Tuesday, January 29, 2019

Kampuni ya Utalii ya Wengert Windrose Safari Yatoa Mamilioni kwa Vijiji 12 Longido


 
Mkuu wa wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe akiwa na baadhi ya viongozi wa vijiji na wafanyakazi wa kampuni ya Wingert Windrose Safaris baada ya kukabidhiwa hundi.


Mwandishi wetu,Arusha.
Arusha.Kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Wengert Windrose Safaris imetoa kiasi cha sh 36 milioni kwa Vijiji 12 vinavyozunguka kitalu cha uwindaji cha Lake Natron North wilayani Longido ili kuchangia huduma na miradi ya maendeleo.
 
Meneja mahusiano ya kampuni hiyo, Clarence Msafiri alimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Longido,Frank Mwaisumbe mfano wa hundi kwa niaba ya vijiji hivyo kisha kukabidhi hundi halisi yenye thamani ya Sh 3 milioni kwa kila kijiji.
 
Vijiji vilivyonufaika na fedha hizo ni Mairowa,Magadini,Gelai,Wosiwosi,Ngoswaki na Matale A, Origrai,Matele B,Lumbwa ,Ilnjakitsapukin ,Kimwati na Alaililai ambapo pia kampuni hiyo imetoa fedha nyingine kiasi cha dola 5000 zaidi ya sh 11 milioni kuchangia huduma za jamii kupitia ada ya kitalu chake cha uwindaji.
 
Akizungumza baada ya kukabidhiwa hundi hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya, Mwaisumbe aliwataka viongozi wa vijiji kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo hasa katika kipindi hiki ambacho ujenzi wa madarasa unaendelea kwa kasi ili kutoa nafasi kwa watoto wa jamii hiyo ya wafugaji kupata fursa ya elimu.
 
Mwaisumbe alisema anaishukuru sana, Kampuni ya Wengert kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika wilaya hiyo, kutokana na kujitoa kuchangia shughuli nyingi za maendeleo katika wilaya hiyo.
 
“Naishukuru kampuni hii kwa kuonesha uzalendo na kuheshimu makubaliano kusaidia vijiji na naamini mtaendelea kushirikiana katika kuhakikisha Longido tunakua na uhifadhi endelevu unaozingatia ustawi wa jamii inazunguka maliasili zetu,”alisema Mwaisumbe
 
Meneja Mahusiano wa kampuni ya Wenget Windrose Safaris Limited,Clarence Msafiri alisema wataendelea kushirikiana na vijiji vinavyowazunguka kuchangia huduma za jamii.
 
Msafiri alisema licha ya fedha hizo, kampuni hiyo pia itaendelea kutoa ajira kwa vijana wa jamii inayowazunguka lakini pia tayari wametoa kiasi cha dola 5000 sawa ni Sh 11.5 milioni ambayo ni malipo kwaajili ya kila kitalu kila mwaka.
 
Msafiri alitaja vijiji vilivyonufaika kuwa ni Mairowa,Magadini,Gelai,Wosiwosi,Ngoswaki na Matale A,vijiji vingine ni Origra,Matele B,Lumbwa ,Ilnjakitsapukin ,Kimwati na Alaililai.
 
Akizungumza kwa niaba ya vijiji hivyo, Diwani wa Kata ya Mundarara ,Alais Mushao alisema mchango wa uhifadhi ni muhimu katika kuinua na kuchangia shughuli za maendeleo na kuitaka kampuni hiyo kufanya kazi zake kwa kutunza mazingira ili rasilimali hizo zinufaishe vizazi vijavyo.
 
Kampuni ya Wingert Windrose Safaris ni kati ya kampuni zinazomilikiwa na taasisi ya Friedkin Conservation Fund(FCF) ambayo pia inamiliki kampuni ya Mwiba Holdings iliyowekeza hifadhi ya Makao na Kampuni ya Game Tracking Safaris(TGTS) ambayo imewekeza maeneo kadhaa nchini.

No comments :

Post a Comment