Tuesday, January 29, 2019

WASAUDIA WATUA TANZANIA KUTAFUTA FURSA ZA KUWEKEZA KATIKA VIWANDA


TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Wasaudia watafuta Fursa za Kuwekeza katika Viwanda Tanzania
 
Ujumbe
wa wawekezaji wa makampuni makubwa 15 ya Saudi Arabia utafanya ziara nchini
Tanzania tarehe 30 na 31 Januari 2019 kwa madhumuni ya kuangalia fursa ya
kuwekeza kwenye viwanda.
 
Ziara
hiyo inatokana na juhudi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kupitia Ubalozi wa Saudi Arabia na wadau wengine  wa kushawishi wafanyabiashara wakubwa kuja
kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.
 
Ujumbe
huo wa watu 20, utakapokuwa nchini pamoja na mambo mengine, utashiriki
kongamano la biashara litakalofanyika kwenye Hoteli ya New Africa jijini Dar Es
Salaam tarehe 30 Januari 2019 kuanzia saa mbili asubuhi. Kongamano hilo litafuatiwa
na mazungumzo ya ana kwa ana baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Saudi
Arabia.
 
Kongamano
hilo linaloratibiwa na Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima
(TCCIA) litatoa fursa kwa wafanyabiashara hao kusikiliza mada mbalimbali kuhusu
fursa, vivutio, sheria na kanuni za uwekezaji nchini kutoka taasisi
zinazoratibu masuala ya uwekezaji ikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
 
Ujumbe
huo pia unatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi mbalimbali; zikiwemo
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania
(TANTRADE), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Uwekezaji na
Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).
 
Ziara
ya ujumbe huo ni moja ya mikakati ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
inayojikita katika diplomasia ya uchumi na inalenga kuhamasisha uwekezaji katika
sekta ya viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe.
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
 
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki,
Dodoma.
29 Januari
2019
  

No comments :

Post a Comment