Friday, March 29, 2019

WAZIRI WA MAJI PROF.MBARAWA AKAGUA MIRADI YENYE CHANGAMOTO MKOANI SONGWE


A
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akiwasili ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Generali Mstaafu Nicodemus Mwangela katikati ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe David Kafulila.
B
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Generali Mstaafu Nicodemus Mwangela.
C
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akipata maelezo ya ujenzi wa tanki (halipo pichani) kutoka kwa Mhandisi wa Maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya Mhandisi Ndele Mengo. Kushoto kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Momba Halmashauri ya Tunduma Bw. Juma Said Irando.
D
Moja ya miundombinu ya maji inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ambapo Waziri Mbarawa alifika kukagua ujenzi huo.
…………………………
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) leo ameanza ziara ya kukagua miradi ya maji mkoani Songwe hususan miradi yenye changamoto ambayo imechukua
muda mrefu kukamilika.
Waziri aliyasema hayo alipofika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas Mwangela mara tu baada ya kuwasili ofisini kwa Mkuu wa mkoa huyo.
“Nimekuja kukagua miradi ambayo ina changamoto kubwa ambayo haijakamilika kwa muda mrefu na wananchi wanaisubiri kwa muda mrefu” alisema Profesa Makame Mbarawa.
Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeahidi kwamba ifikapo mwaka 2020 kwenye miji mikuu ya mikoa wananchi wawe wamepata maji asilimia 95 na miji ya wilaya asilimia 90 na vijijini asilimia 85.
Hata hivyo, Waziri alisisitiza kwamba tunapopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maji inabidi lazima tusimamie kwa uadilifu, ukaribu zaidi na kuhakikisha kwamba wakandarasi wanaolipwa pesa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji wanaanza kazi mara moja baada ya kulipwa, kwa sababu wakandarasi wengine wamekuwa na tabia ya kuchukua pesa za miradi ya maji na kupeleka kwenye miradi mingine.
Naye, Mhandisi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya, Mhandisi Ndele Mengo akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Itumba Isongole amesema Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Singilimo Enterprises Ltd. ya jijini Dar es Salaam ambapo gharama ya mradi ni Tsh. 804,162,330/= na hadi sasa ameshalipwa Tsh. 313,238,780/= ambazo zikihusisha uchimbaji wa mitaro kwenye bomba kuu chanzo cha umbali wa mita 4332 na ulazaji wa bomba za plastic wenye kipenyo cha nchi 8 umbali wa mita 3924 pamoja na tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita laki. Mradi huu amesema unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya. Matazamio ya kukamilika kwa mradi huu ni 30/5/2019.
Aidha, Waziri Profesa Mbarawa ameagiza mradi wa Itumba Isongole uwe umekamilika ifikapo tarehe 30/5/2019 na mradi wa maji wa mji wa Tunduma uwe umekamilika ifikapo 13/4/2019 ili wananchi wapate majisafi na salama kwa sababu karibu wakandarasi wote wameshalipwa pesa zao walizokuwa wanaidai Serikali. 

No comments :

Post a Comment