata wachezaji wanaofuzu kucheza soka la kulipwa
kwenye viwango vya kimataifa kama Mbwana Samatta (Genk –Belgium), Simon
Msuva (Difaa El Jadid – Morocco), “
Wengine
ni Shiza Kichuya (Enppi –Misri), Thomas Ulimwengu (JS Saoura –
Algeria), Hamid Mao (Petrojet – Misri), Adi Yusuph (Blackpool –England),
Hassan Kessy (Nkana – Zambia), Yahya Zaydi (Ismaily –Misri), Shabani
Chilunda, (Tenerife – Hispania) Rashid Mandawa (BDF- Botswana), Farid
Mussa ( Tenerife– Hispania).
Waziri
Mkuu amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, jitihada zaidi
zinahitajika ili kuwa na maendeleo ya kutosha katika shughuli za michezo
nchini.
Hivyo,
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa
kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais
TAMISEMI wakamilishe tathmini ya shule 56 za Serikali zilizokuwa
zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya michezo.
Ufunguzi
huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri
wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Maafisa Elimu
kutoka mikoa yote nchini, walimu wa michezo pamoja na Maofisa wengine wa
Serikali.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JUNI 10, 2019.
No comments :
Post a Comment