Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisoma ramani ya Mji wa Serikali wakati alipokagua Ujenzi wa mji huo,
eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018. Wengine pichani kutoka
kushoto ni Afisa Mipango Miji katika jiji la Dodoma, William Alfayo,
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony
Mavunde, Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi na Kulia ni Katibu
wa Kikosi Kazi cha Kuhamishia Shughuli za Serikali jijini Dodoma,
Meshack Bandawe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka kwa Katibu wa Kikosi Kazi cha Kuhamishia
Shughuli za Serikali jijini Dodoma, Meshack Bandawe kuhusu Ujenzi wa Mji
wa Serikali wakati alipokagua Ujenzi huo, eneo la Ihumwa jijini Dodoma,
Desemba 27, 2018.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua Ujenzi wa jengo Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati alipokagua Ujenzi
wa Mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27,
2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitazama kazi ya kusuka nondo kwa ajili ya nguzo za jengo la Ofisi za
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora wakati alipokagua Ujenzi wa Mji wa Serikali, eneo la Ihumwa
jijini Dodoma, Desemba 27, 2018. Kulia kwake ni Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikagua Ujenzi wa Msingi wa jengo la Ofisi za Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano wakati alipokagua Ujenzi wa Mji wa Serikali,
eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
*Akuta baadhi ya wakandarasi wanasuasua, wengine wako vizuri
*Aitisha kikao cha Mawaziri, Makatibu Wakuu wote kesho saa 5 asubuhi
*Ataka leo jioni apewe taarifa ya kila taasisi inayohusika Ihumwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekagua ujenzi wa eneo la Mji wa Serikali lililoko Ihumwa na kubaini
kuwa baadhi ya wakandarasi hawaendi na kasi inayotarajiwa na Serikali.
Waziri Mkuu ameamua kuitisha
kikao cha Mawaziri wote na makatibu wakuu wote kesho (Ijumaa) saa 5
asubuhi ili waeleze kazi hiyo itakamilishwa lini.
Ametoa agizo kauli hiyo leo
mchana (Alhamisi, Desemba 27, 2018) mara baada ya kukagua
ujenzi wa
ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
katika eneo la Mtumba lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.
“Nimekagua maeneo yote na kukuta
baadhi ya wakandarasi wanatakiwa kujenga majengo ya wizara nne hadi
tano. Sijaridhika na baadhi ya kazi, nimeitisha kikao cha Mawaziri wote
kesho ili tuangalie ni mkandarasi yupi anaweza kumudu hii kazi.”
“Nimebaini kuna tatizo kubwa la
upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama kokoto, nondo, matofali na kikao
cha kesho kitahusisha Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wa Mkoa na Jiji
la Dodoma, wakandarasi wote ili tukubaliane kazi hii inaisha lini,”
amesema.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu
amesema wajasiriamali wanaotengeza matofali Dodoma wako wengi lakini
matofali tyao yako chini ya kiwango, kwa hiyo wanatakiwa watu wa
kutengeneza matofali mengi yenye uimara. “Tuna ujenzi wa wizara 24,
tunataka matofali imara siyo yale ambayo ukilishika tu, mchanga
unamomonyoka,” amesisitiza.
Akisisitiza uharaka wa kazi
hiyo, Waziri Mkuu amesema kazi hiyo ina malengo maalum na inatakiwa
ikamilike haraka sana. “Tarehe ya mwisho ya kukamilisha ujenzi
iliyotolewa na Mheshimiwa Rais ilikuwa Desemba 31, mwaka huu lakini kuna
sababu zimetajwa kukwamisha ujenzi huo zikiwemo mvua na uhaba wa
kokoto,” amesema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesifia
kazi nzuri iliyofanywa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Utumishi,
Ujenzi, Katiba na Sheria, Maji na Elimu. Kazi hizo zimefanywa na
wakandarasi ambao ni Magereza, SUMA JKT, Wakala wa Majengo (TBA) na
Vikosi vya Ujenzi vya Mwanza na Dar es Salaam vilivyoko chini ya Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Wakandarasi walioboronga ni JWTZ – Mzinga, National Housing na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Waziri Mkuu amemwagiza Katibu wa
Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma, Bw.
Meshack Bandawe ahakakishe anapokea taarifa kutoka kila taasisi
inayohusika na ujenzi huko Ihumwa na akishaijumuisha, aiwasilishe kwake
ifikapo leo jioni.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Godwin Kunambi
ashirikiane na Mkurugenzi wenzake wa Chamwiono kuhakikisha vijana wengi
wanapata fursa za ajira kwenye mradi huo.
“Mkurugenzi wa Jiji wasiliana na
Mkurugenzi mwenzako wa Chamwino mhakikishe vijana na akina mama
wanakuja kufanya kazi hapa. Pia itisha kikao cha waandishi wa habari
uwaeleze wananchi wako fursa zilizopo, kuanzia ufyatuaji wa matofali,
uuzaji wa nondo, kokoto na utengenezaji wa pavement blocks, hizi zote ni fursa, tuna wizara 24 na mahitaji ni makubwa,” alisisitiza.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya
Waziri Mkuu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana),
Bw. Anthony Mavunde alisema zoezi la kusafisha eneo la ujenzi wa mji wa
Serikali lilianza Novemba 28, mwaka huu.
Alisema wizara zote zimepata
viwanja na zimeanza ujenzi isipokuwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira
na Vijana) ambao bado wanasubiri kupatiwa fedha.
Alisema kazi ya ujenzi wa Mji wa
Serikali inasimamiwa na Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali
kuhamia Dodoma, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma.
No comments :
Post a Comment