Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya
Michezo wa Wizara ya Habari utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Yusuph Singo
(Kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari leo Machi 30, 2019 Jijini
Dodoma kuhusu kuliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kusimamia
Uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) ufanyike
ndani ya siku 30 kuanzia leo.Kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza hilo
Bw.Alex Nkenyenge.
Katibu Mtendaji wa Baraza la
Michezo la Taifa Bw.Alex Nkenyenge (Kulia) akizungumza na Waandishi wa
Habari leo Machi 30, 2019 Jijini Dodoma kuhusu kutekeleza maagizo ya
Serikali kwa Baraza hilo kusimamia Uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es
Salaam Young Africans (Yanga) ndani ya siku 30 kuanzia leo.Kushoto ni
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari utamaduni
Sanaa na Michezo Bw.Yusuph Singo.
……………………
Na Shamimu nyaki –WHUSM
Serikali imeliagiza Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) kushirikiana na Shirikisho la mpira wa
Miguu
(TFF) kuhakikisha uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es Salaam Young
Africans (Yanga) unafanyika ndani ya siku 30 kuanzia leo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Idara
ya Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo katika mkutano na Waandishi wa
Habari leo Jijini Dodoma ambapo amesema kuwa migogoro iliyokuwepo huko
nyuma imeshafika tamati hivyo uchaguzi ndani ya Klabu hiyo ni lazima
ufanyike.
“Nailekeza BMT iwaelekeze TFF
kuhakikisha taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa na uchaguzi ndani ya
Klabu ya Dar es Salaam Young Africans unafayika ndani ya siku 30 kuanzia
sasa”.amesema Bw.Singo
Aidha Bw.Singo amewahisi Viongozi,
wanachama na wapenzi wa Klabu ya Dar es Salaam Young Africans
kutoanzisha migogoro wala vikwazo vingine bali kutumia siku 30 hizo
kufanya uchaguzi ili kupata viongozi watakaoisimamia na kuiongoza Klabu
hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mpira wa miguu ndani na nje ya
nchi.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw.Alex Nkenyenge amesema amepokea
maagizo na atayafanyia kazi mara moja ili kipindi kilichowekwa na
Serikali cha siku 30 Klabu ya Yanga iwe tayari ina uongozi.
Bw.Nkenyenge ameongeza kuwa
atahakikisha Kamati ya Uchaguzi ya TFF inapanga utaratibu unaotakiwa
kufuatwa kulingana na Katiba ya Shirikisho hilo ili Uchaguzi huo
ufanyike hatimaye migogoro iliyodumu kwa muda mrefu ndani ya Klabu hiyo
ifikie mwisho na Klabu iendelee kufanya vizuri katika mpira wa miguu.
Klabu ya Dar es Salaam Young
Africans (Yanga) ni miongoni mwa Klabu kubwa za mpira wa miguu hapa
nchini ambayo kwa muda mrefu haijatekekeleza uchaguzi kwa mujibu wa
Katiba yao.
No comments :
Post a Comment