Waziri wa Madini Doto Biteko
akitafakari jambo wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika eneo ambalo
shughuli za uuzaji wa madini zinafanyika bila kuwa na leseni. Mbele ni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila. Wengine ni
Maafisa wa Wizara.
Waziri wa Madini Doto Biteko
akieleza jambo wakati akimhoji Munuzi wa Madini Matondo Michembe (wa
pili kulia) ambaye alikutwa akifanya shughuli hizo bila kuwa na leseni
ya kufanya biashara hiyo. Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini, Doto Biteko.
Waziri wa Madini Doto Biteko
akieleza jambo wakati alipotembelea kiwanda cha kuchenjua madini ya
dhahabu cha Umoja eneo la Viwanda la Kizota wakati wa ziara yake ya
kushtukiza. Katikati kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof.
Simon Msanjila, wengine ni Watumishi wa kiwanda hicho kushoto, Katikati
mwenye suruali ya blue ni Afisa aliyesimamishwa kazi, Fundi Sanifu
Asheni Daudi, anayefuatia ni Afisa Madini wizara ya madini, Mhandisi
Assah Mwakilembe.
………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini
Profesa Simon Msanjila amemsimamisha kazi Fundi Sanifu wa Madini, Asheni
Daudi wa Ofisi ya Madini Dodoma baada ya kuagizwa na Waziri wa
Madini
Dotto Biteko.
Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri
Biteko akiongozana na Katibu Mkuu na Wataalam wengine wa wizara
vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, kufanya ziara ya kushtukiza
katika Kiwanda cha Kuchenjua madini ya Dhahabu cha Umoja kilichopo eneo
la Viwanda la Kizota (Industrial Area) na kubaini mapungufu makubwa
katika utendaji kazi wa wataalamu hususan uandaaji wa tarifa za
uzalishaji wa madini.
Akizungumza katika eneo hilo,
Waziri Biteko alisema wizara ilipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu
mienendo inayoendelea katika eneo hilo ambapo wahusika ambao ni Maafisa
Madini wamekuwa hawatoi taarifa halisi za uzito na ubora wa dhahabu
zinazozalishwa baada ya kuchenjuliwa, hivyo, serikali kukosa mapato
stahiki.
Waziri Biteko ameongeza kuwa,
tayari anayo majina yote ya wanaofanya michezo ya ujanja ujanja kwenye
viwanda vya kuchenjua dhahabu, huku akieleza kuwa, hatua madhubuti
zitachukuliwa kwa wote wanaofanya vitendo hivyo na kuongeza kwamba,
zoezi hilo litakuwa endelevu kwa lengo la kuwabaini wanaojihusisha na
vitendo hivyo na kuwataka maafisa madini kuwa makini.
“Nakuagiza Kamishna wa Madini
David Mulagwa kufanya kaguzi katika viwanda vyote vya kuchenjua dhahabu
kwa lengo la kubaini utendaji wa kazi wa viwanda hivyo, ikiwemo taarifa
za uzalishaji zinazotolewa na Lazima tufike mahali tuheshimu taratibu,
madini haya ni mali ya nchi”, alisema Biteko.
Wakati huo huo, Waziri Biteko
alimtaka Afisa Madini Mkoa wa Dodoma Jonasi Mwano kujitathmini kutokana
na mambo yanavyokwenda katika eneo lake la kazi na kumtaka kuwasilisha
kwa Kamishna wa Madini na kwa Waziri wa Madini taarifa za uzalishaji
madini ya dhahabu kwa kipindi cha miezi sita.
Pia, katika ziara yake, Waziri
Biteko alibaini mnunuzi wa madini ya dhahabu katika eneo la Kizota
aliyefahamika kwa jina la Matondo Michembe ambaye anafanya shughuli hizo
bila kuwa na leseni ya biashara ya madini hayo. Hivyo, alimwagiza
Michembe kuwasilisha taarifa za utendaji wake kwa Kamishna wa Madini na
Waziri wa Madini hususan soko analouzia madini hayo ya dhahabu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Prof.
Simon Msanjila ameelezea kuwa, kiutaratibu ilikuwa lazima taarifa za
uzalishaji na kiasi kilichozalishwa kujazwa katika vitabu maalum ndani
ya kiwanda hicho lakini jambo hilo halikufanyika kama inavyotakiwa.
Aidha ameongeza kuwa, Afisa huyo amesimamishwa ili kupisha uchunguzi na endapo itabainika, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa.
No comments :
Post a Comment