Meneja
wa Kili Challenge Manace Ndoroma (wa kwanza kushoto) akiwa katika picha
ya pamoja na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dk. Faustine Ndugulile (wa tano kushoto), Mkurugenzi wa Tacaids,
Dk. Leonard Maboko (wa nne kushoto), Makamu wa rais miradi endelevu wa
kampuni ya AngloGold Ashanti, GGM, Simon Shayo (watatu kulia) pamoja na
viongozi wengi waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la
upandaji wa mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro Challenge 2019), na kuendesha
harambee ya kuchangisha fedha kwa mwaka 2019 kwa ajili ya afua za
UKIMWI nchini. Katika hafla hiyo GGM walikabidhi Tacaids hundi ya Sh
bilioni 1.173.
Makamu
Rais wa Mgodi wa dhahabu Geita (GGM), Simon Shayo (wa pili kulia)
akikabidhi hundi ya Sh milioni 150 kwa Waziri wa Afya, maendeleo ya
jamii, jinsia, wazee na watoto, Dk Faustine Ndungulile na Mkurugenzi
Mtenda wa Tacaids, Dk. Leonard Maboko. Mchango huo unalenga kudhibiti
maambukizi ya VVU kwa kupitia kampeni ya Kilimanjaro Challenge
inayoratibiwa na GGM pamoja na Tacaids.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk.
Faustine Ndugulile akizungumza katika uzinduzi wa katika hafla ya
uzinduzi wa zoezi la upandaji wa mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro
Challenge 2019), na kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa mwaka
2019 kwa ajili ya afua za UKIMWI nchini. Katioka hafla hiyo GGM
walikabidhi Tacaids hundi ya Sh bilioni 1.173.
Mkurugenzi
wa Makao ya watoto moyo wa huruma – Geita, Sr. Adalbera Mukure
akielezea namna kampeni ya Kili Challenge kupitia GGM ilivyonufaisha
kituo hicho na kuwezesha watoto zaidi ya 137 wanaolelewa katika kituo
hicho kupata huduma mbalimbali ikiwamo elimu. Kulia kwake ni George
Emanuel na kushoto ni Rosemarry Emanuel ambao ni baadhi ya watoto
waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Kili Challenge jijini Dar
es Salaam.
***
NA MWANDISHI WETU
NAIBU
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk.
Faustine Ndugulile jana 4, June 2019 amezindua zoezi la upandaji wa
mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro Challenge 2019), na kuendesha harambee
iliyowezesha kupatikana zaidi ya Sh bilioni 1.5 fedha zilizochangwa kwa
ajili ya afua za UKIMWI nchini.
Aidha,
amesema Serikali inatarajia kupeleka bungeni Muswada wa Sheria wa
kushusha umri wa kuridhia vijana kupata huduma zaUKIMWI kutoka miaka 18
hadi miaka 15 ili kupunguza wimbi la maambukizi mapya ya virusi vya
UKIMWI (VVU) hususani kwa vijana.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Tume ya Taifa ya Kuthibiti UKIMWI nchini
(TACAIDS)), kubainisha kuwa kwa siku zaidi ya watu 200 hupata maambukizi
mapya ya VVU, huku kati yao vijana 80 wenye umri wa miaka 15 hadi 24
pia huambuki kwa siku.
Kilimanjaro
Challenge ni mfuko muhimu unaoratibiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita
(GGM) na Tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikisha
taasisi za nje na ndani ya nchi katika kuendeleza mapambano dhidi ya
VVU/ UKIMWI.
Dk.
Ndugulile akizungumza katika hafla hiyo alisema tatizo la ugonjwa wa
UKIMWI linabadilika kila mara hivyo kuchangia zaidi ya asilimia 40 ya
vijana kuathiriwa huku asilimia 80 ya vijana hao wakiwa ni vijana wa
kike.
“Serikali
tumeanza kuliona hilo na kuchukua hatua, hatua ya kwanza kwanza
kushusha umri wa kuridhia kwani ni kweli wanaanza kujamiiana wakiwa umri
wadogo, takwimu zinaonesha kuanzia wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi
19, asilimia 27 ni wajawazito au wana watoto.
“Kwa
hali hii ya maambukizi tumeamua kupeleka muswada bungeni kushusha umri
wa ridhaa hadi miaka 15. Ili sasa iweze kuruhusu kijana kuweza kupata
huduma, kwa sababu kwa sasa inabidi apate ridhaa ya mzazi au mlezi,”
alisema Dk. Ndugulile.
