Thursday, February 28, 2019

MKURUGENZI WA UKAGUZI WA MIGODI NA MAZINGIRA, TUME YA MADINI AONGOZA ZIARA YA KAMATI YA KITAIFA YA UFUNGAJI MIGODI KATIKA MGODI WA DHAHABU WA GEITA


PICHA NA 1-min
Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita.
PICHA NA 2-min
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira  kutoka Tume ya Madini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji wa Migodi, Dkt. Abdulrahaman Mwanga (kulia) akikagua sehemu ya kuhifadhia maji yenye kemikali kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita tarehe 27 Februari, 2019.
PICHA NA 3-min
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira  kutoka Tume ya Madini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji wa Migodi, Dkt. Abdulrahaman Mwanga (kulia) akitoa maelekezo kwa uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita.
PICHA NA 4-min
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira  kutoka Tume ya Madini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji wa Migodi, Dkt. Abdulrahaman Mwanga (kulia mbele) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji wa Migodi wakiendelea na ziara katika sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)
………………………………….
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira  kutoka Tume ya Madini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji wa Migodi, Dkt. Abdulrahaman Mwanga ameongoza wajumbe wa kamati hiyo katika ziara kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) uliopo Wilayani Geita mkoani Geita. Ziara hiyo ni sehemu ya kikao chake kilichofanyika
mgodini hapo kwa ajili ya kujadili Mpango wa Ufungaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Washiriki wa Kamati hiyo  walikuwa ni kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga, Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wengine ni kutoka katika Wizara ya Maji, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Muungano.
Akizungumzia kikao hicho kilichoanza tangu siku ya Jumatatu, Dkt. Mwanga alieleza kuwa lengo la kikao lilikuwa ni kujadili Mpango wa Ufungaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na kusisitiza kuwa iwapo watauridhia wataupitisha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Aliendelea kusema kuwa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) umeandaa mpango huo ambapo ufungaji wa mgodi  unaweza kufanyika kuanzia miaka 10 ijayo au hata zaidi kutokana na utafiti wa madini mengine unaoendelea.
“Hapa ieleweke kuwa mgodi unaweza kuendelea na shughuli zake hata baada ya miaka 10 iwapo kutagundulika madini mengine na kuendelea kuchimba kama kawaida,” alisema Dkt. Mwanga.
Alisisitiza kuwa, Mpango wa Ufungaji wa Mgodi wa Madini ni muhimu kwa mgodi wa aina yoyote nchini na kusisitiza kuwa unatakiwa  kundaliwa mwanzoni mwa shughuli za madini zinapoanza.
Akielezea umuhimu wa kuwepo kwa Mpango wa Ufungaji wa Mgodi, Dkt. Mwanga alisema kuwa, unasaidia mgodi kujiandaa katika udhibiti wa uharibifu wa mazingira unaoweza kujitokeza wakati wa shughuli za uchimbaji wa madini na pamoja na kuwasaidia wananchi kuwa na uchumi endelevu mara baada ya kukamilika kwa shughuli za uchimbaji wa madini.
“Kama Serikali tunapenda kuhakikisha shughuli za kiuchumi za wananchi wanaoishi karibu na migodi inayotarajiwa kufungwa haziathiriki na ufungaji wa migodi husika,” alisisitiza Dkt. Mwanga.
Katika hatua nyingine katika ziara hiyo Dkt. Mwanga alishauri mgodi huo kuhakikisha mali zenye thamani ambazo zinafaa kwa matumizi mengine mara baada ya ufungaji wa mgodi zinaendelea kutumika ili kunufaisha jamii inayozunguka mgodi hususan katika ajira hivyo kujiingizia kipato.
Aidha aliutaka mgodi kuendelea kujiandaa kwa kusawazisha maeneo yenye mashimo pamoja na kupanda miti yenye thamani.

No comments :

Post a Comment