Na Lydia Churi na Dennis Buyekwa-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa uelewa wa sheria, ujuzi na tabia ni
mambo matatu muhimu wanayotakiwa kuwa nayo Majaji wa Mahakama ya Rufani
ili yaweze kuwasaidia katika kutoa maamuzi kwenye mashauri.
Akifungua Mkutano wa mwaka wa
Majaji wa Mahakama ya Rufani wa kutathmini utendaji
kazi wa Mahakama
hiyo wa mwaka 2018 na kuweka mikakati ya kazi kwa mwaka 2019, Jaji Mkuu
alisema Majaji kuwa na uelewa wa sheria na ujuzi haitoshi pasipo
kujenga tabia ya kufanya kazi kwa kasi na kwa weledi.
“Uvivu, uchonganishi, kulalamika
pamoja na ubishi usio na mwelekeo ni tabia za kibinadamu zinazoweza
kuathiri utendaji kazi kwa kuchelewesha upatikanaji wa haki”, alisema
Jaji Mkuu.
Alisema Majaji wanao umuhimu wa
kipekee katika jamii hivyo hawana budi kutoa haki kwa kufuata sheria ili
wananchi waweze kuwa na imani na mfumo wa utoaji haki pamoja na utawala
wa sheria.
“Kupitia mkutano huu mtapata fursa
ya kubadilishana uzoefu wa namna ya kumaliza mashauri kwa kasi kwani
utoaji haki uko katika utamaduni ambao haujaandikwa popote hivyo naamini
mtaibua tamaduni zitakazorahisha utoaji wa haki”.
Akizungumzia ongezeko la idadi ya
Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu alisema kuongezeka kwa Majaji
hao kutasaidia Mahakama kupunguza changamoto ya mlundikano wa mashauri
ya muda mrefu yaliyopo Mahakamani. Hivi sasa kuna Majaji 21 wa Mahakama
ya Rufani ambapo awali kulikuwa na Majaji 15.
Kuhusu changamoto, Jaji Mkuu
alisema Mahakama inakabiliwa na upungufu wa bajeti kwa ajili ya vikao
vya kusikiliza mashauri. Alisema endapo kungekuwa na bajeti ya kutosha
vikao vingi Zaidi vya mashauri vingefanyika na kumaliza mlundikano wa
mashauri ya muda mrefu.
Alisema sheria imerekebishwa na
kuwapa mamlaka Mahakimu na Manaibu Wasajili kusikiliza mashauri ya
Mahakama Kuu hususan yale yanayohusu migogoro ya Ardhi ambapo hatua hii
itasaidia kupunguza mashauri mahakamani. Aliongeza kuwa ili Mahakama
iweze kuwatumia inahitaji kuongezewa bajeti Zaidi ya iliyopo sasa.
Mkutano wa Mwaka huu wa Majaji wa
Mahakama ya Rufani pia umewashirikisha Manaibu Wasajili, wasaidizi wa
kisheria wa Majaji, Makarani na watunza kumbukumbu ili waweze kusaidiana
na Majaji kupanga mikakati ya kumaliza mashauri kwa wakati.
No comments :
Post a Comment