Friday, March 1, 2019

UJUMBE WA KWARESMA 2019 ULIOTOLEWA NA BARAZA LA MAASKOFU TANZANIA TEC

1
FAMILIA KANISA LA NYUMBANI
NA NI
SHULE YA IMANI NA MAADILI

Utangulizi
Wapendwa Waumini,
Kaka na Dada katika Familia ya Mungu,
Na Watu Wote wenye mapenzi Mema,
TUMSIFU YESU KRISTU!


 UTANGULIZI

1.1              Ujumbe wa Kwaresima 2019
Kama ilivyo ada kila mwaka, sisi Maaskofu Katoliki hutoa ujumbe mahsusi katika kipindi cha Kwaresima. Kila ujumbe huwa na dhamira maalum ya kuzingatia, ili katika kujitafakari na kuamsha upya maisha yetu ya Imani Katoliki na Maadili yake, tutambue zaidi na tukiri kwa
dhati jinsi hali yetu ilivyo mbele ya Mungu ambaye ndiye chanzo cha utakatifu, na sisi kama wadhambi tulio safarini kuelekea huo utakatifu. Hivyo basi, kwa mwaka huu wa 2019 baada ya kuadhimisha miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania mwaka jana 2018, tumeona ujumbe wa mwaka huu uzingatie dhamira inayohusu familia zetu. Dhamira hii ni “Familia kama Kanisa la Nyumbani na Shule ya Imani na Maadili”.  Kwa mwaka huu basi, tutafakari kwa namna gani hili lifanyike kwa kuzingatia kuwa Familia ya Kikristu ni Shule ya Imani Katoliki na Maadili yake.




SURA YA KWANZA
FAMILIA NI MSINGI WA JAMII YA KIBINADAMU



1.1              Mwaka 2019 kuwa Mwaka wa Familia: Matunda ya Adhimisho la Jubilei, Miaka 150 ya Uinjilishaji

Kwa kuzingatia hayo, sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, pamoja na kuwa na dhamira hiyo, tumeuteua mwaka huu wa 2019 kuwa ni Mwaka wa Familia, kama ishara na fursa ya kutafakari kwa undani zaidi matunda ya adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania kama Familia ya Mungu. Uamuzi huo unajengwa juu ya sababu kuu nne za msingi kuhusu mwaka huu wa 2019.

Kwanza,ni miaka ishirini na mitano tangu ilipoazimishwa Sinodi ya kwanza ya Afrika, ambapo Kanisa lilikubaliana na mtazamo wa Kiafrika kuwa Kanisa ni Familia ya Mungu. Kwa hivyo, kiimani na kijamii binadamu anakiri kwamba familia ndiyo msingi wa jamii ya kibinadamu, na hivi kuijenga familia imara ni kuwa na jamii na Kanisa imara. Mababa wa Kanisa walielezea familia kuwa ni kiini cha kwanza na cha uhai wa jamii. Kama tunavyosoma kutoka Ecclesia in Africa, “Kwa kuwa Muumba wa vitu vyote ameanzisha ushirika wa mume na mke kama asili na msingi wa jamii ya kibinadamu, familia ni kiini cha kwanza cha uhai wa jamii.” (Ecclesia in Africa no. 85). Lakini Kwaresima hii tunaalikwa kutambua utume wa Familia kupitia wanafamilia ambao wengi wao ni walei, kama Mababa wa Kanisa wanavyotuambia kwenye Mtaguso wa Pili wa Vatikano: “Ni juu ya walei ,kutokana na wito wao, kutafuta ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadri ya Mungu. Wanaishi ulimwenguni, yaani katika kazi zozote na shughuli za kidunia na katika mazingira ya kawaida ya maisha ya kifamilia na ya kijamii, ambayo maisha yao yamefungamanishwa nayo. Hapo wanaitwa na Mungu kusaidia kuutakatifuza ulimwengu, kama kutoka kwa ndani, mithili ya chachu, katika kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya kiinjili, na hivyo wamdhihirishe Kristo kwa wengine, waking’aa hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, imani, matumaini na mapendo. Kwa hiyo yawahusu hao kwa namna ya pekee kuyatangaza na kuyapanga mambo yote ya kidunia, ambayo wamefungamana nayo, ili daima yafanyike na kukua kadri ya Kristo na kuwa kwa sifa ya Muumba na Mkombozi”(Lumen Gentium no. 31). Ili hiki kitelezeke inabidi familia iwe imara kiimani na kimaadili.
                                                                                                        
Pili, mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka ishirini na tano tangu pale Umoja wa Mataifa ulipotamka kuwa mwaka 1994 ni mwaka wa familia. Ni vema tukanukuu maneno ya msingi kuhusu nia ya Umoja wa Mataifa kwa kutenga mwaka huo kuwa ni mwaka wa familia.Umoja wa Mataifa ulitamka kwamba:

“Familia inaunda kitengo cha msingi cha jamii na kwa hiyo inahitaji kuhakikishiwa uangalizi maalum. Hivyo basi, ulinzi mpana kabisa iwezekanavyo na msaada husika lazima vitolewe kwa familia zote ili nazo ziweze kuchukua majukumu yake ndani ya jamii, kutokana na matakwa ya  Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu, Tamko kuhusu Ustawi na Maendeleo ya Kijamii, na Mkataba wa Kufutilia Mbali Namna Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake”[1].

