Monday, April 1, 2019

SERIKALI KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAWASILIANO MIPAKANI


JPEG. NA. 1
Mhandisi Masafa wa Vodacom anayesimamia ujenzi wa mnara eneo la Katangara-Mrere, Rombo uliogharamiwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia UCSAF ili kuboresha mawasiliano akifafanua jambo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi (wa tatu kulia) wakati wa ziara yake Wilayani Rombo ya kukagua changamoto za mawasiliano
JPEG. NA. 2
Katibu Tawala wa Wilaya ya Rombo (mwenye fulana nyeupe) akimuonesha Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano (wa kwanza kushoto) maeneo yenye changamoto ya mawasiliano katika jiwe la mpaka wa Tanzania na Kenya kwenye Kijiji cha Nayeme, Tarakea Wilayani humo
JPEG. NA. 3
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga (wa pili kulia) akifafanua jambo wakati wa ziara ya kukagua changamoto ya mawasiliano eneo la Tarakea mpakani mwa Tanzania na Kenya, wilayani Rombo. Wa pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi na wa kwanza kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Abubakar Asenga wakisikiliza kwa makini
JPEG. NA. 4
Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi, akimsikiliza kwa makini mmoja wa wafanyakazi wa Tarakea mpakani akiomba Serikali iboreshe mawasiliano ya eneo hilo akiwa ziarani Rombo ya kukagua changamoto ya mawasiliano mpakani
JPEG. NA. 5
Diwani wa Kata ya Motamburu-Kitendeni, Wilayani Rombo akiongea na waandishi wa habari kuiomba Serikali iboreshe mawasiliano ya simu na redio maeneo ya mipakani wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi (hayupo pichani) ya kukagua changamoto hiyo wilayani humo
JPEG. NA. 6
Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi (aliyesimama mbele katikati) na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga (wa kwanza kulia mstari wa mbele) wakiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro walipokutana kwenye ofisi ya Wilaya ya Rombo akiwa ziarani kukagua mwingiliano wa mawasiliano mpakani mwa Tanzania na Kenya
…………………….
Na Prisca Ulomi, Rombo
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Jim Yonazi ameongoza timu ya wataalamu kutoka Wizarani, Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote (UCSAF) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya ziara ya kukagua changamoto ya upatikanaji wa mawasiliano mipakani ikiwemo mwingiliano wa mawasiliano mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya kwenye maeneo mbali mbali wilayani Rombo na uwepo wa mawasiliano hafifu kwenye maeneo hayo
“Tumeona kwamba kuna madhaifu madogo madogo, hatua zinaendelea kuchukuliwa, minara inajengwa, mawasiliano yanaboreshwa na tumekuja kuangalia maendeleo hayo ili kuhakikisha kwamba miradi hii ya kuboresha mawasiliano kwa wananchi inakwenda vizuri na wananchi wanapata mawasiliano ipasavyo ili waweze kushiriki  vizuri na kuchangia katika uchumi,” Dkt. Yonazi amesema
Pia, ameongeza kuwa tumeona maeneo mbali mbali ambayo yanahitaji huduma ya mawasiliano na yapo yanayohitaji kuboreshwa ambapo hadi sasa utekelezaji wa miradi mbali mbali ya kuboresha mawasiliano mipakani  inaendelea kufanyika na tupo na wenzetu wa UCSAF ambao wanaendelea kuratibu na kuhakikisha kwamba miradi hii inaenda vizuri na tuna amini kabisa baada ya muda si mrefu eneo lote hili la mpakani ambapo tumeanza hapa na kuna maeneo mengine kama kule Sirali na kusini kwenye mpaka wetu na nchi ya Msumbiji tunahakikisha kwamba yote haya yanakuwa na mawasiliano bora kwa sababu za kiuchumi lakini pia mawasiliano yanahusiana na masuala ya usalama ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa salama na uchumi wetu unaendelea
Amefafanua kuwa Serikali inafanyia kazi mawasiliano yote kwa ujumla yanayohusu mawasiliano ya simu, mawasiliamo ya redio na mawasiliano ya televisheni kwa kuwa tunataka  wananchi popote walipo waweze kupata mawasiliano haya kwa aina mbali mbali kama ambavyo wananchi walioko Dar es Salam au Dodoma au Morogoro wanaweza kupata mawasiliano na tunapenda vile vile wananchi wetu walio kwenye maeneo ya mipaka waweze kupata  huduma kama hizi
