Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu (kulia) akiwasha rasmi umeme katika kijiji cha Ntauna, Kata ya
Rondo, Lindi Vijijini, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 27, 2019.
Wengine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga (kushoto),
Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye (wa pili-kushoto) na Afisa wa
TANESCO Lindi.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu akizungumza wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika
kijiji cha Mvuleni, Lindi Vijijini, Februari 27, 2019. Kushoto kwa Naibu
Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga na wa pili kutoka
kushoto ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu akizungumza wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika
kijiji cha Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, akiwa katika ziara ya
kazi, Februari 27, 2019.
Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape
Nnauye akizungumza, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu (mwenye kilemba cha njano – meza kuu) kijijini Ntauna, Kata ya
Rondo, Lindi Vijijini, Februari 27, 2019. Naibu Waziri aliwasha rasmi
umeme kijijini hapo.
Sehemu ya umati wa wananchi wa
kijiji cha Mvuleni, Lindi Vijijini, wakimsikiliza Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kabla
ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo, Februari 27, 2019.
Viongozi mbalimbali wa Serikali
mkoani Lindi, wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (aliyesimama), wakati akizungumza
na wananchi wa kijiji cha Mvuleni, Lindi Vijijini, alipokuwa katika
ziara ya kazi, Februari 27, 2019. Naibu Waziri aliwasha rasmi umeme
katika kijiji hicho.
…………………
Na Veronica Simba – Lindi
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu amewataka watanzania kuondoa shaka kuhusu mipango ya serikali
kufuatia gesi iliyogunduliwa mikoa ya kusini, kwani haijabadilika na
inaendelea kutekelezwa.
Aliyasema hayo jana Februari 27,
2019 kijijini Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, alipokuwa
akihitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Lindi ambapo alikagua
utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya umeme, kuwasha umeme katika vijiji
mbalimbali na kuzungumza na wananchi.
“Nataka niwaaminishe wana-kusini,
yale ambayo serikali iliahidi baada ya kugundua gesi, mipango yake iko
palepale na inafanyiwa kazi,” alisema.
Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Mgalu alisema moja ya mambo ambayo serikali iliahidi ni umeme wa uhakika utakaowezesha uwekezaji.
Alisema hadi sasa, taratibu za
kukamilisha ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa gesi Mtwara wenye
megawati 300 na Somanga Fungu wenye megawati 330 ziko katika hatua za
mwisho.
“Mradi utaanza ndani ya mwaka huu
wa fedha ambao utawezesha mikoa hii kuzalisha umeme wa kutosha kuweza
kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.”
Aidha, aliongeza kuwa, jambo
jingine kubwa ni kuviwezesha viwanda vya maeneo husika kupata umeme wa
gesi ambapo alisema tayari kiwanda cha saruji cha Dangote
kimeshaunganishiwa.
Pia, alisema, serikali inaendelea
kuzungumza na viwanda vya mbolea ili vizalishe mbolea inayotokana na
gesi ili pamoja na mambo mengine viongeze ajira kwa wananchi.
Vilevile, alisema kwa Mkoa wa
Lindi, eneo la Likongo, serikali inatarajia kujenga kiwanda cha
kusindika gesi iwe katika hali ya kimiminika ambapo Rais John Magufuli
ametoa mwongozo wa kufanya mazungumzo na mbia mmoja mmoja. Alisema
mazungumzo yanaendelea vizuri.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alizungumzia tathmini ya ziara yake mkoani Lindi, ambapo alisema imekuwa yenye mafanikio.
Alisema, kazi ya kuwaunganishia
wananchi umeme vijijini inaendelea na ametoa wito kwa mkandarasi husika
kuboresha utendaji wake ili kuhakikisha anafikia malengo ya kukamilisha
kazi yote kwa mujibu wa mkataba ifikapo Juni 30, mwaka huu ambapo ndipo
mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza utakuwa
unahitimishwa.
Naibu Waziri alisema yeyé pamoja
na viongozi wengine wa Lindi akiwemo Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na
Wabunge wamekubaliana kumsimamia mkandarasi husika katika kuhakikisha
anatimiza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya
Lindi, Shaibu Ndemanga, ambaye alifuatana na Waziri wakati akihitimisha
ziara yake, aliwahakikishia wananchi wa eneo husika kuwa yeyé pamoja na
viongozi wenzake watamsimamia mkandarasi husika ili kuhakikisha kazi
inatekelezwa kwa ufanisi.
“Tumekabidhiwa hawa tuwasimamie,
kwa hiyo nichukue nafasi hii kuwathibitishia kwamba tutawasimamia
kwelikweli ili kuhakikisha zoezi hili linakamilika vizuri sana,”
alisisitiza.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mtama,
Nape Nnauye, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa upande wa nishati
ambapo alisema imekuwa ikifanya kazi nzuri sana.
“Tunawashukuru sana Wizara ya
Nishati kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kama kuna Wizara inafanya vizuri,
basi Wizara hii inafanya vizuri.”
Hata hivyo, Nnape alisema
anatambua kiu kubwa ya umeme waliyonayo wananchi na kuwasihi kuwa
wastahimilivu maana zoezi la kuunganisha umeme ni hatua kwa hatua, awamu
kwa awamu. Alisema anayo imani kubwa kwamba vijiji vyote vitafikiwa na
huduma hiyo kabla ya mradi kuisha.
Mkurugenzi wa kampuni ya State
Grid, ambayo ndiyo inatekeleza uunganishaji wa umeme mkoani Lindi,
Charles Mlawa, akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo,
aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri katika
kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi.
Katika ziara hiyo, viongozi wa
ngazi mbalimbali walipongeza utendaji kazi wa Wizara pamoja na Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuomba jitihada zinazofanyika ziendelee.
Katika Miradi ya Umeme Vijijini,
Mzunguko wa Kwanza (REA III – 1), jumla ya vijiji takribani 133
vitaunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi bilioni 31.9. Matarajio ni
kuwaunganishia wananchi takribani 5,337.
Akiwa Lindi vijijini, Naibu Waziri aliwasha umeme katika vijiji vya Ntauna, Mvuleni na Tulieni.
No comments :
Post a Comment