Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akiteta jambo
wakati akijiandaa kutoa kadi za Bima ya matibabu kwa Watoto wanaoishi
katika mazingira magumu mkoani Mwanza msaada ambao umetolewa na Benki ya
STANBIC. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Dkt. Philis M.
Nyimbi na kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Ruta.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akitoa hotuba
wakati wa tukio la kutoa kadi za Bima ya matibabu kwa Watoto wanaoishi
katika mazingira magumu mkoani Mwanza msaada uliotolewa na Benki ya
STANBIC katika uwanja wa Ghandi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
Wilaya ya Nyamagana, Ilemela na mkoa wa Mwanza.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akitoa kadi za
Bima ya matibabu kwa baadhi ya Watoto wanaoishi katika mazingira magumu
mkoani Mwanza msaada ambao umetolewa na Benki ya STANBIC. Kushoto ni
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Philis M. Nyimbi na kulia ni Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Thomas Ruta.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akiwa na
watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kutoka wilaya ya Ilemela na
Nyamagana muda mfupi baada ya kupatiwa msaada wa kadi za Bima ya
matibabu wengine ni viongozi wa mkoa, wilaya, maafisa ustawi wa jamii na
wadau wa malezi ya watoto na wakilishi wa STANBIC wa mkoani Mwanza.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akiwana watoto
wanaoishi katika mazingira hatarishi muda mfupi baada ya kuwakabidhi
kadi za Bima ya matibabu kwa kwa hisani ya Benki ya STANBIC mkoa wa
Mwanza.
Na mwandishi wetu Mwanza
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Ally Mwalimu amekabidhi Bima za
Matibabu kwa watoto 105 wanaoishi katika mazingira magumu leo
mkoani
Mwanza.
Waziri Ummy alikabidhi
vitambulisho hivyo vya Bima ya Afya kwa watoto hao kufuatia msaada ambao
umetolewa na Benki ya STANBIC kwa watoto hao ili kuwawezesha kumudu na
kutatua changamoto ya kimatibabu ambayo imekuwa ikiwakumba kwa muda
mrefu.
Akitoa msaada huo, Waziri Ummy
ameeleza kuwa Benki ya STANBIC imeonesha moyo ya kizalendo kwa
kuwakumbuka na kuwalipia Bima za Afya watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi wakiwemo yatima na kuongeza kuwa msaada wa bima ya mataibabu
kwa watoto hao ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wanapata malezi, makuzi
na afya bora.
Aidha, Waziri Ummy
amewashukuru watendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuchukua
hatua za haraka katika kuwasajili watoto hao waliopendekezwa na Wizara
yenye dhamana ya maendeleo na ustawi wa watoto kwa umakini wao wa
kukamilisha taratibu za utoaji wa vitambulisho vya Bima ya Afya kupitia
ufadhili wa Benki hiyo.
Kuanzia Julai 2017 hadi Juni
2018 Tanzania ilikuwa na takribani watoto 864,496 wanaoishi katika
mazingira magumu na kwa mkoa wa Mwanza peke yake una jumla ya watoto
29,474 ambapo Benki hiyo imewezesha watoto 105 jambo ambalo ni zuri
hivyo kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano wa Stanbic Bank.
Aidha, Waziri Ummy ameongeza
kuwa jumla ya watoto 6,132 walio katika Mazingira magumu walipatiwa
huduma za msingi katika ‘makao ya watoto’ 157 yanayoendeshwa na Taasisi
za dini, Mashirika ya watu binafsi na Serikali Nchini.
Aidha Waziri Ummy aliendelea
kusema kuwa katika idadi hiyo mkoa wa Mwanza peke yake una watoto 614
waishio katika makao hayo na kwa kupitia takwimu hizi ni dhahili kuwa
Serikali na wadau wengine wa Maendeleo ya Mtoto tunao wajibu wa
kuhakikisha watoto hawa wanaishi katika mazingira salama kwa kuzingatia
ustawi na maendeleo yao.
Waziri Ummy ametoa wito kwa
Watanzania na wamiliki wa Makao ya kulelea watoto wenye shida kuzingatia
Sheria na Kanuni za uendeshaji wa Makao ya Watoto jambo ambalo
litasaidia kuwa na Makao yanayotoa huduma bora za malezi na makuzi kwa
watoto ambao wametoka kwenye shida mbalimbali.
Waziri Ummy amerejea
kuupongeza uamuzi wa Benki ya STANBIC kwa kufadhili Bima za Matibabu za
watoto 900 nchini, ambapo kwa Mkoa wa Mwanza watoto 105 wamenufaika.
Uamuzi huu umekuja wakati muafaka ambapo Serikali ipo mbioni kupeleka
muswada Bungeni wa Sheria ya Bima za Matibabu kwa Wananchi wote.
Bima ya afya ni suluhisho la
utoaji wa huduma ya afya kwa kila mwananchi kabala ya kuugua na
kufikishwa hospitalini hivyo ni muhimu kubadilika na kuchangia matibabu
zaidi ya tunavyochangia huduma nyingine za kijamii.
No comments :
Post a Comment