Mariam Rajab Juma (25) akiwa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako ameanza kupatiwa matibabu ya
kidonda kinachomsumbua mgongoni sehemu ya bega la kulia. Wataalam
wamesema atahamishwa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Mariam akiwa wodini leo wakati waandishi wa habari wakimhoji kuhusu maendeleo ya afya yake.
………………………
Baada
ya Mariam Rajab Juma (25), mkazi wa Singinda kufanyiwa vipimo
mbalimbali ili kubaini ugonjwa unaomsumbua, wataalam wa Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) wameshauri ahamishiwe Hospitali ya Saratani ya
Ocean Road kwa ajili ya kupatiwa matibabu
zaidi.
Wiki
iliyopita Mariam alifikishwa Muhimbili akitokea mkoani Singida na
kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini ugonjwa unaomsumbua katika
kidonda kilichopo sehemu ya bega la mkono wake wa kulia.
Akizungumza
leo na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Muhimbili,
Dkt. Ibrahim Mkoma amesema Mariam ataanza matibabu rasmi katika
Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na kwamba baada ya kumaliza matibabu
atarejeshwa Muhimbili kuendelea matibabu zaidi.
Dkt.
Mkoma amefafanua Mariam atahamishiwa Hospitali ya Saratani ya Ocean kwa
kuwa kuna baadhi huduma za matibabu ambazo anapaswa kupatiwa katika
hospitali hiyo kutokana na ugonjwa unaomsumbua.
Daktari
alipoulizwa kuhusu ugonjwa unaomsumbua Mariam, Dkt. Mkoma amesema suala
la ugonjwa ni siri ya mgonjwa na wataalam wa hospitali na kwamba
taratibu za hazimruhusu kuweka wazi aina ya ugonjwa unaomsumbua
mgonjwa.
Naye
Mariam amesema amefurahishwa na huduma nzuri ya matibabu aliyopatiwa na
walaam wa Muhimbili kwani tangu alipofikishwa hapa amekuwa akihudumiwa
vizuri.
“Hivi
sasa naendelea vizuri, tangu nimekuja Muhimbili naendelea vizuri. Kabla
sijafika Muhimbili nilikuwa siwezi kutembea vizuri lakini sasa naweza
kutembea vizuri,” amesema Mariam.
Mariam
alifanyiwa vipimo vya CT-scan ya kifua na kichwa, Ultrasound pamoja na
vipimo mbalimbali vya damu ambavyo vimesaidia kubaini ugonjwa
unaomsumbua Mariam.
Dkt.
Mkoma amesema kidonda kilichopo sehemu ya mgongo wa Mariam ni kidonda
sugu ambacho kilihitaji kufanyiwa vipimo mbalimbali kubaini ugonjwa
unaomsumbua.
Awali,
Mariam amesema aliwahi kuugua moto akiwa na umri wa miaka mitano ambapo
alitibiwa na kupona ingawa alibaki na kovu kubwa kuanzia sehemu ya
mgongo wake hadi kwenye kisogo.
Amesema
mwezi wa nane mwaka jana alipata kipele kwenye kovu na baadae kipele
hicho kugeuka kuwa jipu. Alipotumbua jipu lilitoa usaha na kisha kuanza
kuota kidonda kilichoendelea kuongezeka siku hadi siku.
“Nilienda
kutibiwa katika Hospitali ya Makiungu iliyopo Manispaa ya Singida,
lakini pia kutokana na wazazi wangu kutokua na uwezo wa kifedha niliacha
kwenda hospitalini na kuanza kusafisha kidonda mwenyewe, huku
nikiwaomba marafiki zangu niliosoma nao sekondari wanichangie fedha ili
niweze kununua dawa,” amesema Mariam.
No comments :
Post a Comment