Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdory Mpango (Mb) akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa , Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2019/20, bungeni jijini Dodoma.
Baadhi ya Mawaziri na Wabunge
Wakimsikiliza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (hayupo pichani), kabla
ya kuwasilishwa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa ,
Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, bungeni
jijini Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdory Mpango (Mb) (kushoto) akizungumza jambo na Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James, katika viwanja vya Bunge Jijini
Dodoma kabla ya kuwasilishwa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa , Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2019/20.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdory Mpango (Mb) (kushoto) akisalimiana na Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako , katikati ni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, katika
viwanja vya Bunge Jijini Dodoma .
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki, akizungumza
jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, baada
ya kuwasilishwa kwa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa
Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza jambo na Mbunge wa Ludewa Mhe.
Deo Ngalawa, kabla ya kuwasilishwa kwa Mapendekezo ya Serikali ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2019/20, ambapo mikopo ya Ndani inatarajiwa kuwa Sh. bilioni
4,960.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James, akizungumza jambo na Mbunge wa Ilala, Mhe.
Mussa Azzan Zungu, kabla ya uwasilishaji wa Mapendekezo ya Serikali ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2019/20, ambapo Sh. bilioni 2,783.7 za mikopo nafuu zinatarajiwa
kutoka kwa washirika wa maendeleo.
…………………………………
MAELEZO YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA
SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA
NA YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA
SERIKALI KWA MWAKA 2019/20
UTANGULIZI
- Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha wabunge wote kukutana tena hapa Jijini Dodoma, kupokea mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, kwa mujibu wa Kanuni ya 97 fasili ya (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016. Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu umoja na amani.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki (Mb), Mheshimiwa Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb), Mheshimiwa Prof. Palamagamba Aidan Kabudi (Mb), Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb), Mheshimiwa Joseph George Kakunda (Mb) na Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mawaziri ili kuongoza wizara mbalimbali. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Mawaziri mlioteuliwa na Waheshimiwa Wabunge wote mtaendelea kunipatia ushirikiano katika kuijenga nchi yetu kwa manufaa ya Watanzania wote.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii inawasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2019/20 ambayo imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi. Sehemu ya pili ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20. Sehemu ya tatu ni tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2018/19 na mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20.
SEHEMU YA KWANZA
TATHMINI YA MWENENDO WA HALI UCHUMI
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuiandaa nchi kuelekea uchumi wa kipato cha kati, uchumi umeendelea kuimarika. Pato la Taifa kwa kutumia mwaka wa kizio 2015 linaonesha kuwa katika robo ya tatu (Julai hadi Septemba) ya mwaka 2018, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 5.0 kipindi kama hicho mwaka 2017. Shughuli za kiuchumi zilizokuwa kwa kasi kubwa ya ukuaji ni afya (asilimia 13.2), usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 12.4); Maji (asilimia 10.7); Ujenzi (asilimia 7.4); Habari na Mawasiliano (asilimia 7.3); viwanda (asilimia 7.3); na Biashara na Matengenezo (asilimia 7.3).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018, mwenendo wa mfumuko wa bei nchini uliendelea kuwa tulivu katika wigo wa tarakimu moja kutokana na kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini na nchi jirani pamoja na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti za Serikali. Mfumuko wa bei ulipungua kutoka wastani wa asilimia 4.0 Januari 2018, hadi kufikia asilimia 3.4 Juni 2018 na kuendelea kupungua zaidi hadi asilimia 3.0 Januari 2019.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka unaoishia Januari 2019 thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nchi za nje ilikuwa dola za Marekani milioni 8,300.0 na thamani ya bidhaa na huduma zilizonunuliwa kutoka nje ilikuwa dola za Marekani milioni 10,462.6. Kwa upande wa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje ilikuwa dola za Marekani milioni 2,982.2 kutokana na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa za mitaji zilizoagizwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo. Kwa matokeo hayo akiba ya fedha za kigeni ni Dola za Marekani milioni 4,884.4 Januari 2019, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takribani miezi 4.8. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi 4.5.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.6 katika mwaka 2018 ikilinganishwa na ongezeko la wastani wa asilimia 5.5 katika kipindi cha mwaka 2017. Mwenendo huo ulichangiwa na kuimarika kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kulikotokana na jitihada za Serikali kupitia Benki Kuu katika kuchochea ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Riba za dhamana za muda mfupi za Serikali zilipungua hadi wastani wa asilimia 6.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 11.1 mwaka 2017. Vile vile, riba za mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi zimeendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2017 hadi wastani wa asilimia 17.4 mwaka 2018.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kuimarika kufuatia utekelezaji wa sera ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi pamoja na jitihada zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu katika kuchochea ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka ambapo Januari 2019 ilikuwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 2.1 Januari 2018. Sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa katika shughuli binafsi (asilimia 27.9 ya mikopo yote) ikifuatiwa na shughuli za biashara zilizopata asilimia 18.4, uzalishaji viwandani (asilimia 11.6) na kilimo (asilimia 7.8).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani umeendelea kuwa tulivu ambapo katika mwaka 2018, Dola moja ya Marekani ilinunuliwa kwa wastani wa Shilingi 2,263.8. Hii ni kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha, usimamizi thabiti wa mapato na matumizi ya Serikali, matumizi ya gesi asilia na umeme wa maji badala ya mafuta katika kuzalisha umeme na baadhi ya viwanda nchini kuzalisha bidhaa ambazo awali zilikua zikiagizwa kwa wingi kutoka nje.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano, itaendelea kutekeleza sera madhubuti za fedha na bajeti ili kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unaendelea kuimarika.