“Kuna maeneo ambayo yana changamoto mbali mbali kama ambavyo yametengwa kutokana na hali ya kijiografia kama milima, yote hiyo tunataka kuhakikisha kwamba tunapeleka minara na mawasiliano ili wote waweze kupata mawasiliano ama yawe ya simu, redio au televisheni ili yote yaweze kupatikana, hivyo tunaendelea kuchukua kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma wanayohitaji,” amesisitiza Dkt. Yonazi
Pia, amefurahishwa na wananchi wa Rombo kwa nia ya kushiriki kwenye shughuli za kimaendeleo kwa kuwa wanadai mawasiliano, tunahakikisha wanapata mawasiliano ambayo wanayahitaji na muda si mrefu kote hapa kutakuwa na mawasiliano mazuri,  tumeona minara mbali mbali ya Halotel, TTCL ambapo miradi inaendelea kutekelezwa, kwa hiyo wananchi wasiwe na wasiwasi, mawasiliano yatakuwa bora na watashiriki vizuri katika shughuli za maendeleo
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Rombo, Abubakar Asenga amesema kuwa Rombo ni Wilaya yenye changamoto ya mawasiliano ya redio na simu ambapo ziara ya Dkt. Yonazi ya kupita maeneo mbali mbali ambapo ameona mwenyewe baadhi ya maeneo anapata mawasiliano kwenye simu yake na mengine hapati mawasiliano, tuna imani ataenda kufanyia kazi ili wananchi waweze kusikia yale mazuri ambayo yanafanywa na Mhe. Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kupitia TBC na vyombo vingine vya habari kwa kuwa usikivu wa redio uko chini ya asilimia 60.
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa wanaendelea kutoa  ruzuku kwa niaba ya Serikali na kuzipatia kampuni za simu ambapo UCSAF wamekuwa na mradi wa kuongeza usikivu wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani ili kuweza kuongeza biashara mipakani na kuimarisha ulinzi ambapo miradi hiyo imetekelezwa  Wilaya ya Rombo miradi mingine minne ya kuongeza usikivu katika eneo hilo itatekelezwa
Pia, amekiri kuwa kupitia ziara hiyo, UCSAF imepata uelewa zaidi wa matatizo ya eneo la Rombo kwa kuwa sehemu kubwa ya Wilaya hiyo ina mlima Kilimanjaro ambao umekuwa kama ukuta unaozuia mawasiliano na inaruhusu mawasiliano ya nchi za jirani,  jukumu letu ni kuboresha mawasiliano yanayotoka kwenye kampuni za mawasiliano za Tanzania ili kuongeza usikivu wa mawasiliano ya simu ambapo kwa upande wa mawasiliano ya redio tayari tuna ushirikiano baina yetu na TBC ili kuweza kuhakikisha kuwa redio za Tanzania zinasikika na tutaendelea kushirikiana na TBC kuongeza vituo zaidi vya mawasiliano ya redio katika Wilaya hii ili kuhakikisha kwamba wananchi wanafaidika na kusikiliza habari kutoka Tanzania
Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kaskazini ya TCRA, Mhandisi Imelda Salumu amesema kuwa TCRA inashughulikia ukosefu wa mawasiliano ama mwingiliano wa mawasiliano hasa  maeneo ya mipakani na tayari wamefanya ziara ya kutembelea maeneo ya mipaka ya kaskazini kwa kuwashirikisha watoa huduma wa Tanzania na wa nchi ya jirani ya Kenya pamoja na mdhibiti wa mawasiliano wa upande wa nchi hiyo ili kuhakikisha kuwa vigezo vilivyowekwa na Umoja wa Watoa Huduma na Wadhibiti wa Mawasiliano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACO) vinatekelezwa ili wananchi waweze kupata mawasiliano ambayo hayana mwingiliano na wanaendelea na hatua ya pili ya kuhakikisha kuwa maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa au yenye mawasiliano hafifu, kwa kushirikiana na watoa huduma yanapata mawasiliano. Aidha, wamepokea maombi na wanayashughulikia ya watoa huduma wengine wawili ya kutoa huduma za mawasiliano ya redio mipakani ili kuondoa mwingiliano wa redio kama ilivyo kwa TBC ambao wanapatikana mpakani ili kuondoa tatizo la watanzania kusikiliza redio za nchi jirani  

No comments :

Post a Comment