Dar-es-salaam, Juni 11, 2019: Benki
ya Azania (ABL) imefungua maduka matano maalum kwa ajili ya
kubadirishia fedha za kigeni katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na
Kilimanjaro ili kuwapa fursa wateja wa benki hiyo pamoja na wananchi
wote njia rahisi ya kuweza kupata huduma hiyo muhimu katika sekta ya
kifedha nchini Tanzania.
Maduka ya kubadirishia fedha
yaliyofunguliwa ni pamoja na katika Jengo la IPS na Hoteli ya Seacliff
jijini Dar es Salaam. Maduka mengine yamefunguliwa jijini Arusha, KIA
pamoja na Moshi.
Huduma za kubadirishia fedha za kigeni
zitakuwa zikitolewa kwenye maduka hayo kwa saa za kawaida za kazi kama
matawi mengine ya Benki ya Azania.
Uamuzi wa kufungua maduka haya mapya
maalum kwa ajili ya huduma za kubadirishia fedha za kigeni tu, unatokana
na mwongozo wa hivi karibuni wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama hatua
ya kuhakikisha watoa huduma wote wa kubadiri fedha za kigeni
wanatambuliwa na BoT.
Akizungumzia juu ya uamuzi wa Benki ya
Azania kufungua maduka hayo mapya, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo,
Charles J Itembe amesema benki inajivunia kupanua wigo wake hususani
katika kutoa huduma za kubadirisha fedha za kigeni katika maeneo
mbalimbali nchini hasa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi wa
huduma hiyo.
“Licha ya kutoa huduma ya kubadiri
fedha za kigeni, maduka haya mapya yatakuwa na uwezo wa kutoa huduma
nyingine za kibenki kama vile kufungua akaunti, kuweka na kutoa fedha
pamoja na huduma za kifedha kwenye simu za mkononi (sim banking)”.
Amesema Itembe. Itembe pia ameongeza
kuwa Benki ya Azania itaendelea kuwa na madirisha ya kubadiri fedha za
kigeni kwenye matawi yake yote nchini mbayo huwa wazi kila siku kuanzia
saa mbili asubuhi mpaka saa mbili usiku.

No comments :
Post a Comment