SEHEMU YA PILI
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2018/19 NA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2019/20
- TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2018/19
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/19, Serikali ilitenga Shilingi bilioni 12,007.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, zikijumuisha Shilingi bilioni 9,876.4 fedha za ndani na Shilingi bilioni 2,130.9 fedha za nje. Hadi Januari 2019, jumla ya Shilingi bilioni 2,788.5 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, Shilingi bilioni 144 zilipokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na kupelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretaieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vile vile, Shilingi bilioni 3,803.4 zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Serikali imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 1,433.8 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo mradi wa kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji Mto Rufiji (MW 2,115).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo katika mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:
(i) Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge:
Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) unaendelea
vizuri kama ilivyopangwa, ambapo shughuli zinazoendelea ni ujenzi wa
madaraja, makalavati, daraja lenye urefu wa km 2.54 katikati ya jiji la
Dar es Salaam, ukataji wa miinuko, ujazaji wa mabonde na utandikaji wa
reli. Katika kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422), kazi
zinazoendelea ni pamoja na ukataji wa miinuko na ujazaji wa mabonde,
usanifu wa njia na ujenzi wa kambi za Kilosa na Ihumwa. Kwa upande wa
kipande cha Isaka – Rusumo (km 371), hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa
mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa njia ya reli.
Aidha, taratibu za ununuzi wa mabehewa, injini na mitambo itakayotumika
kutoa huduma ya usafiri kwenye reli ya Standard Gauge zipo katika hatua za mwisho.
Katika miradi inayogharamiwa na
mfuko wa reli, shughuli zilizofanyika ni: kununua vichwa 11 vya treni
kwa ajili reli ya kati; kuendelea na ukarabati wa reli ya Tanga – Arusha
(km 439) ambapo kipande cha Tanga – Mombo (km 129) kimeanza kufanya
kazi ya kusafirisha mizigo na ukarabati wa vipande vya Mombo – Same
(km124) na Same – Arusha (km 186) unaendelea. Aidha, kazi ya ukarabati
wa mabehewa inaendelea ambapo hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa
ukarabati wa mabehewa 15.
(ii) Mradi wa Kufua
Umeme wa Maji Rufiji – MW 2,115: Hatua iliyofikiwa ni: kupatikana kwa
mkandarasi wa mradi wa kufua umeme utokanao na nguvu ya maji katika Mto
Rufiji ambaye ni Kampuni ya Ubia kati ya Arab Contractors na Elsewedy Electric S.A.E
kutoka Misri ambapo mkataba wa ujenzi umesainiwa na mkandarasi
alikabidhiwa eneo la mradi mwezi Februari 2019. Mafanikio yaliyopatikana
ni pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu wezeshi ikijumuisha
njia ya umeme wa msongo wa kV 33 kutoka Msamvu hadi eneo la mradi;
mifumo ya huduma ya maji na ya mawasiliano ya simu; kukamilika kwa
ujenzi wa nyumba 10 na kuendelea na ukarabati wa nyumba 28 za iliyokuwa
kambi ya RUBADA; ujenzi wa barabara za Kibiti – Mloka – Mtemere –
Matambwe Junction – Mto Rufiji (km 210) na Ubena Zomozi – Mvuha – Kisaki – Mtemere Junction (km 178.39) zimekamilika.
(iii) Kuboresha Shirika la
Ndege Tanzania: Hatua iliyofikiwa ni: kuwasili kwa ndege nyingine tatu,
moja ikiwa ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na mbili zikiwa ni Airbus
A220-300, na hivyo kufanya idadi ya ndege zilizonunuliwa kuwa sita;
kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege moja aina ya Boeing 787-8
Dreamliner na Bombadier Q400 zinazotarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa
mwaka 2019. Kufuatia hatua hiyo, ATCL itaanzisha safari za ndege kwenda
nchini China na India ambazo kimkakati ndizo masoko mapya ya utalii.
