Kufuatia
nchi za Kanda ya Afrika Mashariki kuwa katika hatari ya kuathirika na
magonjwa ya mlipuko kama Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya Ndege na
Ebola, na kwa kuwa magonjwa hayo husambaa kutoka nchi moja kwenda nchi
nyingine, Tanzania kwa kushirikiana na Kenya wameanza kutekeleza zoezi
la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, lilofunguliwa leo mpakani
mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga, kuanzia tarehe 11 hadi 14
Juni mwaka huu.
Zoezi hilo, linazingatia Dhana ya Afya moja ambayo hujumuisha sekta ya
afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na mazingira katika kujiandaa,
kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu. Jumla ya
washiriki 150 ambao wanatoka Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Kenya na
Tanzania washiriki 130 kutoka ngazi ya taifa, mkoa na wilaya katika
mpaka wa Namanga; pamoja na nchi nyingine wanachama ambapo watakuwa
watazamaji ikiwa ni Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini
wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo.
Akiongea
leo tarehe 11 Juni, 2019, wakati wa Kufungua rasmi zoezi hilo la siku
nne, mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu,
amefafanua kuwa, serikali kupitia Wizara hiyo inatumia zoezi hilo
kufanyia majaribio ya utekelezaji wa Mipango ya Dharura ya Taifa na
Kanda, Miongozo ya Utendaji na kuwapa washiriki fursa ya kujifunza namna
sekta zingine zinavyotekeleza majukumu katika kuzuia na kupunguza
madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na maafa ya magonjwa ya mlipuko.
“Hapa nchini Tanzania tunalo Dawati la Kuratibu masuala ya Afya Moja
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati hilo sisi kama wizara ya
Afya tunasubiri tu ripoti ya zoezi hili na tutaitekeleza mara moja.
Utekelezaji wa ripoti hiyo tutahakikisha unakuwa wa ufanisi na tija kwa
nchi ili tuweze kusaidia kuimarisha ushirikiano wa sekta za Afya hapa
nchini kwa kuzingatia dhana ya Afya moja.” Amesisitiza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy, ameongeza kuwa zoezi hilo linalenga kutathmini
utaratibu wa kutumia kikosi cha taifa cha dharura cha kukabili lakini
pia kuhakiki matumizi ya maabara zinazohamishika, kutathmini uwezo wa
uchunguzi na usimamizi wa magonjwa ya mlipuko kwa vituo vilivyopo
mpakani kwa magonjwa ya mifugo na binadamu; kupima hatua za kujiandaa
kukabiliana katika viwanja vya kimataifa vya Jomo Kenyatta na
Kilimanjaro.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Mhe.
Stella Ikupa, akiongea kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.
Jenista Mhagama, ameeleza kuwa Serikali kupitia ofisi hiyo, itaendelea
kuratibu sekta zote za Afya nchini kwa kutumia Dhana ya Afya moja, ili
kuhakikisha Afya za wananchi zinakuwa imara na salama kwa kudhibiti
magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kusababisha maafa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega,
akiongea kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina,
amebainisha kuwa, kwa kutambua umuhimu wa Dhana ya Afya moja, Wizara
inafahamu kuwa mifugo huwa ni chanzo cha vimelea vya magonjwa ambayo
huambukizwa binadamu, hivyo serikali imeendelea kuboresha maabara za
Mifugo nchini ili kuweza kutambua vimelea kwa haraka na wakati ili
visisababishe magonjwa ya mlipuko kwa binadamu.
Naye, Waziri wa Afya wa Kenya, Mhe. Sicily Kariuki, amebainisha kuwa
zoezi hilo ambalo linahusisha mlipuko wa virusi vinavyo shabihiana na
Homa ya Bonde la Ufa katika eneo la mpakani, ni muhimu katika kuimarisha
ushirikiano wa sekta za Afya, kwa kuwa washiriki watahitajika kuonesha
utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo kwakuzingatia Dhana ya Afya
Moja.
Zoezi
hilo linafanyika nchini Tanzania kufuatia Kikao cha 11 cha Kawaida cha
Mawaziri wa Sekta ya Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika
mwezi Machi, 2015, ambapo kilielekeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki kuandaa Zoezi la Nadharia la kukabiliana na magonjwa ya
mlipuko katika mpaka wa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga.
Zoezi hilo ambalo linafanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo
la Namanga, linaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa kushirikiana na nchi wanachama kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo
la Ujerumani la GIZ na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILINO SERIKALINI
OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments :
Post a Comment