HATIMAYE mwili wa aliyekuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya IPP Limited, Dkt. Reginald Mengi
umezikwa katika makaburi ya familia yao yaliyopo nyumbani kwa wazazi
wake, Nkuu, Machame, wilayani hai mkoani Kilimanjaro, leo Alhamisi, Mei
9, 2019.
Mazishi ya Dkt. Mengi ambayo
yameanza na ibada katika Kanisa la KKKT, Usharika wa Moshi Mjini,
yamehudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiongozwa na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, Spika Job Ndugai, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya,
wabunge, viongozi wa dini, siasa na taasisi mbalimbali za Serikali na
binafsi.
Mengi ameacha simanzi kubwa kwa
Watanzania wengi kutokana na ukarimu wake katika kuwasaidia watu
mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu, vijana, wazee na maskini ili
kujikwamua katika wimbi la umaskini.
Akihubiri wakati wa ibada ya kuaga
mwili huo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dkt. Fredrick Shoo amemtaka Spika Job
Ndugai, Bunge na wote wenye mamlaka wakatende haki kwa watu wote.
“Nashukuru Mheshimiwa Ndugai uko
hapa. Kazi ya Bunge ni kutetea maslahi ya wananchi. Teteeni maslahi ya
wananchi mnaowawakilisha, kama kweli tunasema tumejifunza kutoka kwa Dk
Mengi,” amesema Dkt. Shoo.
Mengi alifariki dunia usiku wa
kuamkia Alhamisi iliyopita, Mei 2, 2019, nchini Dubai katika Falme za
Kiarabu na mwili wake uliwasili nchini Jumatatu, Mei 6 kabla kuagwa
Karimjee na kusafirishwa kwenda Machame ambako umezikwa leo.
Ameacha mjane, Jacqueline Ntuyabilwe, watoto wanne ambapo watatu ni wa kiume na mmoja wa kike.



No comments :
Post a Comment