(iv) Miradi ya Umeme: Hatua
iliyofikiwa ni: kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa
km 250 ya msongo wa kV 220 Makambako – Songea pamoja na vituo vitatu
vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea, hivyo kuwezesha mikoa
ya Njombe na Ruvuma kuunganishwa katika Gridi ya Taifa; kuendelea na
mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 wa Singida – Arusha –
Namanga wenye urefu wa km 414; kuendelea na miradi ya kusafirisha umeme
ya Geita – Nyakanazi (kV 220), Rusumo – Nyakanazi (kV 220) na Bulyankulu
– Geita (kV 220); kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Kusambaza Umeme
Vijijini na Makao Makuu ya Wilaya ambapo vijiji 1,782 na wateja 96,832
wameunganishiwa umeme hivyo kufikia jumla ya vijiji 1,039
vilivyounganishwa na umeme; kukamilisha utengenezaji wa mitambo minne ya
kufua umeme na kupelekwa mitambo miwili ya kufua umeme katika eneo la
mradi wa Kinyerezi I Extension – MW 185; Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo
MW 80: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa barabara za
kuingia eneo la mradi; kukamilika kwa ujenzi wa kikinga maji; kuanza
kazi ya kuchimba handaki la kupitisha maji; kuendelea na uchimbaji wa
eneo itakapofungwa mitambo; na kukamilika kwa ujenzi wa nyumba mbili
kati ya tano za wafanyakazi.
(v) Huduma za Maji
Mijini na Vijijini: miradi 65 imekamilika na kufanya jumla ya miradi
yote iliyokamilika kufikia 1,659 na vituo vya kuchotea maji kuongezeka
hadi 131,370 na kuhudumia wananchi 25,359,290. Upatikanaji wa huduma za
maji Jijini Dar es Salaam umefikia asilimia 85, katika mikoa mingine
asilimia 80, miji midogo asilimia 64 na vijijini asilimia 64.8. Aidha,
utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mengine unaendelea katika
hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa maji wa Ziwa Victoria –
Igunga – Nzega na Tabora, mradi wa maji katika jiji la Arusha na Same –
Mwanga – Korogwe. Vile vile, utekelezaji wa mradi wa maji katika miji 28
wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 465 upo katika hatua za
kumpata Mtaalamu Mwelekezi na Mkandarasi wa mradi.
(vi) Miradi ya Afya:
Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza upatikanaji
wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa asilimia 96.
Hatua nyingine zilizofikiwa ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa jengo
la vifaa vya uchunguzi (X–Ray Building) na kununua vifaa vya tiba ya
mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya; na kuongeza utoaji wa chanjo
kufikia asilimia 97. Aidha, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya
afya katika ngazi zote ikijumuisha ujenzi na ukarabati wa hospitali za
rufaa za mikoa, kanda na kitaifa; ujenzi wa hospitali za halmashauri 67;
ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya 352; kuajiriwa kwa watumishi
wa sekta ya afya 7,680; ujenzi wa nyumba 310 za watumishi wa afya;
ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa Hospitali za Rufaa za Mikoa,
Hospitali za halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati. Serikali
imeendelea kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuboresha
miundombinu ya kutolea huduma, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na hivyo
kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi katika hospitali za Muhimbili,
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean
Road (ORCI), Taasisi ya Mifupa (MOI), hospitali ya Benjamin Mkapa na
Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi – Mloganzila.
(vii) Miradi ya Elimu:
Serikali imeendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo kila mwezi
kiasi cha shilingi bilioni 24.4 kinatumika. Hatua nyingine zilizofikiwa
ni: ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia
ikijumuisha madarasa 870, matundu ya vyoo 1,958, mabweni 210, mabwalo
79; ukarabati wa shule kongwe; ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika
vyuo vya ualimu Ndala, Shinyanga, Patandi, Mpuguso na Murutunguru;
kukamilisha maboma ya madarasa, mabweni na nyumba za walimu 39;
ukarabati wa vyuo vya kati 20 kati ya 54 vya Maendeleo ya Wananchi
(FDCs), nyumba za walimu 39; kukamilika na kuzinduliwa kwa Maktaba ya
Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; ujenzi wa mabweni katika Chuo Kikuu
cha Mzumbe yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000; ujenzi na ukarabati
wa miundombinu katika vyuo vikuu vya Sokoine na Dar es Saaalm; na
mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu 119,214; uimarishaji wa vyuo 10
vipya vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana; na ujenzi wa shule kwa ajili
ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika chuo cha Ualimu Patandi.