Familia ni kitovu/kiini cha jamii (cell of the society) na ni lazima ijengeke katika hadhi ya binadamu kadri ya hulka ya binadamu iliyokusudiwa na Muumba, na sivyo inavyotafsiriwa bila kurejea kwa Mungu.Hii ndiyo italeta umaana wa familia kuwa msingi wa jamii. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili anathibitisha kuwa ukweli unaojikita kwenye hulka upo kwenye jamii tayari kama wote tuko kwenye hulka aliyoitengeneza Mungu kama wote tunakubaliana naye. “The splendour of truth shines forth in all the works of the Creator and, in a special way, in man, created in the image and likeness of God (cf. Gen 1:26). Truth enlightens man’s intelligence and shapes his freedom, leading him to know and love the Lord” (Veritatis Splendor page no.1).


Tatu, mwaka huu pia ni mwaka wa Jubilei ya Miaka 50 tangu Halmashauri ya Walei ya Kanisa Katoliki ilipoanzishwa mwaka 1969. Kwa kuwa Halmashauri ya Walei katika ngazi zake zote inayo Kamati Ndogo inayohusika na Familia na Malezi, ni haki na ni vema Dhamira ya Familia ikawa ndiyo kiini mwafaka cha ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka huu tunapoidhimisha Jubilei hiyo. Na hasa kwa sababu zaidi ya asilimia 90 ya Waumini Wakatoliki ni walei wanaotakatifuza malimwengu kupitia maisha ya kitume katika familia zao, kama baba na mama, au babu na bibi, au mjomba na shangazi, au kaka na dada, shemeji au binamu. (Gaudium et Spes, no. 43 / Lumen Gentium, no. 31, 33).

Nne, mwaka huu pia ni adhmisho la mwaka wa Jubilei ya Dhahabu (Miaka 50) tangu chama cha kitume kinachowaunganisha wanafunzi wote Wakatoliki walioko sekondari; chama kinachojulikana kwa jina la Young Catholic Students, au kwa kifupi YCS. Kwa kuwa vijana bado wako chini ya wazazi wao na familia kwa upana wake kimalezi na kimakuzi, ni mwafaka basi tukatafakari kwa namna gani familia zinaweza kuwa kweli shule za Imani Katoliki na Maadili Yake kwa vijana hawa ambapo kwa sasa tunaona wengi; idadi yao kitakwimu ni takribani zaidi ya milioni moja na laki saba kidato cha kwanza hadi cha sita. Hiki chama cha kitume katika jubilei yao ya miaka hamsini hatuna budi kama familia tutafakari upya tuwaongezee malezi gani ili wawe raia wema zaidi, na hatimaye waweze kuwa msingi katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani na mbinguni.

1.2              Haja na Hoja ya Kuitafakari Familia

Leo hii, baada ya neema, baraka na mwanga zaidi wa Jubilei ya miaka 150 kuhusu nini maana ya kuwa Mkristu; maana na utume wa Familia ya kikristu ni vitu ambavyo haviwezi kuendelea kuchukuliwa juujuu tu; ni lazima vitamkwe kwa dhati, vielezwe upya, vitetewe bila mashaka yoyote, na wanafamilia wenyewe watoe ushuhuda kwa jamii nini maana ya familia, kuwa ni Kanisa la nyumbani, na hivyo kuwa ni Shule ya imani na maadili.

 Sababu kuu ya kuwa na msimamo thabiti juu ya familia ni nini na ndoa na maana halisi ya ndoa, ni kwa sababu leo hii kuna dhana potofu na hata nadharia zisizo sahihi zinazolenga kuhalalisha vitendo vinavyopelekea kutenganishwa kwa ndoa na familia.

Kutenganisha huku kunatokana na dhana yenye maana potofu ya ndoa inayotolewa kwamba ndoa ni maridhiano ya wawili bila kufungamanishwa na jinsia zao. Hii ni maana potofu inayotetewa na baadhi ya jamii. Hii ni dhana iliyopotoka kihulka (unnatural), kiimani na kimaadili. Imani Katoliki na maadili yake inapingana kabisa na mtazamo wa namna hii, au hoja zinazoweza kutokana na mtazamo kama huo.

 Hii ni kwa sababu Muumba wa vitu vyote ameisimika taasisi ya familia kwa kuweka muungano wa kindoa kati ya mwanaume na mwanamke kuwa ndiyo chanzo na msingi wa jumuiya ya kibinadamu, yaani familia.

Kwa maana hiyo, familia ndiyo kiini cha kwanza cha uhai wa jamii. Siku zote tutilie maanani kuwa katika mpango wake Mungu Muumba, mahali pa msingi ambamo watu wanajifunza kuwa watu ni kwenye familia. Hii inamaanisha kuwa ni katika familia ambamo kila mtoto kwanza anajifunza uwepo wa Mungu, kumpenda Mungu huyu, kutenda yanayoendana na huyu Mungu na mtoto huyu kutamani kuungana na Mungu huyu milele. Mtoto hupokea haya kutoka kwa wazazi wake na walezi wake, yaani kutoka kwenye familia.

