
Rais
Magufuli ametaja sababu za kumng’oa Waziri wa Viwanda na Biashara,
Joseph Kakunda na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Charles Kichere, huku akitoa pole kwa walioteuliwa kushika nyadhifa
hizo.
Rais
Magufuli alitaja sababu hizo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati
akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni ambao ni Waziri wa Wizara
ya Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Kamishna Mkuu wa TRA, Edwin
Mhede na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Kichere.
Katika
mkutano huo, Rais Magufuli alishuhudia Kampuni ya Bharti Airtel
ikiikabidhi serikali gawio la Sh. bilioni tatu la miezi mitatu kuanzia
Aprili pamoja na fedha binafsi iliyotolewa na mwanzilishi na Mwenyekiti
Mtendaji wa kampuni hiyo, Sunil Mittal, dola za kimarekani milioni moja
(Sh. bilioni 2.2).
Akitaja
sababu za kuwaondoa kwenye nafasi zao Kakunda na Kichere, Rais Magufuli
alisema: “Tutaambizana maneno mazuri mazuri, lakini maneno mazuri
hayasaidii, ukitaka maneno mazuri kaelezwe na mume wako, mke wako basi,
lakini sisi tunataka matokeo mazuri basi,” alisema.
Rais Magufuli alisema jukumu lake ni kuteua ili kusudi nia ya Watanzania wanayohitaji ikatimie.
“Ninapotengua
mahali siyo kwamba wewe ninakuchukia, nakupenda tu na ninakupongeza
mheshimiwa Joseph Kakunda kwa kuja, huku ndiko kukomaa kisiasa, hizi
kazi ni muda mfupi, maisha yenyewe ni ya muda mfupi, hakuna kazi ya
kudumu,” alisema.
Alisema,
“Lakini amejitoa amekuja, safi sana lakini ni ukweli kwenye wizara
hakuisukuma ninavyotaka, ni mimi ninataka matokeo na Watanzania
walionichagua wakatupigia kura wanataka kuona utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi.”
“Changamoto
za wafanyabiashara kwani kulikuwa na ubaya gani, Naibu Waziri, Katibu
Mkuu, Waziri mwenyewe siwangekuwa wameshapanga mikutano wa
wafanyabiashara, palikuwa na dhambi gani? Nani angewakataza? kwamba leo
tunazungumza na wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa, leo Kanda ya
Kaskazini, leo Kusini, nisikie shida na changamoto zao.”
Rais
Magufuli alisema: “Wanasema hawajawahi kumuona, hata ningeuliza hata
Manyanya (Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Viwanda) nikasema labda
hawajawahi kumuona, kwa sababu Watanzania siyo wanafiki,” alisema.
Kuhusu korosho, Rais Magufuli alisema wamefanya biashara hiyo zaidi ya tani 223,000 na kuhoji ni tani ngapi zimeshauzwa.
“Wizara
inaitwa Wizara ya Viwanda na Biashara ni biashara gani inafanya? Wizara
ya Kilimo imetimiza wajibu wake, imenunua, wanajeshi wametimiza wajibu
wao wamesomba korosho yote wameweka kwenye maghala, Wizara ya Biashara
inafanya nini? Ipo tu, korosho zimekaa,” alihoji.
“Wakati
huo Tanzania ilikuwa ndiyo wazalishaji peke yetu, tumesubiri hadi mwezi
wa tatu mpaka wa nne ukaingia nchi nyingine za Benin, Nigeria, Cote
d’Ivoire nazo zikazalisha bado hatujauza, wapo tu, sasa unakuwa
unajiuliza wa nini? Kupeperusha bendera barabarani? Haiwezekani,”
alisema.
Rais
Magufuli alimwambia Bashungwa kuwa inawezekana wamempongeza, lakini
alifikiri wangempa pole kwa sababu akiona mambo hayaendi atamtengua.
“Kwa
sababu nitaangalia yale ambayo hayaendi, nikiona hayaendi ninatengua
nasema ukweli, Prof. Palamagamba Kabudi (Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.
Philip Mpango, wamezungumza tu hapa hawataki kusema, lakini kama ni
‘pumbavu’ kwenye simu wametukanwa mno waulizeni,” alisema na kuongeza:
“Wananizidi
umri, lakini neno pumbavu linakuja tu haraka haraka, ndiyo ukweli kwa
sababu hii kazi siyo ya kubembelezana, lazima tuipeleke kijeshi,
mwanajeshi usiposonga mbele kupigwa risasi na mwenzako siyo tatizo, mpo
kwenye vita… hatuwezi kukawa na vita halafu tukawa tunabembelezana na
kupeana maneno mazuri tu, lazima tubadilike, wanaotuangalia hawana muda
wa kusubiri.”
Rais Magufuli alisema Wizara ya Viwanda na Biashara wamebangua tani 2000, nyingine wanasubiri atelemke nani ndiyo waziuze.
“Na
una waziri pale wa biashara ana vyombo vyote vya kufanya biashara
nikitakiwa nimpandie kutoka juu mpaka chini, pamoja na wewe Muhende
ulikuwa uende huko huko, ukienda kafanye kazi usibembeleze mtu
usimchekee mtu nafuu wakuchukue mimi ninayekuteua nikusimamie kinyume na
hapo utakwenda kunusa tu pale urudi Karagwe,” alimweleza waziri mpya.