(viii) Kilimo: Utoshelevu
wa Chakula kwa mwaka 2018/19 umefikia asilimia 124. Aidha, Serikali
imeanza utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya
pili (ASDP II) na mkazo umewekwa katika kuendeleza mazao ya kimkakati
yakiwemo Kahawa, Pamba, Chai, Korosho, Tumbaku, Alizeti, Michikichi,
Mpunga na Mahindi. Ili kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo, Serikali
inaendelea kuimarisha shughuli za ushirika, ujenzi wa maghala na vihenge
vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 250,000 katika kanda saba,
kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta hususan alizeti na michikichi,
kuimarisha shughuli za utafiti wa mazao, kuongeza thamani ya mazao ya
kilimo kwa kufufua vinu vya kusindika mazao ya nafaka na mafuta,
kudhibiti visumbufu vya mazao, kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa
pembejeo za kilimo na kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao. Vile vile,
Serikali imeanza kuboresha mifumo ya takwimu za kilimo kwa kuanza
usajili wa Wakulima.
(ix) Mifugo: Hatua
iliyofikiwa ni kuendelea kuimarisha vituo 3 vya kuzalisha vifaranga vya
samaki vya Kingolwira (Morogoro), Mwampuli (Igunga) na Ruhila (Songea)
kwa kuzalisha na kusambaza vifaranga vya samaki kwa wafugaji wa samaki
wakiwemo vijana. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta Binafsi
imeweza kuzalisha jumla ya vifaranga 17,301,076 kama ifuatavyo:
kambamiti 11,080,000, sato 5,072,800 na kambale 1,148,276. Vile vile,
jumla ya wananchi 6,995 wamepatiwa elimu ya ugani katika ukuzaji wa
viumbe maji.
(x) Mradi wa Bomba la
Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania):
Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa tathmini ya athari za mazingira na
jamii kwa upande wa Tanzania; kukamilika kwa tafiti za kijiolojia katika
eneo la Chongoleani; kukamilika kwa tathmini za Kijiolojia na
Kijiofizikia katika eneo la mkuza wa bomba; na kutwaa ardhi eneo la
Bandari – Tanga (Chongoleani) kutakapojengwa miundombinu ya kuhifadhi
mafuta.
(xi) Miradi ya Viwanda:
Kiwanda cha Kuunganisha Matrekta (TAMCO, Kibaha): Hatua iliyofikiwa ni:
kuingiza matrekta 822 aina ya URSUS (semi knocked down) ambapo matrekta
571 yameunganishwa na matrekta 339 yameuzwa; Kituo cha Zana za Kilimo na
Ufundi Vijijini – CAMARTEC: kutengeneza zana zikijumuisha mashine 64 za
kupandia mbegu za pamba, kusaga karanga, kukausha mbogamboga na kukata
majani pamoja na ujenzi wa mitambo 55 ya biogas; SIDO:
kuendelea na ujenzi wa majengo ya viwanda 11 katika Mikoa ya Dodoma,
Geita, Kagera, Katavi, Manyara, Mtwara na Simiyu na ujenzi wa ofisi za
SIDO katika mikoa mipya ya Geita na Katavi.
(xii) Miundombinu ya Biashara
ya Madini: Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya
kuboresha mazingira ya biashara kwenye sekta ya madini ikihusisha: vituo
vya umahiri katika mikoa saba, vituo vitatu vya mfano, jengo la taaluma
la madini katika chuo cha madini, One Stop centre Mirerani, Brokers house
Mirerani, uanzishwaji wa masoko ya madini mikoani, na uwekaji wa mfumo
wa ulinzi wa kidigitali Mirerani, ununuzi wa mtambo wa uchorongaji
miamba kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo kupitia STAMICO.
(xiii) Ardhi na Makazi:
Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na: kuandaliwa na kusajiliwa kwa Hati
Milki 110,000 na Hati za Kimila 133,000; kuandaliwa kwa mipango ya
matumizi ya ardhi ya vijiji 263 katika Wilaya 45; kuandaliwa kwa Mipango
Kabambe ya miji mikuu ya mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Mara,
Singida, Iringa na Pwani, Ruvuma, Tabora na Simiyu; kuendelea na hatua
za maandalizi ya Mipango Kabambe ya miji mikuu ya mikoa ya Dar es
Salaam, Morogoro, Rukwa, Shinyanga, Manyara, Dodoma, Tanga, Mbeya,
Kagera, Kigoma, Katavi, Lindi, Kilimanjaro, Njombe na Geita; kuanzishwa
kwa Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi; na kuongezeka kwa idadi ya
benki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba kufikia 31 na
kuwanufaisha wananchi 4,174. Aidha, Mfuko wa Mikopo Midogo Midogo ya
Nyumba ulio chini ya Benki Kuu umeongezewa mtaji wa dola za Marekani
milioni 18 ambapo taasisi za fedha tano (5) zimepatiwa mtaji wa shilingi
bilioni 13.87 kwa ajili ya kukopesha wananchi wa kipato cha chini kwa
masharti nafuu.
