Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt.
Mary M. Mwanjelwa (Mb) akijibu swali la Mhe. Joram Hongoli (Mb) Bungeni
leo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora lililohusu upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wa umma walioajiriwa mwaka 2012.
………………….
Serikali imewapandisha madaraja
watumishi wa umma 113,520 walioajiriwa mwaka 2012 katika awamu tatu,
ambapo ya kwanza walipandishwa vyeo Watumishi 28,049 waliokuwa
wameidhinishiwa vyeo kabla ya zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na
uhakiki wa vyeti
kuanzia mwezi Juni, 2016, awamu ya pili ilianza mwezi
Novemba, 2017 na ilihusisha watumishi 59,967 ambao taarifa zao zilikuwa
kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS)
kabla ya zuio na awamu ya tatu ilianza mwezi Aprili, 2018 na ilihusisha
Watumishi 25,504 ambao barua zao zilikuwa hazijaingizwa kwenye Mfumo.
Ufafanuzi huo, umetolewa
Bungeni leo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) wakati akijibu swali
la Mhe. Joram Hongoli (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililohusu watumishi wa
umma walioajiriwa 2012 kutopandishwa madaraja mpaka hivi sasa.
Dkt. Mwanjelwa amesema, watumishi
walioajiriwa Mwaka 2012 walistahili kupandishwa madaraja kuanzia mwaka
2016/2017 kipindi ambacho Serikali ilikuwa ikifanya zoezi la uhakiki wa
watumishi hewa na uhakiki wa vyeti, hivyo mara baada ya kukamilika kwa
zoezi hilo Serikali ilianza kuwapandisha watumishi hao kwa awamu hizo
tatu kwa kuzingatia vigezo stahiki na kuongeza kuwa watumishi wengine
ambao wamekidhi vigezo wataendelea kukasimiwa katika bajeti ya mishahara
ili waweze kupandishwa vyeo katika mwaka huu wa fedha 2018/2019.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa
ameainisha kuwa, watumishi 31,188 walioajiriwa na TAMISEMI mwaka 2012,
kati ya hao watumishi 15,320 wamepandishwa vyeo na kubadilishiwa
mishahara, na watumishi 3,349 waajiri wao wamewapandisha vyeo lakini
majina yao yapo UTUMISHI kwa ajili ya kupitia taarifa zao kabla ya
kuwabadilishia mishahara na watumishi 1,064 waliopandishwa vyeo
wamebainika kuwa na hoja mbalimbali ambazo waajiri wanapaswa
kuzikamilisha na kurejesha majina yao UTUMISHI kwa ajili ya
kuwaidhinishia mishahara, watumishi 4,552 hawapo tena katika Utumishi wa
Umma na watumishi 6,903 bado hawajapandishwa vyeo ambapo Serikali
inatarajia kuwapandishwa vyeo wakati wowote katika mwaka huu wa fedha
2018/19.
Suala la upandishwaji vyeo
kwa Watumishi wa Umma linazingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
utendaji kazi mzuri, kukidhi sifa zilizoainishwa katika Miundo ya
Maendeleo ya Utumishi, uwepo wa nafasi wazi na bajeti iliyotegwa. Kwa
mujibu wa Miundo ya Maendeleo ya Utumishi, mtumishi anapaswa kutumikia
cheo kimoja si chini ya miaka mitatu kabla hajafikiriwa kupandishwa
cheo. Aidha, iwapo mtumishi ameajiriwa kwa mara ya kwanza atapaswa
kumaliza mwaka mmoja wa kuthibitishwa kazini kisha ndipo atumikie cheo
hicho si chini ya miaka mitatu, hivyo kwa kuzingatia sifa mtumishi
anaweza kupandishwa cheo baada ya miaka 3, 4, 5 au hata saba kutegemea
na kukidhi vigezo stahiki.
No comments :
Post a Comment