1.3 Changamoto Zinazoikabili Familia ya Sasa
Kazi kubwa ya Kristo ilikuwa ni kumkomboa mwanadamu dhidi ya dhambi na matokeo yake mabaya (Rej.Lk. 4:18-19; Lk. 5:20, 27-32). Kanisa kama mwili wa fumbo wa Kristo linao wajibu wa msingi wa kuendeleza kazi ya Kristo kwa wanadamu.  Mahali pazuri pa kufanya kazi hiyo ni kupitia familia ambapo mtu hupata uhai na malezi ya kiutu na kiroho.
Kwa kuzingatia hali ya sasa na changamoto zake katika familia na ndoa jitihada zozote za kuelimisha jamii juu ya mpango wa Mungu kwa kila binadamu hapa duniani, lazima familia zetu zijipange kukabiliana na changamoto zile  zinazoukabiri ulimwengu wetu wa sasa katika karne ya ishirini na moja na nchi yetu ya Tanzania ikiwemo. Changamoto hizo ni kama vile:-
·         Talaka, 
·         Ndoa za utotoni
·         Uchumba sugu
·         Ndoa za mitaala
·         Kukosa uaminifu ndani ya ndoa
·         Ndoa za kurithi wajane
·         Ndoa za Jinsia moja
·         Ndoa baada  ya ndoa ya kwanza halali
·         Ndoa zisizo na watoto
·         Kubadili maumbile
Ø  Familia za mzazi moja
Ø  Familia zenye mchanganyiko wa Imani
Ø  Familia zinayoishi katika mazingira magumu ya uchumi
Ø  Familia zenye watoto walemavu
Ø  Familia zisizo na mzazi hata mmoja
Ø  Familia zisizoishi imani
Ø  Familia zisizo na maadili
Ø  Familia zilizopoteza uwezo wa kulea
Ø  Familia zisizo na kipato.



Asili ya matatizo katika ndoa na familia ni pamoja na:-
1.3.1        Utamaduni na Mazingira.
Tunaishi katika historia yenye mazoea, mila, desturi na mapokeo ya wazee wetu.  Iko sehemu ya utamaduni wetu isiyokubaliana na ukweli wa kimungu ambao ni wa lazima katika kuishi ndoa safi na familia bora. Mpaka sasa katika mazingira yetu zipo tamaduni zinazoruhusu talaka, ndoa za utotoni, uchumba sugu, ndoa za mitaala, “nyumba ndogo”, ndoa za kurithi wajane, ndoa za jinsia moja na ndoa baada ya ndoa ya kwanza halali.

 Ni jukumu la kila mkristu, ndani ya familia, kuchekecha utamaduni wake, kwani kumekuwa na chenga zisizopita katika chujio la Kristo aliye Mwanga wa maisha yetu.

1.3.2        Harakati za kila mmoja ambazo zinalenga moja kwa moja kuibomoa familia
Harakati hizi zinatangaza na kupigia upatu uhuru usio wa kweli kwa mwanadamu.  Zinapotosha ukweli kwa kutenganisha ukweli wa maisha na ukweli wa asili katika viumbe na maumbile yao.  Maisha ya kiroho, maisha ya ndoa na familia, yanakuwa ni jambo binafsi na la faragha bila kuhusisha jamii na wala kumhusisha Mungu.  Uhusiano wa mtu na jamii unahuishwa katika sheria tu ambazo jamii inazitunga na kuzibadili mara kwa mara.
Matokeo mabaya ya harakati hizi ni kukithiri kwa ubinafsi, kuenea na kuzagaa kwa matukio yenye kuchochea waziwazi tamaa za ngono kati ya watu wa rika zote. Wimbi kubwa la maisha huria, bila malengo wala kanuni na nidhamu ya kukataa malengo mema.

Kuongezeka kwa mifarakano ya ndani ya nafsi na hivyo mifarakano kati ya mtu na mtu ndani na nje ya familia kunakoshuhudiwa na matatizo ya msongo wa mawazo, hali ya kukata tamaa.
Harakati hizi zimejaa kwa wengi, na pia mtazamo potofu kuhusiana na maadili katika ndoa na familia. Na hivi mtu kufikia mahali kujiaminisha kwamba maisha yanawezekana bila Mungu na bila utu.

Msimamo huu haumwezeshi mtu kupokea na kudumisha tunu njema za maisha ya ndoa na familia, ambazo kuasisi tunu hizo huzifanya ndoa na familia zifanyike katika kweli na zidumu na kusitawi na kuzaa matunda.
Changamoto za ndoa na familia kimsingi ni changamoto za kukubali na kupokea tunu za maisha ya ndoa na familia. Tunahitaji kujihoji mbele ya Kristo juu ya wito wa kuwa wavumilivu, wasamehevu, wenye kiasi na wenye subira Rej. 1Kor.13:1-8).

Tunahitaji kujipima tena kama tunazithamini na kuvutiwa nazo zile heri nane alizozitangaza Bwana wetu Yesu Kristo ambazo ni usafi wa moyo, upole, unyenyekevu, upatanisho, kuudhiwa kwa ajili ya haki, kukubali kushindwa/kudhulumiwa kwa sifa na utukufu wa Mungu (Mt.5:3-12).

Tunahitaji kujithamini mbele ya Mungu, kuona thamani ya upendo wa Kristo kwetu na wa yule aliyetupatia Kristo.  Maana “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye” (Rum.8:32). Hakuna anayeweza kututenga na upendo wa Kristo (Rum.8:35-39).
Utatuzi wa matatizo mengi katika ndoa unajikita kimsingi katika changamoto ya kurudisha sura njema ya maagano kati ya Mungu na katika utakatifu kati ya Kristo na Kanisa lake (Rej.Waefeso 5:21-25).