(xiv) Ujenzi wa Barabara
Dar es Salaam: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa barabara
ya juu katika makutano ya TAZARA (Mfugale flyover); kuendelea na ujenzi
wa barabara za muingiliano Ubungo; mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es
Salaam km 210 za barabara kwa kiwango cha lami; na kuendelea na ujenzi
wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (km 19) kwa njia nane.
(xv) Ujenzi wa Meli:
Hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na Ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa
kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika ziwa Victoria; kufikia
asilimia 82 ya ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200
na mizigo tani 200 za mizigo katika ziwa Nyasa; na kukamilika kwa
ujenzi wa matishari mawili katika Ziwa Nyasa. Kwa upande wa Ziwa
Tanganyika, Ujenzi wa Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani
400 za mizigo, ambapo uandaaji wa mikataba kwa ajili ya ujenzi wa meli
hiyo pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba umekamilika. Miradi
mingine ni kukamilika kwa ujenzi wa kivuko kipya cha Kigongo – Busisi;
kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha MV Pangani II; kuendelea
kukarabati vivuko vya MV Sengerema, MV Kigamboni na MV Misungwi.
(xvi) Viwanja vya Ndege:
Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa asilimia 90.7 ya ujenzi wa jengo
jipya la abiria (Terminal III) katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere; kuendelea na upanuzi wa maegesho ya ndege, ujenzi wa
jengo la mizigo, uzio wa kiwanja, maegesho ya ndege za mizigo na jengo
la kuongozea ndege katika kiwanja cha ndege cha Mwanza. Aidha, ujenzi na
ukarabati wa viwanja vya ndege vya mikoa vikiwemo vya Sumbawanga,
Kigoma, Shinyanga, Mtwara, Songea, Mara, Songwe, Mbeya, Mwanza, Kigoma,
Tabora na Iringa unaendelea.
(xvii) Mawasiliano: Hatua
iliyofikiwa ni: kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
ambapo vituo vitatu (3) vya Mkongo katika maeneo ya Tukuyu, Kibaha na
Kahama vimejengwa na kuvipa nguvu vituo vitatu (3) vya mkongo (Optical
Line Amplifier (OLA) katika maeneo ya Ifakara, Kidatu na Mafinga; na
kuendelea kutekeleza mradi wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi
umetekelezwa kwa kubandika vibao vya namba za nyumba katika Halmashauri
12. Vile vile, Mfumo wa Usimamizi na Ufuatiliaji wa Mawasiliano ya Simu
(TTMS) umekabidhiwa rasmi kutoka kwa Mkandarasi SGS/GVG ambapo katika
kipindi cha Julai, 2018 hadi Februari, 2019 jumla ya miamala
2,004,196,139 imepita katika mitandao ya simu na wastani wa fedha
zilizopita ni Shilingi bilioni 12,202.7.
(xviii) Uendelezaji wa
Bandari: Bandari ya Dar es Salaam: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa
ujenzi na kuanza kutumika kwa gati Na.1; na kuendelea na ujenzi wa
sakafu ngumu katika gati la kupakua na kupakia magari; Bandari ya Tanga:
ukarabati wa miundombinu ya barabara kuelekea lango Na. 2 umekamilika;
Bandari ya Mtwara: ujenzi wa gati la mita 300 la kuhudumia shehena
mchanganyiko unaendelea. Aidha, ujenzi wa Bandari katika Maziwa Makuu
(Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa) unaendelea.
(xix) Ujenzi wa Barabara
na Madaraja Makubwa: kazi zilizofanyika ni kujengwa kilomita 140.42 za
barabara kuu na kilomita 12.43 za barabara za mikoa kwa kiwango cha
lami. Aidha, kwa upande wa madaraja hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa
ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa (Dar es Salaam); kuendelea na ujenzi wa
madaraja ya Momba (Rukwa) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 94,
Sibiti (Singida) asilimia 88.35, Mara (Mara) asilimia 85; na Ruhuhu
(Ruvuma) asilimia 76; na kuanza ujenzi wa Daraja Jipya la Selander na
barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2.
