Thursday, January 31, 2019

KAMPUNI YA KENYA KUNUNUA TANI LAKI MOJA ZA KOROSHO GHAFI TANZANIA


Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Dkt. Hussein Mansoor (kushoto) kwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INDO Power Solutions ya nchini Kenya, Bw. Brian Mutembei (kulia) wakisaini Mkataba wa mauziano ya korosho ghafi kiasi cha tani laki moja kwa malipo ya Shilingii bilioni 418. Wanaoshuhudia tukio hilo muhimu ni Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (wa pili kushoto), Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Kakunda (kushoto), Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Innocent Bashungwa (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Kilimo na Mhe. Dan Kazungu, Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini. Tukio hilo lilifanyika kwenye Ukumbi wa mikutano uliopo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 30 januari 2019. Mawaziri hao wapo jijini humo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki


Dkt. Mansoor na Bw. Mutembei wakibadilishana Mkataba huo mara baada ya kusaini
Mhe. Prof. Kabudi akizungumza kabla ya kuanza kwa tukio hilo la kihistoria la kusainiwa mkataba wa ununuzi wa tani laki moja za korosho ghafi
Mhe. Kakunda nae akizungumza
Mhe. Dkt. Bashungwa akizungumza mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani)
Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Kazungu akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya kusainiwa mkataba wa ununuzi wa tani laki moja za korosho kutoka Tanzania
Bw. Mutembei nae akieleza furaha yake katika kukamilisha ununuzi wa korosho kutoka Tanzania
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Joseph Buchweshaija akizungumza kwa ufupi kuhusu hafla hiyo ya uwekaji saini mkataba wa ununuzi wa korosho. Wengine katika picha ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Mhe. Prof. Florens Luoga ( kulia walioketi) akifuatiwa na Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria na Dkt. Evaristo Longopa, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Mkutano ukiendelea. Kushoto ni Mkurugenzi wa TanTrade, Bw. Edwin Rutageruka
=============================================================================================
Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya
Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imesaini mkataba wa mauzo ya korosho
ghafi kiasi cha tani laki moja kwa Kampuni ya Kenya ya INDO Power Solutions kwa
malipo ya Shilingi bilioni 418.
Mkataba huo umesainiwa jijini Arusha
tarehe 30 Januari 2019 kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Dkt. Hussein
Mansoor kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw. Brian Mutembei, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya INDO Power Solutions ya nchini Kenya.
Tukio hilo la kihistoria lilishuhudiwa
na Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Kakunda,
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Innocent Bashungwa, 
Naibu Waziri wa Kilimo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga,  Dkt. Evaristo Longopa, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Viongozi wengine walioshuhudia ni
Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu, Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Joseph Buchweshaija, Katibu Mkuu wa Viwanda
na Biashara, Prof. Siza Tumbo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Edwin
Rutaberuka, Mkurugenzi wa TanTrade, Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini na
Waandishi wa Habari.
Awali wakizungumza kabla ya
kusainiwa kwa Mkataba huo Mawaziri hao wakiongozwa na Prof. Kabudi, kwa pamoja walipongeza
kwa dhati uamuzi wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wa Serikali kununua korosho kutoka kwa wakulima ili
kuepusha wakulima hao kuuza korosho zao kwa bei ya chini kwa watu wasio kuwa na
nia njema kwa wakulima. Itakumbukwa kuwa, mwezi Novemba 2018, Mhe. Rais
Magufuli alitoa maelekezo kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na
Wizara ya Kilimo waratibu zoezi  la
ununuzi wa korosho kutoka kwa wakulima kwa shilingi 3,300 kwa kilo moja.
Kwa upande wake Prof. Kabudi alisema
kuwa anampongeza  Mhe. Rais Magufuli kwa
uamuzi huo wa Serikali kununua korosho yote ili wakulima wapate bei
inayolingana na jasho lao ambao hatimaye umezaa matunda kwa faida na maendeleo
ya nchi.
Naye Mhe. Kakunda alieleza kuwa Bw.
Mutembei ni mnunuzi wa kwanza kati ya wengi ambao walikuwa kwenye mazungumzo na
Serikali kuhusu ununuzi wa korosho hizo. Mhe. Kakunda alisema katika majadiliano
Serikali iliangalia kufanya biashara ya faida ambayo itawezehsa kulipa gharama mbalimbali
ikiwemo gharama za upakiaji na upakuaji, malipo kwenye Serikali za Mtaa na
michango mingine ya kijamii kwa mujibu wa makubaliano. Hivyo aliwataka
watanzania na wenye viwanda kutokuwa na wasiwasi kwani Serikali ina nia njema
ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan kupitia sekta ya kilimo cha korosho.
“Wakulima wa Korosho wanatakiwa
kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi wake ambao unalinda maslahi ya mkulima
na umewawezesha kuuza korosho zao kwa faida. Nawakaribisha wafanyabiasha makini
kuja nchini kwani Serikali ipo tayari kuwasikiliza watu wa aina hiyo na kufanya
nao biashara” alisema Mhe. Kakunda.
Kwa upande wake, Mhe. Bashungwa
alieleza kuwa katika msimu wa korosho wa mwaka 2018/2019 tayari zimekusanywa
tani 213,159 ambazo kati ya hizo tani 126,194 zimehakikiwa na tayari  wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na
Pwani wamelipwa fedha zao kwa zaidi ya asilimia 95.5. Mhe. Bashungwa aliongeza
kuwa, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Wakulima wote kulipwa fedha zao hadi
kufikia tarehe 05 Februari 2019.
Akizungumza wakati wa tukio hilo,
Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Kazungu alisema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni
faraja kubwa kwake katika historia ya mahusiano kati ya Tanzania na Kenya
ambayo yanaendelea kuimarika siku hadi siku. Aidha, alieleza kuwa mkataba huo
ni mfano mzuri wa kuimarika kwa mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
hususan katika masuala ya kilimo na biashara.
Kwa upande wake, mnunuzi wa korosho
hizo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Indo Power Solutions, Bw.
Mutembei alisema amekuja kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Magufuli za
kumwinua mkulima wa Tanzania na kwamba anawataka wale wote wanaobeza jitihada
hizo za Mhe. Rais Magufuli kuacha mara moja huku akilaani kitendo cha baadhi ya
wafanyabiashara kuendelea kuwakandamiza wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei
ndogo wanazopanga wao huku wakijua wazi kuwa wakulima hao wametumia gharama
kubwa katika uzalishaji wa mazao hayo.
Pia aliwataka wafanyabiashara
kufuata taratibu na sheria katika kufanya biashara kama Serikali zinavyoelekeza
na kuacha kuchanganya biashara na siasa.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka,
Dkt. Mansoor alieleza kufurahishwa na tukio hilo ambalo limekuja wakati mwafaka
wakati nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikijiandaa na Mkutano wa
Wakuu wa Nchi utakaofanyika jijini humo hivi karibuni. Aidha alisema kuwa, kwa
kiasi kikubwa tukio hilo limeiinua Bodi yake na kwamba anatoa wito kwa wafanyabiasha
wengine wa ndani na nje ya Tanzania kuja nchini na kushirikiana na Bodi hiyo
ili kuwakomboa wakulima wengi Zaidi.
Mkataba huo umesainiwa wakati baadhi
ya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Tanzania wakiwa jijini Arusha kwa ajili ya kuhudhuria
vikao vya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
utakaofanyika kwenye Kituo cha  Mikutano
cha Kimataifa cha Arusha (AICC) tarehe 1 Februari 2019.

No comments :

Post a Comment