Wakristo wenye ndoa na ni wazazi kwa njia ya ubatizo wao wanawajibika kutoa mchango wao wa pekee kwa ajili ya kufafanua mafundisho na tunu za kiinijli katika mazingira na tamaduni mbalimbali za leo ambamo kwazo wanafamilia huishi maisha ya familia. Wanandoa kwa namna ya pekee wamestahilishwa jukumu hilo kwa sababu ya karama yao na jukumu lao la kisakramenti hasa sakramenti ya ndoa. Wanandoa kwa kuheshimu mpango wa Mungu hubeba jukumu kuu la kuwa wazazi ambapo hukubaliana na wito wa Mungu kuwaleta duniani watoto. Mungu huendeleza kazi yake ya uumbaji na kuendeleza uhai wa kimwili na kiroho kwa kuwatumia wazazi. Hivi kukubali kuwa mwanandoa ni kukubali jukumu la kuuweka uhai wa binadamu kuwa ni jukumu la kimungu linalomtaka mtu amsikilize Mungu Muumbaji na anaye- takatifuza.
1.4 Hali ya Familia katika Ulimwengu wa Leo
Katika ulimwengu wa leo, familia hujikuta katika hali ambayo uhuru wa mtu binafsi huonekana kuwa na nguvu kubwa katika kufanya maamuzi juu ya maisha ya ndoa. Kwa watu wenye kufuata utamaduni huu huathiri tunu za ndoa zinazotokana na Injili. Hulka ya binadamu na utu wa mwanandoa huonekana kutenganishwa na kusudio la Mungu la kumuumba mwanadamu. Mungu amemuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake yaani ukutanapo na mwanadamu kwa kutumia milango ya fahamu na akili unapaswa kuuona uwepo wa Mungu aliye hai. 
Ni dhairi ya kuwa leo hii ipo hali mbaya ya udhalilishaji wa tunu za msingi kama vile:-
–       Maana isiyo ya sahihi ya kinadharia na kiutendaji kuhusu uhuru wa wote waliooana kwa kuhusiana wao kwa wao;
–       Mawazo potofu kuhusu uhusiano wa mamlaka kati ya wazazi na watoto;
–       Hali halisi ya matatizo ambayo kwayo familia hupata katika kurithisha tunu za familia
–       Kuongezeka kwa idadi ya talaka
–       Pigo la uharibifu wa mimba
–       Utumiaji wa daima wa madawa ya kuua kizazi
–          Kujitokeza dhairi mwelekeo wa fikra za uzuiaji wa mimba n.k.

Kwa hiyo maisha hayatambuliwi kama ni zawadi na baraka, bali kama ni hatari kuu ambayo inabidi kujihadhari nayo.
Hali hii ndiyo imetufanya sisi Maaskofu wa Tanzania kuwaletea tafakari juu ya familia ili Kanisa liweze kupambana na hali ya upotoshaji wa matumizi ya uhuru binafsi juu ya ndoa na familia. Mwanadamu aliye nje ya mpango wa Mungu juu ya ndoa na familia amesababisha uvunjivu wa mahusiano kati ya mtu na Mungu na hata kati ya mtu na mtu kadri ya msemo wa Mt. Augustino, mgongano wa hali ya mapendo ya kumpenda Mungu kiasi cha kudharau nafsi na kupenda nafsi kiasi cha kumdharau Mungu (St. Augustine, De Civitate Dei, XIV, 28: CSEL, 40: II56-57).
Licha ya mchango chanya wa utandawazi na mwingiliano wa tamanduni mbalimbali mwanafamilia aliyelelewa na kujilea kwa kuheshimu mpango wa Mungu amejikuta katika giza pale anapojikuta katika utamaduni ambapo mtu anajipangia kila kitu juu ya ndoa na familia bila kumhusisha muumba wake. Tuliwaona wana waisraeli na hata desturi za jamii mbalimbali siku za nyuma walivyompa Mungu nafasi ya pekee katika kufanya maamuzi yao juu ya ndoa na familia.
Hali ya kumweka Mungu pembeni katika masuala yahusuyo ndoa na familia inasababisha upotoshaji mkubwa juu ya maana ya ndoa na familia. Kupotosha huku kumepelekea kuwa na baadhi ya watu kushindwa kujenga mshikamano na Kristu aliye mkombozi pekee wa mwanadamu. Watu wanaopotosha mpango wa Mungu juu ya ndoa na familia wanaweka mazingira magumu kwa kazi ya Yesu Kristo na hata kusababisha utawala wa Yesu Mfufuka usiwe bayana kwenye jamii. Yesu amekuja kuunda jamii inayotokana na familia zinazoongozwa na Neno la Mungu ambalo ni chakula kiletacho uzima wa milele kwa wanafamilia.
Ili kurejesha uelewa sahihi na maisha sahihi ya wanandoa na wanafamilia watu wote tunaalikwa na Huruma na Upendo wa Mungu unaotualika kuongoka. Na hapa kitakachotupatia mwanga katika safari ya kuuelekea wongofu, ni Maandiko Matakatifu, yaani Biblia Takatifu pamoja na nyaraka mbali mbali za Mababa Watakatifu.


SURA YA PILI

2.0 FAMILIA KATIKA BIBLIA KWA UJUMLA

Kwa kuwa chimbuko la Imani Katoliki ni Kristu Mfufuka, ambaye anaendelea kuilea jamii ya kibinadamu kama Mkombozi pekee wa binadamu wote hatuna budi kuyatumia Maandiko Matakatifu katika kuielewa familia. Yesu huyu aliyezaliwa Nazareti katika jamii na familia ya Kiyahudi anaendelea kuongea na binadamu kupitia maisha katika yeye, na kupitia Maandiko Matakatifu, tunayoyapata kwenye Biblia Takatifu.

Turejee baadhi ya sehemu za Maandiko Matakatifu na desturi za Kiyahudi ili kujenga msingi na hoja ya kiimani kuhusu maana ya kuiona familia kuwa ni shule ya Imani na maadili.

2.1 Nafasi ya Familia katika Agano la Kale

Uelewa wote wa Kiyahudi juu ya maisha ya familia, uwe mzuri au mbaya ulitegemea sana Maandiko Matakatifu hasa kitabu cha Mwanzo 1:26-28:

Mungu akasema, ‘Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale  samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.’ Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia. Mungu akawaambia, ‘Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha, mkatawale samaki wa baharini na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi’”.

