Mkurugenzi
Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru akiongea kuhusu sifa na utaratibu wa
utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 leo jijini Dar es salaam.
Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utoaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronica
Nyahende.
Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza mwongozo wa ...utoaji mikopo kwa mwaka
wa masomo 2019/2020 unaotaja sifa, vigezo na utaratibu wa kuwasilisha
maombi ya mikopo ya elimu ya juu na kuwasihi waombaji mikopo watarajiwa kuusoma
kwa makini na kuuzingatia.
Mkurugenzi Mtendaji wa
HESLB Abdul-Razaq Badru amewaambia wanahabari leo (Jumanne, Juni 4, 2019)
jijini Dar es salaam kuwa lengo la kutoa mwongozo huo ni kuwawezesha waombaji
mikopo kuandaa nyaraka muhimu zinazotakiwa.
Kwa mujibu wa Badru, HESLB
imetoa mwongozo huo kabla ya kufungua mfumo wa maombi ya mkopo ili kuwawezesha
waombaji mikopo watarajiwa kuandaa nyaraka muhimu. Mfumo wa maombi kwa njia ya
mtandao utafunguliwa Juni 15, 2019 na utafungwa Agosti 15, 2019.
Uzoefu
na sababu za kutoa mwongozo
“Uzoefu wetu unaonesha
kuwa waombaji wengi hukimbilia kwenye mtandao na kujaza fomu za maombi wakati
mwingine bila kusoma mwongozo. Mwaka huu tumetoa mwongozo huu kwanza ili
wausome kwa wiki takribani mbili kabla ya kuruhusiwa kuanza kujaza fomu kwa
njia ya mtandao,” amesema Badru na kuongeza kuwa katika mwaka 2018/2019,
waombaji zaidi ya 9,000 kati ya 57,539 waliokuwa na sifa za
msingi walikosea kujaza fomu za maombi.
Ili
kutatua tatizo hilo mwaka 2019/2020, Badru amesema HESLB imetembelea shule za
sekondari 81 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar na
kukutana na wanafunzi 27,489 ambao walielimishwa kuhusu sifa na utaratibu
wa kuomba mkopo kwa usahihi.
Mkurugenzi Mtendaji
huyo amesema mwongozo huo unapatikana katika lugha za kiingereza na kiswahili katika
tovuti ya HESLB ambayo ni www.heslb.go.tz
“Pamoja na mwongozo
huo, pia tumeandaa kijitabu chenye maswali na majibu yanayoelekeza namna ya
kuomba mkopo kwa lugha ya kiswahili … nacho pia kinapatikana kwenye tovuti yetu
na tunawashauri wakisome,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Nyaraka muhimu za kuandaa
Waombaji wote wanatakiwa na vyeti vya kuzaliwa ambavyo vimethibitishwa
na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa
Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA). Aidha, kwa waombaji mikopo ambao wazazi
wao wamefariki dunia, watatakiwa kuwa na nakala za vyeti vya vifo ambavyo
vimethibitishwa na RITA au ZCSRA.
“Vilevile tunafahamu kuwa kuna wanafunzi waliofadhiliwa na taasisi
mbalimbali katika masomo yao ya sekondari au stashahada, hawa wanatakiwa kuwa
na barua kutoka katika taasisi hizo,” amesema Badru katika mkutano huo
uliohudhuriwa na Mkurugenzi wa Upangaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronika Nyahende.
Kwa wanafunzi wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu, Badru
amesema wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu wao kutoka kwa waganga
wakuu wa wilaya au mikoa.
Maeneo muhimu yaliyoboreshwa kwa
2019/2020
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo aligusia maeneo muhimu
yaliyoboreshwa katika utoaji mikopo kwa lengo la kuwafikia wanafunzi wahitaji
wengi Zaidi.
“Baada ya kupokea maoni ya wadau, tumeongeza umri wa waombaji mikopo
kutoka miaka 33 hadi 35 na pia mwaka huu tutapokea maombi kwa wanafunzi
waliomaliza kidato cha sita au stashahada ndani ya miaka mitano iliyopita …
kabla ilikuwa miaka mitatu tu,” amesema Badru.
Malengo na bajeti
Katika mwaka wa masomo 2019/2020, Serikali kupitia HESLB imepanga kutoa mikopo na
ruzuku ya elimu ya juu yenye thamani ya TZS 450 bilioni kwa jumla ya wanafunzi 128,285. Kati ya hao, wanafunzi 45,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza. Mwaka huu 2018/2019, unaoelekea mwisho; jumla ya
TZS 427.5 bilioni zilitolewa kwa jumla ya
wanafunzi 123,000.
Dawati la huduma kwa wateja
Pamoja na mwongozo
uliotolewa, dawati la huduma kwa wateja litakuwa wazi ili kutoa ufafanuzi pale
utakapohitajika. Wateja wetu pia wanaweza kupiga simu au kutuandikia barua pepe
anuani na namba: Simu: 0736 665533 au 0738 66
55 33 au 022 5507910; Barua
pepe: adcp@heslb.go.tz au info@heslb.go.tz
Taarifa hii pia inapatikana
kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz
No comments :
Post a Comment