Kutoka kushoto, Naibu Waziri wa
Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo pamoja na Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, John Mongella wakimsubiri Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter
Lokeris pamoja na ujumbe wake kabla ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza tarehe 01 Aprili, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John
Mongella (kushoto mbele) akiwaongoza Naibu Waziri wa Madini Nchini
Tanzania, Stanslaus Nyongo, Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter
Lokeris pamoja na ujumbe wake kwenye ukumbi wa mikutano.
Waziri wa Madini Nchini Uganda,
Peter Lokeris (wa pili kushoto) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya
kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella
Naibu Waziri wa Madini Nchini
Tanzania, Stanslaus Nyongo, akielezea mafanikio ya nchi ya Tanzania
kwenye usimamizi wa sekta ya madini kwa ujumbe wa Uganda.
Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris akifafanua jambo kwenye mkutano huo.
Naibu Waziri wa Madini Nchini
Tanzania, Stanslaus Nyongo pamoja na Waziri wa Madini Nchini Uganda,
Peter Lokeris (waliosimama katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na
wajumbe kutoka nchini Uganda na Tanzania.
………………
Greyson Mwase na Remija Salvatory, Mwanza
Waziri wa Madini Nchini Uganda,
Peter Lokeris pamoja na ujumbe wake wameanza ziara nchini Tanzania leo
tarehe 01 Aprili, 2019 yenye lengo la kujifunza namna sekta ya madini
nchini Tanzania inavyoendeshwa. Waziri Lokeris ameongozana na maafisa
waandamizi kutoka
Serikali ya Uganda pamoja na wawakilishi wa wachimbaji
wadogo. Waziri wa Madini Nchini Uganda pamoja na ujumbe wake
walipokelewa na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo
pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.
Akizungumzia lengo la ziara
hiyo kupitia mahojiano maalum aliyoyafanya na vyombo vya habari, mara
baada ya kupokelewa na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus
Nyongo, Waziri Lokeris alisema kuwa lengo la ziara yake ni kujifunza
sheria na kanuni za madini nchini Tanzania zinavyosimamiwa vyema pamoja
na uendeshaji wa shughuli za uchimbaji wa madini nchini Tanzania kwa
vitendo kupitia wawekezaji waliowekeza nchini pamoja na wachimbaji wa
wadogo wa madini.
“Tulifanya utafiti na kubaini
Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini na uzoefu mkubwa kwenye
uchimbaji wa madini na tumeona wachimbaji wadogo wakisaidiwa sana na
Serikali ya Tanzania,” Alisema Lokeris.
Aliongeza kuwa, kati ya
maeneo wanayotarajia kujifunza ni pamoja na ushirikishwaji wa wazawa
kwenye shughuli za uchimbaji wa madini (local content) utoaji wa huduma
kwa jamii inayozunguka shughuli za uchimbaji wa madini (corporate
social responsibility), usimamizi wa sheria ya madini pamoja na kanuni
zake.
Aliongeza kuwa ushirikiano wa
Tanzania na Uganda umekuwa ni wa muda mrefu na kusisitiza kuwa Serikali
ya Uganda ipo tayari kujifunza na kubadilishana uzoefu kwenye usimamizi
wa sekta ya madini.
Aliendelea kusema kuwa,
Serikali ya Tanzania inapenda kuona wananchi wake hususan waishio
vijijini wananufaika na sekta ya madini kupitia uboreshwaji wa huduma za
jamii kama vile elimu huduma za afya, na ili kuhakikisha wananchi wake
wananufaika, Serikali imeamua kutuma wataalam wake Tanzania kujifunza
kutokana na hatua kubwa iliyopigwa na nchi ya Tanzania kwenye usimamizi
wa sekta ya madini.
Akielezea changamoto kwenye
usimamizi wa sekta ya madini kwa nchi ya Uganda, Waziri Lokeris alieleza
kuwa ni pamoja na kutokuwa na teknolojia ya kutosha kwenye uongezaji
thamani wa madini pamoja na utoroshwaji wa madini unaofanywa na
wachimbaji wadogo.
Wakati huohuo Naibu Waziri wa
Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo alisema kuwa nchi ya Tanzania
ipo tayari kutoa uzoefu wake kwenye usimamizi wa sekta ya madini kwa
nchi ya Uganda kupitia wataalam wake.
Alisema katika ziara ya ujumbe
huo, mbali na nchi ya Tanzania kutoa uzoefu wake kwenye usimamizi wa
sekta ya madini nchini, wanatarajia kuupeleka ujumbe huo kwenye soko la
madini mkoani Geita lililozinduliwa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasim Majaliwa pamoja na baadhi ya
mitambo ya kuchenjulia dhahabu.
Akielezea mikakati ya Serikali
ya Tanzania kwenye usimamizi wa sekta ya madini, Naibu Waziri Nyongo
alieleza kuwa ni pamoja na uboreshaji wa sheria ya madini pamoja na
kanuni zake ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa
madini.
Alieleza mikakati mingine
kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini katika kila mkoa ili
kudhibiti utoroshwaji wa madini nchini.
No comments :
Post a Comment