Kadiri ya Maandiko Matakatifu familia ni taasisi inayounganisha mwanaume na mwanamke, na hawa ndiyo wanaoleta mwendelezo wa uhai wa binadamu wengine na kuunda jamii ya kibindamu inayotawala dunia.

2.1 Nafasi ya Familia katika Agano la Kale

Wayahudi walifurahia na kuheshimu familia, lakini hasa familia pana ilikuwa tunu ya pekee. Kwa namna hii hakukuwa na nafasi ya walea pweke wala watu wa jinsia moja kuoana kwa maana katika hali kama hizo kusingewezekana kujenga familia yoyote.
Kupata watoto wengi tangu mapema kulikuwa jambo muhimu na la baraka. Haya ndiyo yanayofafanuliwa na Zaburi ya 127. Zaburi hii inasifia baraka ya kupata watoto wengi mtu angali kijana maana angeliweza kusaidiwa nao mapema, mathalani, kutetewa mahakamani. Mzazi aliruhusiwa kuwatumia watoto wake wa kiume kama mashahidi wa upande wake. Ndipo tunaposoma, “Watoto ni riziki kutoka kwa Mungu Mwenyezi, watoto ni tuzo lake kwetu sisi. Watoto walio na nguvu ni kama mishale mikononi mwake askari. Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi. Hatashindwa atakapokabiliana na adui mahakamani” (Zab 127:3-5). Kwa namna hii inaeleweka kwa nini kuzaliwa kwa watoto kulikuwa matukio ya furaha kubwa ndani ya familia.

2.3 Maisha ya Ndoa kadiri ya Sheria ya Kiyahudi

Awali ya yote, Wayahudi walilichukulia suala la kuoa na kuolewa kama amri ya kimungu kwa sababu ya amri iliyotolewa wakati wa uumbaji. Mwa 1:28 ilieleweka kama uanzishwaji wa taasisi ya ndoa na maisha ya familia. Hivi useja uliokuwa ukifanyika huko Qumran lilikuwa jambo la nadra sana. Ni kwa sababu hiyo, Yesu na Paulo, hapo mbele, walipoeleza kwamba mtu angeliweza kuacha kuoa au kuolewa kwa ajili ya ufalme wa Mungu, waliwashtua Wayahudi wengi (rej. Mt 19:1-12, 1Kor 7:1-16. 25-35).
Kwa kadiri ya uelewa wa Kiyahudi au wa kirabbi, maisha ya ndoa ndiyo yalikuwa hali mujarabu kwa kila mwanaume na mwanamke. Ndipo, kwa Wayahudi, mtu kuoa au kuolewa lilikuwa wajibu wa kidini. Wayahudi walifundishana kwamba maisha ya familia ndiyo yalikuwa utimilifu wa utu. Hata hivyo, aliyewajibika kuingia katika maisha ya ndoa alikuwa mwanaume siyo mwanamke. Kwa mwanamke haikuwa lazima kuolewa isipokuwa alishauriwa asiishi peke yake. Hivyo ndivyo ilivyotafsiriwa katika Kitabu cha Mwanzo  1:28. 

2.4 Jinsia ya wenye Kuoana

Je, wenye kuoana wawe watu wa jinsia zipi? Mintarafu watu wa jinsia gani, Biblia nayo haina utata, ni mume na mke yaani watu wawili wa jinsia tofauti. Hao ndiyo watu wanaoweza kuzaana na kutimiza agizo la kuijaza dunia (Mwa 1:28). Matakwa ya Mungu ni watu wawili wa jinsia mbili tofauti. Tena, watu wawili wakitofautiana jinsia ndipo tunapoweza kusema mmoja anaoa na mwingine anaolewa. 
Wanaume wawili hatuwezi kusema mmoja anaoa na mwingine anaolewa mpaka mmoja ahesabiwe kuwa mume na mwingine ageuzwe kuwa mke, jambo linalogeuza maumbile aliyowatakia Mungu. Watu wa jinsia mmoja ni kama chanya na chanya au hasi na hasi, hawawezi kutimilizana. Mwanamume na mwanamume hawawezi kuwa mwili mmoja wala wanawake wawili hawawezi kuwa mwili mmoja.
Marufuku ya Biblia ambayo hatuna mamlaka ya kuibadili imeandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Walawi 18:22-24 hivi, “Kamwe usilale na mwanamume mwenzio kama kwamba ni mwanamke. Hilo ni chukizo. Kamwe usilale na mnyama ili usijitie unajisi, mwanamume au mwanamke yeyote kamwe asifanye hivyo, kufanya hivyo ni upotovu.  Msijitie najisi kwa kufanya mambo hayo kwani kwa sababu ya mambo hayo nayafukuza mataifa  yaliyo mbele yenu kwa vile  hufanya hayo na kujitia najisi. Nchi yao ilitiwa najisi nami nikaiadhibu nayo ikawakataa wakazi wake.”

Hii ndiyo kawaida ya neno la Mungu kwenda kimuhtasari.Kumbe, haikuwa lazima kuorodhesha hapa kila aina ya dhambi.Maovu ya aina hii tunayosema yote yanamedokezwa na kumaanishwa hapa.
Lakini, kwa kuwa neno la Mungu linapokezana mafundisho, maovu ya sampuli hii, yaani dhambi hizi, zimedokezwa na kukemewa kwa msimamo usioyumba siyo tu katika Agano la Kale bali hata kwenye Agano Jipya.
Tunasoma, “Kwa sababu walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakjinena kuwa wenye hekima walipumbazika,wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege na ya wanyama na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo, Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.
“Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakibadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili, wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa…. Wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu ya kwamba wayatendao hayo wastahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana na wayatendao” (Rum 1:21-28,32).