(xx) Ufungaji wa rada nne
za kuongozea ndege za kiraia JNIA, KIA, Mwanza na Songwe: Hatua
iliyofikiwa ni: JNIA: Kukamilika kwa asilimia 95 ya miundombinu ya rada.
Mwanza: Ujenzi wa miundombinu ya rada unaendelea vizuri. KIA: Ujenzi
wa miundombinu ya rada unaendelea na umefikia asilimia 90. Songwe:
taratibu za ujenzi wa miundombinu zinaendelea. Aidha, mitambo itafungwa
miundombinu itakapokamilika.
(xxi) Miradi ya Mahakama:
Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama za Wilaya za
Bukombe, Chato, Ruangwa, Geita na Kilwa; kukamilika kwa ujenzi wa
Mahakama za Mwanzo za Magoma (Korogwe) na Mlowo (Mbozi); kuendelea na
ujenzi wa Mahakama za mikoa ya Njombe, Katavi, Lindi na Simiyu;
kuendelea na ujenzi wa Mahakama za Wilaya za Kasulu, Sikonge, Kilindi,
Bunda, Longido, Kondoa, Njombe, Rungwe, Chunya, Wanging’ombe, na Makete;
kuendelea na ujenzi wa Mahakama Kuu Kigoma na Mara ambao umefikia
asilimia 80; ujenzi wa Mahakama za Mwanzo za Mkunya (Newala), Uyole
(Mbeya), Ngerengere, Mlimba na Mang’ula (Morogoro); ukarabati mkubwa wa
nyumba tatu za kufikia Majaji Mtwara; na kukamilika kwa uboreshaji wa
mfumo wa ukusanyaji takwimu na kusajili mashauri, kuingiza taarifa
muhimu za wadaawa ikiwa ni pamoja na kutuma taarifa kwa ujumbe mfupi
(sms) kwa wadaawa kuhusu mwenendo wa mashauri. Aidha, imeanzishwa huduma
ya mahakama zinazotembea (mobile court, kwa kuanzia na mikoa ya Dar es
salaam na Mwanza, magari ambayo yamezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwezi Februari
2019.
(xxii) Miradi ya Kimkakati
ya kuongeza mapato katika Halmashauri: Hatua iliyofikiwa ni utekelezaji
wa miradi ya kimkakati 37 ya kuongeza mapato ya halmashauri na kupunguza
utegemezi wa kibajeti kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali ikijumuisha Soko la
kisasa – manispaa ya Morogoro, soko la kisasa – halmashauri ya mji
Kibaha, Pwani, ghala la kisasa – halmshauri ya wilaya ya Ruangwa, kituo
cha mabasi Mbezi Louis – Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, soko la
Mburahati – manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, ujenzi na upanuzi wa
kiwanda cha kutengeneza chaki na kiwanda cha vifungashio – halmashauri
ya wilaya ya Maswa, Simiyu, stendi ya mabasi Korogwe. Miradi hii
inatekelezwa katika halmashauri 29 na ipo katika hatua mbalimbali.
(xxiii) Uwekezaji: Sekta ya
Uwekezaji imeendelea kukua ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika
Mashariki ambapo ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha
Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji kati ya nchi za Afrika
Mashariki. Kwa mfano, Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia ya mwaka 2018
inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo
(UNCTAD) inaonesha kuwa Tanzania imevutia uwekezaji wenye thamani ya
Dola za Kimarekani milioni 1,180, ikifuatiwa na Uganda Dola za
Kimarekani milioni 700 na Kenya Dola za Kimarekani milioni 672. Aidha,
ripoti ya “Where to Invest in Africa” ya mwaka 2018 inayojulikana kama RMB’s Investment Attractiveness Index
inayoonesha nchi zinazovutia zaidi kwa uwekezaji barani Afrika,
Tanzania imeendelea kuwa katika kumi bora kwa kushika nafasi ya saba (7)
kati ya nchi 52 ikipanda kutoka nafasi ya 9 mwaka 2017.
