Serikali imesema kuwa imekusanya
Sh. Milioni 3,010.5 kwa mwaka fedha 2016/17 na Sh. Milioni 2,545.6 kwa
mwaka wa fedha 2017/18 za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika
taulo za kike(sanitary pads) zilizozotengenezwa nchini na zilizoingizwa kutoka nje ya nchi.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Upendo Peneza
(Chadema) aliyetaka kujua Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyokusanywa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/17 na 20017/18.
Dkt. Kijaji alisema kiasi hicho
cha kodi kilikusanywa kabla ya kuondolewa kwa asilimia 18 ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT)Juni, 2018.
Katika maswali ya nyongeza,
yaliyoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Dkt. Immaculate Swale kwa
niaba ya Mhe. Peneza, alisema pamoja na Serikali kuondoa baadhi ya kodi
katika uzalishaji wa taulo za kike lakini bado bei ya bidhaa hiyo ipo
juu, na kutaka kujua mkakati wa Serikali kushusha bei ya bidhaa hiyo ili
kuhakikisha inawafikia walengwa.
“Kama Serikali imeshindwa
kusimamia kushuka kwa bei, haioni kwamba iendeleze zile kodi za awali
lakini kodi hii ikusanywe na iwe refinance ili kuweza kununulia hizi taulo za kike na izigawe bure mashuleni”, aliongeza Dkt. Swale.
Akijibu maswali hiyo, Dkt. Kijaji
alisema kuwa Serikali haijashindwa kusimamia bei ya bidhaa hizo na kwa
sasa inaendelea kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi ili kuona
namna bora ya kuwafikia walengwa.
Alisema Serikali inaendelea
kufanya tafiti mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuona namna ya
kuwasaidia watoto wa kike ila kuna changamoto kodi inakusanywa ikiwekwa
kwa ajili ya kununua na kugawa taulo za kike mashuleni.
“Yapo makundi mengine ambayo kodi
zinazotozwa kwenye bidhaa zinazotumika na makundi hayo, tutatengeneza
ombwe la kila kundi kuja kuomba kodi inayotozwa kwenye makundi hayo
waweze kupewa wao”, alisema Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji alishauri kuwa
kinachotakiwa kufanywa ni kubuni njia nyingine ili kuona watoto wa kike
wanaweza kupata bidhaa hii bila kuhusisha kodi, au tozo zozote
zinazotozwa katika bidhaa hii kwasababu imebainika kuwa inapoondolewa
kodi wanaonufaika ni wazalishaji kwa kuwa taifa lipo katika soko huria.
No comments :
Post a Comment