Aidha, alisema wizara hiyo italeta mpango wa kuruhusu watu kujipima wenyewe ili kutoa motisha kwa akina baba kupima VVU”
“Kama ilivyo kwa wanawake wanavyojipima ujauzito na kina baba watahamasika kujipima na naamini litawapa motisha,” alisema.
Aidha,
Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk. Leonard Maboko alisema muswada huo
ukipitishwa na kuwa sheria utasaidia vijana kupata huduma zaUKIMWIkwa
haraka bila ridhaa ya mzazi au mlezi kama ilivyo sasa.
Alisema hadi sasa Tanzania inao watu milioni 1.5 wenye VVU ambao ni sawa na asilimia 4.7.
“Lakini
maambukizo mapya yamepungua kutoka 80,000 miaka mine iliyopita hadi
72,000. Katika kundi hili watanzania 6000 wanapata maambukizo mpaya kwa
mwezi na kwa siku ni 200,” alisema.
Aidha, alisema sababu za vijana kupata maambukizo zaidi ni kutoka kwenye utoto kwenda kwenye ujana.
“Hawajapata
elimu sawasawa hivyo inakuwa rahisi kwake kufanya maamuzi ambayo hana
taarifa za kutosha. Lakini pia vijana wa kike kutaka kupata vitu kwa
haraka.
“Ndio maana tuna miradi ambayo inagusa kaya maskini kwa kuwasaidia kupata elimu ya ujasiriamali katika mikoa mitatu,” alisema.
Kutokana
na tatizo hilo Makamu wa rais miradi endelevu wa kampuni ya AngloGold
Ashanti, GGM, Simon Shayo alisema kwa mwaka huu katika kampeni hiyo ya
kuchangia afua za UKIMWI wamelenga kukusanya Sh bilioni mbili.
Hata
hivyo, alisema hadi sasa tayari wamekusanya zaidi ya Sh bilioni 1.5
sawa na asilimia 67 ya lengo la kampeni hiyo ya mwaka huu ambayo sasa
inatimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake.
Alisema
tangu kuanzishwa kwa Kilimanjaro Challenge, zimekusanywa zaidi ya Sh
bilioni 13 ambazo zimenufaisha asasi na taasisi mbalimbali 50
zinazoshughulikia masuala ya UKIMWI.
“Lengo kuhakikisha maambukizi mapya yanatokomea na kufikia lile lengo la sifuri tatu,” alisema.
Alisema
tangu kampeni hiyo ianzishwe watu zaidi ya 800 wamepanda Mlima
Kilimanjaro, na mwaka huu wanategemea zaidi ya watu 80 wakiwamo
waendesha baiskeli.
Aidha,
Mkurugenzi wa Makao ya watoto moyo wa huruma – Geita, Sr. Adalbera
Mukure alisema tangu kituo hicho kifunguliwe mwaka 2006 kwa kuwezeshwa
na GGM, kimeweza kuboresha maisha ya watoto mbalimbali.
Alisema
kituo kimesomesha watoto 18 wa chekechea, shule za msingi, 70,
sekondari 29, kidato cha tano na sita 8, vyuo vikuu wawili, mmoja chuo
cha walimu, wawili wameajiriwa kwenye sekta binafsi na wawili bado
hawajapata ajira.
“Tunaomba
michango yenu ili kuwezesha ujenzi wa shule ya English medium ili
kuwezesha watoto kusoma na hata watoto wa nje ya kituo kusoma na fedha
zitakazopatikana kutumika kuendesha kituo,” alisema.
Meneja
wa Kili Challenge Manace Ndoroma alisema bodi ilikaa na kuamua kuwa
mwaka huu zitatolewa Sh milioni 800 ambazo kati yake Sh milioni 550
zitabakia kusubiri maombi ya asasi mbalimbali zitakazowasilisha maombi
yao.
“Sh
Milioni 150 zitaenda Tacaids kujenga vituo vyta huduma za ukimwi. Sh
Milioni 50 moyo wa huruma kuwezesha kituo kiuchumi Sh milioni 50
zitakwenda kwa mfuko waUKIMWI (ATF) wakati Sh bilioni 1.173 zilizotolewa
na GGM zitaenda Kili Trust Fund,” alisema.

No comments :
Post a Comment