2.5 Nyumba ya Familia
Maisha ya familia yaliwekewa makazi. Heshima ya familia ilikuwa pia kuwa na nyumba, yaani makao. Basi, mintarafu mahali familia zilipoishi, zamani hizo, familia nyingi za Kiyahudi ziliishi kwenye nyumba ndogo ambazo kimsingi zilikuwa chumba kimoja tena kisichokuwa na dirisha (rej. Lk 15:8). Nyumba ilikuwa haifungwi; stoo peke yake ndiyo iliyokuwa ikifungwa (rej. Mt 6:6). Usiku familia nzima ililala pamoja na kujifunika shuka moja (rej. Lk 11:7). Kwa kuonesha uhai wa familia, taa za majumbani mwa Wayahudi zilikuwa hazizimwi siku zote. Kuzimika kwa taa hizo kulimaanisha kifo cha familia. Ilikuwa wajibu wa mama kutafuta mafuta taa ya familia isizimike. (Mit 31:18).


2.6 Malezi ya watoto katika imani na maadili kwa Wayahudi

Katika sehemu tuongelee kwa karibu zaidi jinsi Biblia inazungumzia makuzi ya watoto wa Kiyahudi, malezi yao na kufundishwa kwao hata kuwa watu wa imani na maadili stahiki. Tuanzie mwanzoni kabisa, yaani tuanzie tangu kuzaliwa kwa watoto.

2.6.1 Masuala ya Kuzaliwa Mtoto

Mojawapo ya furaha za familia ya Kiyahudi ilikuwa ni kupata uzao. Ndipo familia za Kiyahudi zilifurahia sana ujauzito wa mama kwa sababu zilitambua kwamba ujauzito ulikuwa ndiyo ishara ya Mungu kuwabariki na kuwajalia kushiriki kazi ya uumbaji kwa ajili ya kuijaza dunia (rej. Mwa 1:27-28). Lakini kwa kutokana na ufinyu wa elimu ya viumbe (biolojia), walikuwa na miiko mingi waliyodhani inalinda ujauzito.

2.6.2 Siku ya Kuzaliwa Mtoto

Siku ya kuzaliwa mtoto ilikuwa na mambo yake pia. Katika siku yenyewe ya kuzaliwa mtoto, wakunga na tabibu walihitajika kumsaidia mwanamke anayezaa katika utungu wake. Wahudumu hao walisamehewa mambo mengi hata shughuli za Sabato. Yaani waliruhusiwa hata kuivunja Sabato.

2.6.3 Malezi ya Watoto

Kimsingi, malezi ya mtoto wa Kiyahudi yalikuwa ya kidini. Kupanga uzazi kuliendana na kipindi cha kunyonyesha. Wayahudi walihimizana kuwanyonyesha watoto wao kwa miaka miwili au mitatu na walipaswa kulelewa kidini kabisa.

Watoto walipoanza kusema tu, walifundishwa kutamka mambo matakatifu na majina mbadala ya Mungu, ndiyo Adonai, Maqom, Shem na Shamaim. Mintarafu sala, “Shema” (Kum 6:4-9) ilikuwa ndiyo sala ya msingi. Watoto walipofikisha miaka mitano walifundishwa kusoma Maandiko Matakatifu.

Watoto wa kiume, tofauti na watoto wa kike, walipaswa kuhudhuria masomo ya chekechea kwenye sinagogi ya karibu. Watoto wa kiume walipofikisha umri wa miaka 12 walipaswa kushika sheria ya Musa. Walipofikisha umri huo, walifanyiwa ibada maalumu (Bar Mitzvah) na tangu wakati huo waliruhusiwa rasmi kusoma masomo ya kiliturujia kwenye sinagogi. Shuleni kwao wanafunzi wote walitakiwa kujifunza masimulizi ya tukio la Kutoka Misri.

Injili ya Luka 2:41-45 inasimulia jinsi Maria na Yosefu walivyomlea Yesu Kristo kidini. Walimlea kwa kadiri ya sheria ya Kiyahudi. Utamaduni wa kitalmudi ulielekeza kwamba watoto hata wadogo sana walitakiwa kufika hekaluni wakati wa sikukuu. Ndiyo kisa Yesu hakuachwa pembeni. Kwa kawaida, wavulana walifikia balehe walipofikisha umri wa miaka 12 na ni kuanzia wakati huo walipoanza kuwa huru kwa kiasi fulani. Jambo hili ndilo linaloeleza, siku ile ya kupotea Yesu, kwa nini wazazi wake mwanzoni hawakuwa na wasiwasi sana na mahali alipokuwapo kwa vile “walidhani kuwa yumo katika msafara”. Wazazi hao walianza tu kuhangaika mwishoni mwa safari ya siku moja.   

