Friday, March 1, 2019

BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA


1
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akisalimiana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina alipomtembelea ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo maalum, baada ya Mkutano  wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki, Abidjan, Ivory Coast
2-min
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Gabriel Negatu, muda mchache kabla ya kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, Abidjan, Ivory Coast.
3-min
Washiriki wa Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Rais Mwandamizi wa AfDB, Bw. Charles Boamah, Abidjan nchini Ivory Coast.
4-min
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akichangia mada katika Mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, uliofanyika Abidjan, Ivory Coast, kulia ni Katibu Mkuu wa Benki hiyo, Prof. Vicent Nmehielle.
5-min
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akijadili jambo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, baada ya Mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki na Rais huyo,  Abidjan, Ivory Coast.
6-min
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Dkt. Akinumwi Adesina na baadhi ya wajumbe wa benki hiyo, baada ya kikao maalum cha Mhe. Mpango na Rais huyo, Abidjan, Ivory Coast.

7-min
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Dkt. Akinumwi Adesina, na baadhi ya Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki waliohudhuria Mkutano wa Kikanda wa Mawaziri wa Fedha na Rais huyo, Abidjan, Ivory Coast.
(Picha na Farida Ramadhani-WFM, Abidjan, Ivory Coast)
…………………………….
Na Farida Ramadhani,  WFM, Abidjan
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika
kutekeleza miradi mbalimbali ya maedeleo ikiwemo mindombinu ya barabara, umeme na ujenzi wa viwanja vya ndege hususan Kiwanja cha Msalato mkoani Dodoma.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na  Rais wa AfDB, Dkt. Akinwumi Adesina, wakati wa  Mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki, uliofanyika Abidjan nchini Ivory Coast.
Dkt. Mpango,  ambaye pia ni Gavana wa Benki ya Maendelo ya Afrika (AfDB), alisema Rais wa Benki hiyo amekubali ombi la Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli la kuipatia Tanzania mkopo nafuu ili kuwezesha kuanza ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato mkoani Dodoma.
“Benki hii imekuwa ni ya msaada mkubwa sana na yapo maeneo mengi ambayo Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika amekubali kuendelea kushirikiana na nchi yetu”,  alisema Mhe. Mpango.
Mhe. Mpango alieleza kuwa Dkt. Adesina ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Magufuli, kwa juhudi zake za kupiga vita rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma kwa vitendo, kufanya maamuzi magumu ya kulinda rasilimali za Taifa hususan madini, kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima Serikalini, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti ukwepaji kodi.
Alisema kuwa Dkt. Adesina ameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ambazo zimesababisha Tanzania kupata mafanikio makubwa katika maendeleo kwa kipindi kifupi.
Akizungumza wakati wa  Mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki, Mhe. Mpango aliishukuru  Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kuendelea kuipatia mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
Katika mkutano huo wa Mawaziri, Mhe. Mpango aliuomba  uongozi wa Benki kuharakisha maandalizi ya miradi inayotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2019 ikiwemo: Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato (USD milini 200); Ujenzi wa Barabara ya Kuzunguka Jiji la Dodoma (USD  milioni 180).
Miradi mingine ni Mradi wa Kufua Umeme wa Maji (87 MW) wa Kakono (USD milioni 350); Ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo-Tanga/Lungalunga-Mombasa-Malindi (USD milioni 158.2); na Awamu ya Pili ya Mpango wa Kuendeleza Utawala Bora na Maendeleo ya Sekta Binafsi (USD milioni 56).
Benki ya Maendeleo ya Afrika imeahidi kuiwezesha Tanzania kupata mikopo nafuu ili miradi hiyo iweze kuanza kutekelezwa mapema. Aidha, iliahidi kuwa mkataba wa Dola za Marekani milioni 256 kwa ajili ya ujenzi ya barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) kwa kiwango cha lami utasainiwa mapema mwanzoni mwa mwezi machi, 2019.

Kwa upande mwingine,  Mawaziri wa  Fedha wa nchi za Afrika Mashariki waliohudhuria mkutano huo, walimuahidi Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kuwa wataendelea kuunga mkono kusudio la Benki hiyo la kuongeza mtaji ili kuziwezesha nchi wanachama kupata mikopo nafuu kwa ajili kutekeleza miradi ya maendeleo.

No comments :

Post a Comment