Rais
Magufuli alimtaka waziri huyo yale ambayo yamekaa yatatuliwe, viwanda
vilivyoshindwa kuendelezwa visiorodheshwe tu, vitafutiwe watu
wavichukue.
“Kiwanda
kama cha Mbeya cha nguo kinakwenda kubadilishwa kiwe cha pipi,
hakiwezekani, tunaonekana tunakula pipi tu, zipo changamoto nyingi
kashirikiane na wenzako kuzitatua,” alisema.
Akigeukia
kilichomwondoa Kichere, Rais Magufuli alisema Waziri Mpango amezungumza
alivyokuwa pale Kamishna wa TRA, aliipandisha kutoka Sh. bilioni 850
hadi trilioni 1.3.
“Nikampandisha
cheo kutoka TRA akawa Waziri wa Fedha, sasa wengine mnaokwenda
mnasimamia hapo hapo kana kwamba ni fomula, lakini tatizo malalamiko ni
mengi na hamchukui hatua, kama kuna ujumbe mfupi nimekutumia kamishna
uliyeondoka yawekezana zinazidi 20 au 30 zingine nilikuwa natuma saa
nane za usiku, nyingine saa tisa na nyingine saa kumi kwa sababu watu
wanapolalamika ninamtumia na jamaa huyu ni kama diplomat
(mwanadiplomasia) anasema nimepoka mheshimiwa,”
Aliongeza,
“Ukifuatilia hakuna matokeo, ndiyo ukweli, mimi huwa sisahau ndiyo
dhambi niliyonayo, haiwezekani mkurugenzi wako wa kukadiria anatoa
makadirio ya kijinga kwa wafanyabiashara upo unamwangalia tu wakati una
nguvu unashindwa kuitumia, unaona makusanyo ya kodi ya ndani yanashuka,
labda huyu wa sasa imepanda kidogo, lakini hakuna hatua inayochukuliwa.”
Rais
alisema: “Unaona kuna wafanyabiashara wanapakia mizigo wanaiandika
inakwenda Tunduma hadi nchi jirani, wakifika Tunduma wanagongewa mihuri
wanarudi kuishusha wakati barabara yote TRA, lori linatembea kilometa
1,300 linasema linakwenda nchi jirani wanachukua nyaraka wanagonga
mpakani wanarudi, kama gharama mtu ameamua kusafirisha hadi Tunduma
anarudi halafu amehonga za kugonga muhuri, zingejumlishwa zote
angetelemsha mizigo yake hapa si mngemsaidia atumie mafuta vizuri.
Rais
Magufuli alibainisha kuwa kuna mwekezaji alikuja na vifaa vyake anataka
kuchimba dhahabu, lakini vimekaa zaidi ya mwaka alikuwa kiasi kidogo
akaongezewa zaidi.
“Badala
ya kuangalia huyu atawekeza hiki atatoa ajira na serikali itapata
mapato kutoka kwenye dhahabu, utafikiri TRA wote hawakusoma, ndiyo maana
nikasema siwezi, ndio maana siku ile walivyokusema nakuuliza unasema
hujui unamwangalia mtu wa nyuma yako utamwangalia mpaka lini ukikuta
hawapo, nafuu utoke na wewe hapo hapo,” alisema.
Rais Magufuli alimwambia Kichere kuwa amempeleka Njombe akajaribu ukatibu tawala na endapo akiusimamia vibaya atamtoa.
Aliwambia kuwa kuna watu wamebobea pale TRA na kumtaka akawakamate ili kodi ipatikane.
“Hakuna
nchi duniani iliyoendelea bila kodi, niache kuwalipa mishahara si
nitawakuta Ikulu wamesimama, usicheke na mtu, ni sawa na useme usiende
mbinguni tutakuombea wote tunaofaidi utakwenda kwa nguvu tutakusukumiza
Watanzania wote milioni 55 uingie mbinguni,” alisema.
Pia
alimtaka akashirikiane na wafanyabiashara ili wampe taarifa nyingi na
wale walioghushi siku za nyuma kutokana na mazingira akakae nao waseme
wanaweza kulipa kiasi gani, kwa sababu anayo mamlaka ya kusamehe
asilimia fulani.
Kuhusu
watumishi wanaokwenda kwa wafanyabiashara kuwapa makadirio makubwa na
kusema wametumwa juu, amemtaka asiogope kuwafukuza, awashike na
kuwapeleka mahakamani.
“Kama
unawafanyakazi 1000, halafu 200 wakaishia kufukuzwa na kwenda
mahakamani sawa tu, lakini ukiwa mtaratibu watakukaribisha na siku
ukiingia ofisini watakuletea au karibu wote watakuita bosi hata kama
naye ni bosi achana na sherehe, jana nimekutumia ujumbe wa mtu
analalamika, kabla sijakuapisha,” alisema.
Alisema kuna makamishna wa TRA katika mipaka, ambapo mpaka wa Rusumu unafanya vizuri lakini Tunduma na Sirari hakufai.
No comments :
Post a Comment