2.6.4 Malezi Endelevu ya Watoto
Wazazi waliwaanzishia watoto wao, hasa wa kiume, malezi ya imani na maadili au dini kwa ujumla. Baada ya kufundishwa dini nyumbani na kuzoeshwa sala na kuingizwa katika desturi ya kushika sheria ya Musa, watoto wa kiume walipenda wenyewe kujifunza dini kwa kina kutoka kwa marabbi maarufu. Ndipo watoto walipojichagulia wenyewe walimu na kujipatia elimu kutoka kwao. Kujipatia elimu huku kuliitwa “kukaa chini ya miguu ya mwalimu” au “kumfuata mwalimu.”
Shuleni, ndiyo katika kumfuata mwalimu, Myahudi alijifunza sheria ya Musa, historia ya kutoka Misri, namna ya kufafanua Torati, mambo ya imani kwa ujumla na maadili. Kwa kufundishwa maadili, Wayahudi walitumia vitabu vya hekima, hususan, kitabu cha Yoshua ben Sira, kama vitabu vya kiada.
Ndani ya vitabu vya hekima Wayahudi walifundishwa mambo mbalimbali, mathalani, mambo ya kuwaheshimu watu, kulea watoto, kazi, urafiki, afya, furaha, nidhamu katika kunywa divai, ukweli wa mateso, ukweli wa kifo, ujasiri na sifa za watu wa zamani, utawala, umuhimu wa hekima na kadhalika. Mambo hayo yalifundishwa kwa mitindo ya kukaa pamoja kwa amani, kuulizana maswali, kujadiliana na kupeana mifano.
Mtu alikaa chini ya miguu ya mwalimu au alimfuata mwalimu kwa takribani miaka 38 ndipo alipofuzu na mtu akawa Farisayo au Mwandishi wa sheria. Aliyefuzu kama Farisayo aliweza kuwa mwalimu na yeye kufuatwa na wanafunzi wa kwake. Aliyefuzu kama Mwandishi wa sheria aliweza kuwa mnakili vitabu vitakatifu na kufanya kazi za uwakili au uhakimu.
Hata hivyo, matokeo ya jumla ya kujiendeleza katika dini yalikuwa kila baba kuweza kumudu vyema shughuli ya kuisimamia familia yake katika kuikuza, kuilea na kuidumisha katika mambo ya dini kama tulivyoona wajibu za baba.
2.6.5 Ukomo wa Watoto Kuwatunza Wazazi Wao
Watoto walipaswa kuwatunza wazazi wao maisha yao yote, yaani mpaka kufa kwao (rej. Mit 23:22 na YbS. 3:1-16). Kutokuwa na mwisho kwa wajibu huo wa kuwatunza wazazi ndiko kulikowafanya watoto jeuri au wakorofi kutumia vibaya kanuni ya “korbani”, yaani kuweka wakfu mali zao ili kukwepa kuzitumia katika kuwatunza wazazi wao (rej, Mk 7:9-13). Kanuni hiyo ilisema mtu akiweka mali yake wakfu, yaani kumwekea Mungu, alikuwa haruhusiwi kuitumia kuwasaidia wala kuwatunzia wazazi wake.  Kwa namna hii kanuni hii ilitumika vibaya na Yesu alifuta tabia hii (rej. Mk 7:8-13).
Kutokana na ukweli wa wajibu wa watoto kuwatunza wazazi wao mpaka kufa kwao, tunapata ushahidi kwamba Yesu alikuwa mtoto wa pekee kwa Bikira Maria na Yosefu, maana kama angelikuwa na kaka na dada zake wa damu, Yesu asingelimkabidhi mama yake kwa mwanafunzi aliyempenda. Kama wangelikuwapo ndugu zake wa damu, Yesu angelipata urahisi mkubwa wa kuwakumbusha wajibu wao wa kumtunza mama yao mpaka kufa kwake. Tena mahangaiko hayo hayo ya Yesu, ya kumkabidhi mama yake kwa mwanafunzi aliyempenda, yanatudokezea kwamba wakati Yesu anakufa, Yosefu alikuwa ameshakufa, vinginevyo asingelithubutu kumtenganisha mama yake na baba yake huyo (rej. Yn 19:25-28).

2.6.6 Uonevu kwa Akinamama
Maisha ya ndoa ya Kiyahudi yalihusisha mambo mawili magumu, talaka na kurithi wajane. Kati ya Wayahudi kulikuwa na uonevu mkubwa uliojengwa juu ya maisha ya ndoa. Wayahudi walipojaribu kufafanua Kumbukumbu la Torati 24:1-4 iliyotoa ruhusa mume kumwandikia talaka mkewe na kumfukuza toka nyumbani mwake, yaani kumwacha, marabbi wawili wakubwa waliwagawanyisha watu. Suala lenyewe lilikuwa juu ya maana ya “neno ovu” (erwat dabar) ambalo lilimruhusu mume kumwacha mkewe kwa sababu yake.  Rabbi Hillel aliwafundisha Wayahudi kwamba waliruhusiwa kuwaacha wake zao kwa sababu yoyote (erwat dabar) walioiona wenyewe kuwa nzito. Rabbi Shamai hakuleta nafuu yoyote maana naye aliruhusu talaka ingawa yeye alisisitiza kuwepo sababu nzito inayohusiana na kuonekana kwa uchi wa mke, kama vile, ugoni au kuvaa ovyo mbele ya watu.

Kuhusu hili,hata  Yesu mwenyewe alipinga sana desturi ya talaka kama tunavyosoma katika Maandiko Matakatifu; “ Wafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, “Je, ni halali mume kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?” Yesu akawajibu, “Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke, na akasema: kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba na mama yake, ataungana na mke wake nao wawili watakuwa mwili mmoja?” Kwa hiyo wao si wawili tena bali mwili mmoja. Basi alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe!”  (Mt. 19:3-6).

