Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi na ujumbe wake (kushoto) wakizungumza na
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Bi. Michelle Bachelet
Jeria na ujumbe wake (kulia). Mazungumzo hayo yalifanyika Mjini Geneva
nchini Uswisi Februari 27, 2019
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi na ujumbe wake katika mazungumzo na Kamishna
wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Bi. Michelle Bachelet Jeria na
ujumbe wake Mjini Geneva nchini Uswisi Februari 27, 2019
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi na ujumbe wake katika picha ya pamoja na
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Bi. Michelle Bachelet
Jeria na ujumbe wake baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao
yaliyofanyika Mjini Geneva nchini Uswisi Februari 27, 2019
……………………………………………………………………………..
Waziri wa Katiba na Sheria,Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna wa
Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Bi. Michelle Bachelet Jeria Mjini
Geneva, Uswisi.
Prof. Kabudi amekutana na
Kamishna wakati akihudhuria Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za
Binadamu
la Umoja wa Mataifa kinachoendelea Mjini Geneva-Uswisi.
Katika mazungumzo yao Kamishna
Bachelet alitaka kujua kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu haki za
binadamu nchini hususan haki za kina mama na watoto, makundi maalum na
kwa jinsi gani Baraza hilo la Mataifa linaweza kuisaidia Tanzania
kuendelea kukuza, kudumisha na kulinda haki za binadamu nchini.
Akizungumza katika mazungumzo
hayo Prof. Kabudi alisema licha ya Serikali kuendelea na mikakati
mbalimbali ya kulinda na kukuza haki za wanawake, imeendelea kutoa fursa
kwa wanawake kupata nafasi za uongozi wa juu Serikalini na kwenye
taasisi mbalimbali za umma ambazo zinawawezesha kushiriki katika utoaji
wa maamuzi yenye manufaa kwa nchi.
Prof. Kabudi alisema Tanzania
inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari na uwepo wa vyama vya siasa na
demokrasia nchini na kuongeza kuwa mwaka huu inatarajia kufanya uchaguzi
wa Serikali za Mitaa ambao utafuatiwa na uchaguzi mkuu utakaofanyika
mwaka 2020.
Prof. Kabudi alimhakikishia
Kamishna Bachelet kuwa Tanzania itaendelea na jitihada za kukuza,
kuheshimu na kulinda haki za binadamu nchini pamoja na kutekeleza wajibu
wake na ahadi zake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa
Mataifa.
Aidha Prof. Kabudi alielezea
jitihada zinazofanwa na Serikali kwenye maeneo ya elimu, afya, mapambano
dhidi ya rushwa na dawa za kulevya pamoja na malengo ya kuleta
maendeleo nchini.
Prof. Kabudi alisema Serikali
imeboresha mfumo wa ukusanyaji kodi na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa
huduma za kijamii kwa wananchi wake bila ubaguzi.
Mhe. Kabudi alimshukuru Kamishna
Bachelet kwa ushirikiano uliopo kati ya Ofisi yake na Wizara ya Katiba
na Sheria na Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Mjini Geneva-Uswisi na kwamba
Serikali kwa ujumla itaendelea na mazungumzo kuhusu maeneo ambayo
wataweza kushirikiana.
Ofisi ya Kamishna ya Umoja wa
Mataifa ya Haki za Binadamu iliundwa mwaka 1993 ili kusimamia ukuzaji na
ulinzi wa haki za binadamu duniani. Ofisi ya Kamishna wa Haki za
Binadamu pamoja na mambo mengine inazisaidia Serikali za nchi wanachama
wa Umoja wa Mataifa kwa kutoa mafunzo na utaalamu kwenye maeneo ya
upatikanaji wa haki, mabadiliko ya sheria na masuala ya uchaguzi. Vile
vile inazisadia Serikali za Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa
kutekeleza wajibu walionao kimataifa wa kulinda, kuheshimu na kukuza
haki za binadamu.
No comments :
Post a Comment