Aidha, jitihada za Serikali
kuhamasisha ujenzi wa viwanda nchini zimewezesha kuongezeka mitaji
katika viwanda mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mtaji uliowekezwa chini ya
Mamlaka ya EPZ umeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.422 mwaka
2016 hadi Dola za Marekani bilioni 2.23 hapo Novemba, 2018, ikiwa ni
ongezeko la Dola za Marekani milioni 808 (sawa na ongezeko la asilimia
56.8). Mwenendo wa mauzo ya bidhaa za viwanda hivyo nje ya nchi yamekuwa
yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.194
hapo Novemba 2018, kutoka Dola za Marekani bilioni 1.1 mwaka 2016,
ikiwa ni ongezeko la asilimia 99.45. Mtaji mkubwa umewekezwa katika
viwanda vya kuongeza thamani mazao (agro processing) ambapo ina asilimia
38 ya mtaji wote; zikifuatiwa na viwanda vya kuunganisha mitambo
(assembling & engineering) asilimia 31 ya mtaji, mavazi na nguo
asilimia 21 ya mtaji na uchakataji madini asilimia 10 ya mtaji. Aidha,
viwanda 71 ni vya makampuni ya kigeni, viwanda 58 ni vya makampuni ya
ubia na viwanda 45 ni vya makampuni ya ndani.
(xxiv) Kuhamishia Utekelezaji
wa Majukumu ya Serikali Makao Makuu Dodoma: Serikali imetekeleza azma
yake ya kuhamia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma ambapo mpaka hivi sasa
Wizara zote zimeshahamia Dodoma na jumla ya Watumishi 8,883 wanatekeleza
majukumu yao wakiwa hapa Dodoma (Watumishi hao ni kutoka Ofisi/Wizara
na Vyombo vya Ulinzi na Usalama). Vile vile, Mheshimiwa Makamu wa Rais,
Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri pia wameshamia Dodoma.
Uendelezaji wa eneo la Mji wa Serikali – Ihumwa umeanza na jumla ya
majengo 22 ya Ofisi za Wizara na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yako
katika hatua za mwisho za ujenzi.
(xxv) Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana: Serikali imeendelea kuwawezesha Vijana kiuchumi ili waweze
kujiajiri katika nyanja za uzalishaji mali na kutoa huduma ambapo hatua
iliyofikiwa ni: kutolewa kwa mikopo nafuu yenye thamani ya Shilingi
bilioni 2.74 kwa vikundi vya vijana 523, vyenye wanachama 3,661 katika
Halmashauri 128 za Tanzania Bara; na kuanzishwa kwa SACCOS 127 za Vijana
kati ya 184 zinazotarajiwa kuanzishwa hadi kufikia mwaka 2020.
(xxvi) Mafanikio mengine ni
kuendelea kuimarika kwa Amani, utulivu na usalama nchini hivyo,
kuwezesha kukua kwa shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kutimiza
jukumu hilo, Jeshi la Polisi limeendelea kuweka juhudi katika kudhibiti
uhalifu sanjari na kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia
mbalimbali ili jamii ibadilike na kuachana na matukio ya uhalifu.
(xxvii) Mazingira:
Serikali imetekeleza hughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha
mfumo wa ikolojia ili kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, kujenga uwezo w
taasisi na jamii kuhimili changamoto za mazingira na athari za
mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha kanuni za kutoa leseni za tathmini
ya mazingira kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni za muda kabla ya
kuanza mradi.
(xxviii) Miradi
ya Sekta Binafsi: Sekta hii imeendelea kushiriki katika ujenzi wa
viwanda ambapo katika kipindi cha 2015 hadi 2018, jumla ya viwanda 3,530
vilijengwa na kuanza uzalishaji.
- MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2019/20
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20 ni wa nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21, wenye dhima ya Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu. Maandalizi ya Mpango huu yamezingatia azma ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; na Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambavyo ni:
(i) Viwanda vya
kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda: Miradi
itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kujenga viwanda
vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususan kilimo, madini na
gesi asilia. Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata
Gesi Asilia, Uanzishwaji na Uendelezaji wa Kanda Maalamu za Kiuchumi na
Kongane za Viwanda, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo
na uvuvi, kuongeza thamani ya madini na usimamizi endelevu wa
rasilimali za misitu;
(ii) Kufungamanisha
Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa katika
eneo hili ni ile yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya,
elimu na ujuzi, upatikanaji wa chakula na lishe bora na huduma za maji
safi na salama. Shughuli zitakazotiliwa mkazo ni pamoja na kugharamia
utoaji wa elimu msingi bila ada, kupunguza vifo vya akina mama
vinavyotokana na uzazi, utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya
Elimu (Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu), ujenzi na
ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi nchini, kuboresha huduma za maji
vijijini;
(iii) Uboreshaji wa
Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji: Miradi
itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kuendeleza
ujenzi na ukarabati wa miundombinu (reli, bandari, nishati, viwanja vya
ndege, barabara). Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji
Rufiji MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; Ujenzi wa Reli ya
Kati kwa kiwango cha Standard Gauge; na kuendelea na
utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na
Uwekezaji. Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 umeweka
msukumo katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza
ikiwemo kupitia upya mfumo wa kitaasisi, kisera na kisheria pamoja na
kanuni zake ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika
kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo; na
(iv) Kuimarisha usimamizi
wa utekelezaji wa Mpango: Miradi inayotekelezwa katika eneo hili
inalenga kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa Mpango, kuweka
mfumo utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha na kuweka
vigezo vya upimaji wa mafanikio ya utekelezaji.