Shauri la kurithi wajane lilikuwa la ajabu sana. Wayahudi walikuwa wanahimizana kurithi wajane kwa sababu walau tatu. Mosi, walitaka kuhakikisha mali ya ndoa iliyokoma kwa kifo cha mume haiendi mbali. Pili, walikusudia kumsitiri mjane asifikwe na taabu sana.
Tatu kwa kuwa waliamini kwamba Mungu atakuwa anawataka watu walioona ushahidi wa kumwonesha mtoto waliomzaa walitaka kutatua tatizo la kukosekana ushahidi wa aina hiyo kwa watu waliopata bahati mbaya ya kutokuwa na mtoto walipoishi pamoja. Ilikuwa kwamba kama kaka alimwacha mjane pasipo mtoto, ndugu yake au jamaa yake alipaswa kumchukua mjane na kumzalia mtoto, mtoto alihesabika kuwa mali ya marehemu (rej. Kum 25:5-10). Jambo hili liliwakandamiza akina mama kwa sababu waliweza kufedheheshwa kwa kukataliwa na shemeji au ndugu za marehemu na pengine alitakiwa kumgonja shemeji mdogo akue hadi aweze kuamua kumchukua au kutomchukua.

Kuhusu kurithi wajane, Yesu katika Luka 20:27-38 alijibu swala la jane kuwa ni mke wa nani baada ya ufufuko.

2.6.7 Majumuisho ya Maelezo ya Agano la Kale
  1. Kuthamini familia: Maisha ya familia yalithaminiwa sana na Wayahudi hivyo kuoa na kuolewa zilikuwa hali zilizotegemewa kutokea katika maisha yao.
  2. Kutayarisha uchumba mwema: Waliotarajia kuoana walijipatia kipindi cha walau mwaka mmoja kujiandaa kwa maisha ya familia.
  3. Kufunga ndoa vizuri: Maisha ya familia yalianzishwa rasmi siku ya harusi, bibi harusi alipoingizwa nyumbani mwa bwana harusi.
  4. Kukataa mahusiano ya kujamiiana kati ya ndugu: Mipaka ya kujamiiana iliainishwa katika Torati ya Musa (rej. Law 18).
  5. Kukataa mahusiano ya kujamiiana yasiyo ya kawaida: Kujamiiana kinyume na maumbile au na wanyama kulikatazwa na Torati (rej. Law 18).
  6. Kukataa ndoa za jinsia moja: Watu wa jinsia moja walikatazwa kujamiiana sembuse kuoana.
  7. Kudumu katika maagano ya ndoa: Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao, Musa aliwaruhusu Wayahudi kuachana, lakini ilikuwa kinyume na matakwa ya Mungu (Kum 24:1-4, Mt 19:1-12).
  8. Kutunza usafi na utakatifu wa ndoa: Ugoni ulipata adhabu kali. Aliyefumaniwa alipewa adhabu ya kupiga mawe hadi kufa.
  9. Kutunza mimba vyema: Mimba zilitunzwa kwa miiko kadhaa iliyopaswa kushikwa na mama mjamzito.
  10. Kuangaliwa watoto na kupewa majina mazuri: Watoto waliangaliwa sana, wakanyonyeshwa kwa kipindi cha kufaa na walipewa majina yenye maana fulani kusudi wapate kuhamasika na sifa zinazoendana nayo.
  11. Kupanga uzazi: Miaka miwili au mitatu ya kunyonyesha watoto ndiyo iliyowatumika kupanga uzazi. Idadi ya watoto haikuwa na ukomo.
  12. Kulea watoto vyema: Watoto walilelewa na wazazi wote wawili, lakini baba aliwaangalia watoto wa kiume kwa namna ya pekee na mama watoto wa kike. Mintarafu kusoma, watoto wa kiume walijichagulia wenyewe walimu wa kuwafundisha Torati kwa kina.
  13. Wanafamilia kutunzana na kushika majukumu husika: Wanafamilia waligawana majukumu. Baba alikuwa na majukumu yake  na mama sawia. Hata watoto walikuwa na yao.
  14. Kusaidiana kwa udumifu: Wazazi waliwalea watoto mpaka walipoanza maisha ya familia wenyewe. Kutoka hapo kazi iliwageukia watoto kuwatunza wazazi wao mpaka walipoaga dunia. Watoto kukwepa majukumu ya kuwatunza wazazi wao kwa kuweka mali zao wakfu (“korbani”) ilikuwa ni uhuni wa kusikitikiwa.
  15. Kutoachana ovyo: Ijapokuwa talaka iliruhusiwa, ugumu wa kulipa mahari ulipunguza talaka za ovyo ovyo. Mara nyingi ni kifo kilichomaliza maisha ya ndoa.

2.6.8 Usafi wa Ndoa na Maisha ya Familia

Ya kwamba ndoa inatakiwa kuwa na usafi wa pekee inadokezwa katika maneno ya Kristo pale alipokuwa anajibu swali aliloulizwa na Mafarisayo kama ni kweli kwamba waume wanaweza kuwapa talaka wake zao na kuwaacha kwa sababu yeyote. Yesu alifuta misimamo ya akina Hillel na Shammai akisisitiza kwamba agano la ndoa halifunguliki (Mt 19:3-6).

Kwa kusema hivyo alimaanisha vile vile kwamba ndoa ni agano la watu wawili tu, mume mmoja na mke mmoja. Kwa kusema hivyo alionesha uharamu wa mitara. Hapo hapo kwa kusema hivyo alidokeza uharamu wa mahusiano yoyote yasiyozingatia jinsia hizo tofauti za mume na mke. Na hiyo maana yake lilikuwa dokezo la uharamu wa mahusiano yote yaliyo kinyume na mume na mke, yaani mahusiano kama ya mwanaume na mwanaume, mwanamke na mwanamke au mwanadamu na hayawani. Aidha, maneno yake hayo yalifunga mwanya wa mtu kujibadili jinsia au mtu kujitengeneza ili awe na jinsia zote mbili. Haya yote yanasomeka katikati ya mistari ya Mt 19:1-12.Soma aya hizi huku ukitafakari vyema nawe utaona jinsi kina chake kilivyo kirefu.

No comments :

Post a Comment