Mkuu wa Wilaya wa Mvomero Mhe.
Mohamed Utaly (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Kaimu Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Waislam Morogoro(MUM) Dkt.Abdallah Yahya Tego wakielekea
katika ukumbi wa Hema Jeupe kulikofanyika mashindano ya kuhifadhi na
kusoma Qur’an leo mkoani Morogoro.
Mkuu wa Wilaya wa Mvomero Mhe.
Mohamed Utaly (wa pili kulia) akifatilia mashindano ya kuhifadhi na
kusoma Qur’an yaliyo fanyika leo katika Chuo Kikuu cha Waislam
Morogoro(MUM).
……………………..
Na.Majid Abdulkarim, Morogoro
Taasisi za elimu nchini zimetakiwa
kuwalea wanafunzi katika maadili mema ili kuwajengea
misingi bora
katika utendaji na kuleta uadilifu katika kuhudumia jamii
inayowazunguka.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa
Wilaya wa Mvomero Mhe. Mohamed Utaly aliyemuwakilisha mgeni rasmi Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(OR-TAMISEMI) Mhe.Selemani Jafo katika mashindano ya kusoma na kuhifadhi
Qur’an yaliyofanyika leo Chuo Kikuu Cha Waislam Morogoro (MUM).
Aidha Mhe.Utaly amesisitiza kuwa
taasisi za elimu kubadili mitazamo ya wanafunzi wao ili kujenga mitazamo
chanya yenye kusaidia katika utendaji na kufikia malengo yanayotakiwa.
Hata hivyo Mhe.Utaly amesema kuwa
ili kupata utendaji bora lazima kuwa muadilifu,mcha Mungu, kuwa na
huruma kwa wale unao waongoza na kuwa mzalendo katika kuleta maendeleo
endelevu .
Wakati huo huo Mhe.Utaly ameongeza
kuwa kila mtanzania anawajibu wa kuimarisha maadili katika jamii
inayomzunguka ili kupata watendaji waadilifu makazini na wazalendo
katika kulitumikia taifa.
“Kila msomi hapa nchini anawajibu
wa kuelimisha jamii inayomzunguka ili kubadili mitazamo potofu iliyo
jengeka katika nyoyo za baadhi ya watu na kukemea matendo maovu ya
ubakaji, ulawiti na mauaji ” Aliongezea Mhe.Utaly
Lakini pia Mhe.Utaly amesema kuwa
watanzania wawe tayari kutoa ushirikiano katika kuzuia matendo maovu
katika jamii ili kudumisha Amani kwa watanzania.
Mhe. Utaly ameendelea kusema kuwa
Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero inafursa mbali mbali na kuwataka
watanzania kuchangamkia fursa hizo.
“Karibuni Mvomero kuna fursa ya
kilimo , viwanja na nyingine nyingi ambazo zitahamasisha kuleta
maendeleo katika nchi yetu” Amehitimisha Mhe.Utaly
Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu
wa chuo MUM Dkt.Abdallah Yahya Tego amesema kuwa chuo kinamalengo ya
kujenga hospitali ya Rufaa Mkoani Lindi, kuanzisha kozi za uchimbaji wa
gesi na mafuta na kuanzisha chuo cha Biashara Mkoani Dar es salaam.
Mashindano hayo yalianzishwa mnamo
mwaka 2011na jumuiya ya kusomesha na kuhifadhi Qur’an MUM baada ya kuwa
wamepata mwaliko kutoka nchini Uganda walipokwenda kushiriki katika
mashindano ya kusoma na kuhifadhi Qur’an katika Chuo Kikuu cha Kiislam
Uganda.
No comments :
Post a Comment