SEHEMU YA TATU
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19 NA MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2019/20
- TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19
- Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018/19, Serikali ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 32,476.0. Kiasi hicho kinajumuisha: mapato ya ndani shilingi bilioni 20,894.6; misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo shilingi bilioni 2,676.6; na mikopo yenye masharti ya kibiashara kutoka vyanzo vya ndani na nje shilingi bilioni 8,904.7. Aidha, matumizi ya kawaida yalikadiriwa kuwa shilingi bilioni 20,468.7 na matumizi ya maendeleo shilingi bilioni 12,007.3.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 9,111.9, mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni 1,522.9 na mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 371.7.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kama ilivyoainishwa ndani ya Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na Uwekezaji (Blueprint) kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya Serikali. Hatua hizo ni pamoja na: Kupunguza kodi kwa wachimbaji wadogo wa madini; Ugawaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wadogo; Kupunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye pombe kali zinazotengenezwa nchini kwa kutumia zabibu zinazozalishwa nchini; Kuweka utaratibu mpya wa ukusanyaji wa kodi ya majengo; Kuboresha mifumo ya TEHAMA ya kukusanya kodi na maduhuli ikiwemo Electronic Fiscal Device Management System (EFDMS) ambao hupokea na kutunza kumbukumbu za utoaji wa risiti za mauzo.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Januari 2019, Washirika wa Maendeleo walitoa jumla ya shilingi bilioni 1,034.8. Kati ya kiasi kilichotolewa, misaada na mikopo nafuu ya Kibajeti ilikuwa shilingi bilioni 125.4 na miradi ya maendeleo shilingi bilioni 782.0. Mifuko ya Kisekta ilipokea shilingi bilioni 127.4.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, Serikali ilikopa shilingi bilioni 2,025.0 kutoka soko la ndani. Aidha, katika kipindi hicho, Serikali ilifanya majadiliano na taasisi mbalimbali za kifedha za kimataifa na kupata shilingi bilioni 458.6 kutoka Benki ya Credit Suisse mwezi Februari 2019 na shilingi bilioni 247.7 zinatarajiwa kupatikana kutoka benki ya HSBC hivi karibuni. Vile vile, Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na baadhi ya wakopeshaji walioonesha nia ya kuikopesha Serikali kwa mwaka 2018/19.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya jumla ya shilingi bilioni 13,750.6. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 10,962.1 zilitolewa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi bilioni 2,788.5 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Mahitaji yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha ni pamoja na: Ulipaji wa deni la Serikali ikijumuisha michango ya mwajiri katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii shilingi bilioni 5,465.9 ambapo Shilingi bilioni 3,803.4 zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo; na mishahara ya watumishi wa Serikali shilingi bilioni 3,890.0. Serikali imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 1,433.8 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo mradi wa kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji Mto Rufiji (MW 2,115).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ili kufikia malengo ya bajeti ya mwaka 2018/19. Miongoni mwa mikakati hiyo ni: Kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari kupitia vipindi mbalimbali vya elimu kwa umma; Kutekeleza mwongozo wa ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo; Kuendelea kusisitiza nidhamu ya matumizi katika utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015; kulipa madai yote yaliyohakikiwa ya makandarasi; Kuanza kutumika kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Stampu za kodi (ETS) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi; na Kutekeleza Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS) ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa makusanyo ya kodi za ndani.
- SERA ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/20
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera za mapato kwa mwaka 2019/20 zitalenga: Kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogondogo na za kati pamoja na ukuaji wa uchumi endelevu; Kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari, upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika usimamizi wa kodi; Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; Kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wakala za Serikali na Mamlaka za Udhibiti; na Kuwajengea uwezo maafisa wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala na Halmashauri ili kuimarisha uwezo wa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa mazingira haya utawezesha kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uwekezaji, uzalishaji, ajira na miamala ya biashara ambayo kwa ujumla itachangia kuongezeka kwa vyanzo vya mapato. Aidha, kwa upande wa misaada na mikopo nafuu, Serikali itaendelea kuimarisha mahusiano kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Ushirikiano na Washirika wa Maendeleo.
No comments :
Post a Comment