Na.Bushiri Matenda- MAELEZO
Chuo cha Bandari kilichopo Temeke
Jijini Dar es Salaam kinatarajia kuanza udahili wa wanafunzi wapya
kupitia mfumo wake mpya wa kidijitali ujulikanao kama Student’s
Information Management System (SIMS).
Mfumo huo wa kidijitali
uliozinduliwa jana tarehe 29-01-2019 na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe, utakiwezesha chuo hicho kudahili
wanafunzi wengi kwa wakati mmoja lakini pia kutarahisisha kazi ya
udahili tofauti na awali ilivyokuwa
ikifanyika.
Mfumo huo ambao ulibuniwa na
kutengenezwa na wafanyakazi wa TPA kitengo cha TEHAMA, pia utatumika
kukokotoa matokeo ya mitihani na kuanda taarifa ya mwisho wa mwaka wa
mafunzo yaani ‘final year transcript’.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa
tovuti ya mfumo huo mpya, Waziri Kamwelwe alisema uwepo wa mfumo huo
utasaidia kudhibiti udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya
watendaji wasiokuwa waaminifu.
Mhandisi Kamwelwe ameongeza kwamba
awali wakati udahili ulipokuwa ukifanywa kwa kujaza fomu kwa mkono
‘manual’, kulikuwa na tatizo la uchakachuaji wa vyeti na upotevu wa
pesa.
“Wakati wa application za manual
(kujisajili kupitia mikono) kuna fomu za maombi zilikuwa zinapotea na
kulikuwa na upotevu wa pesa pamoja na tatizo la kuchapisha vyeti feki na
baadhi ya wanafunzi kutohudhuria mafunzo ipasavyo,” alisema Waziri
Kamwelwe.
Mhandisi Kamwelwe ameongeza kwamba
kipindi hicho kuna baadhi ya wanafunzi waliishia kusajiliwa tu na baada
ya miaka miwili unamkuta mtaani na cheti lakini kwa uwepo wa mfumo,
hayo mambo hakuna tena.
Kwa upande wake Mkuu wa Bodi ya
Magavana ya Chuo hicho, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimshukuru Waziri kwa
kutenga muda na kuja kuwazindulia tovuti hiyo ambayo ni muhimu mno kwa
chuo hicho.
Mhandisi Kakoko ambaye pia ni
Mkurugenzi Mkuu wa TPA amesema uwepo wa mfumo huo, utarahisisha
utendaji kazi wa chuo na kudhibiti wale wote waliokuwa wakitumia mianya
ya kutokuwepo kwa mifumo hiyo, kufanya udanganyifu.
Aidha faida nyingine za mfumo huo
ni kumwezesha mwanafunzi kuweza kujisajili popote pale alipo ilimradi tu
pawe na mtandao wa intaneti, pia taarifa zote za wanafunzi wa chuo
hicho zitapatikana kidijitali kupitia mfumo huo.
Mbali na hayo, pia mfumo huo
utatumika kuzalisha taarifa ya mwisho ya matokeo ‘final year
transcript’, na utawezesha kuoana kwa mifumo ya ndani na nje ya taasisi
kama vile NACTE, NECTA na GePG.
No comments :
Post a Comment