Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo (kulia mbele) na Meneja wa Kiwanda cha chokaa cha Lime Africa
kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani Songwe, Fredy
Msindo (kushoto mbele) pamoja na msafara wakiendelea na ziara katika
eneo la kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika
mkoa wa Songwe yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji
wa madini tarehe 17 Oktoba, 2018.
Meneja wa Kiwanda cha chokaa cha
Lime Africa kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani
Songwe, Fredy Msindo (katikati) akielezea shughuli zinazofanywa na
kiwanda hicho kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo pamoja na
msafara wake.
Kutoka kushoto Afisa Madini Mkazi
katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa
Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi na Afisa Madini anayesimamia
wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko wakinukuu maelekezo
yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
(hayupo pichani) katika mkutano wake na wachimbaji wadogo uliofanyika
katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe .
Sehemu ya wachimbaji wa madini ya
chokaa na ujenzi kutoka katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani
Songwe, wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani)
Diwani wa Viti Maalum kutoka
Tarafa ya Iyula iliyopo Wilayani Mbozi mkoani Songwe, Messiah Swella
akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
(hayupo pichani) katika mkutano huo.
……………………………
Na Greyson Mwase, Songwe
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo amewataka wachimbaji wa madini wanaoendesha shughuli zao za
uchimbaji wa madini ya chokaa na ujenzi katika kijiji cha Nanyala
kilichopo
katika Wilaya ya Mbozi iliyopo mkoani Songwe kuendelea na
shughuli zao wakati wakisubiri suluhu ya mgogoro baina yao na kiwanda
cha saruji cha Mbeya.
Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo
leo tarehe 17 Oktoba, 2018 alipokuwa akizungumza katika mkutano na
wachimbaji wadogo uliofanyika katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi
mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa
huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza
na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake Nyongo
aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, John Palingo, Afisa Madini
Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini anayesimamia
wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko, Afisa Madini kutoka Ofisi
ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi, vyombo vya ulinzi na
usalama vya wilaya pamoja na waandishi wa habari.
Nyongo alifafanua kuwa, awali
maelekezo yalitolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kutaka
viongozi kutoka katika mikoa ya Mbeya na Songwe kukaa pamoja na
kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa Songwe na
Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji nje ya mahakama jambo ambalo
linafanyiwa kazi kwa sasa.
Alielekeza viongozi kutoka katika
mikoa husika kuhakikisha wanashughulikia mgogoro wa ardhi kati ya mikoa
miwili na kiwanda cha saruji cha Mbeya kwa wakati huku wananchi
wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini wakiendelea na
shughuli zao kama kawaida katika maeneo husika.
Aliendelea kusema kuwa, jukumu kuu
la Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ni kuhakikisha wanatoa
leseni za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini
na kusisitiza kuwa leseni ya uchimbaji wa madini ni tofauti na hati ya
ardhi kwa kuwa inahusisha madini yaliyopo chini ya ardhi.
“Ningependa ieleweke kuwa, leseni
ya madini inampa mtu kibali cha kuchimba madini yaliyopo chini ya ardhi
ambayo ni tofauti na hati ya ardhi, hivyo wachimbaji wa madini wana haki
ya kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini wakati suala la mgogoro
wa ardhi likiendelea kushughulikiwa na mamlaka husika,” alisisitiza
Nyongo.
Akielezea taratibu za kuchimba
madini mara baada ya kupata leseni, Naibu Waziri Nyongo alisema mara
baada ya mchimbaji kupata leseni ya uchimbaji wa madini anatakiwa kufika
katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadaye kutambulishwa katika Ofisi ya
Kijiji ili kukutanishwa na wananchi na kufanya makubaliano ya ulipaji
fidia kabla ya kuanza shughuli rasmi za uchimbaji wa madini.
Alisisitiza kuwa, ni lazima
wawekezaji wote katika shughuli za uchimbaji wa madini kuhakikisha kuwa
wanajitambulisha na kufanya makubaliano na wananchi kabla ya kuanza
rasmi kwa uchimbaji wa madini ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Nyongo aliwataka maafisa madini katika mikoa ya Mbeya na Songwe
kuendelea na zoezi la kuainisha maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa
madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa leseni ili uchimbaji wao uweze
kuleta tija kwenye uchumi wa nchi.
Aidha, aliongeza kuwa katika
maeneo ambayo ni ya hifadhi au vivutio vya utalii leseni zake zifutwe
ili kuhakikisha rasilimali za maliasili zinalindwa na kuongeza pato
kwenye uchumi wa taifa.
Wakati huohuo Nyongo aliwataka
wachimbaji wa madini kuhakikisha kuwa wanalipa kodi mbalimbali ili
fedha hizo ziweze kutumika katika uboreshaji wa huduma nyingine za jamii
kama vile elimu, afya, miundombunu ya barabara.
Pia, Nyongo aliwataka wachimbaji
wa madini kuorodhesha kodi na tozo mbalimbali ambazo wanaona ni nyingi
na kuziwasilisha katika Wizara ya Madini, ili Wizara iangalie namna ya
kuzipunguza na wapate faida zaidi kwenye uchimbaji wa madini.
Awali wakizungumza katika nyakati
tofauti wachimbaji hao walieleza changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja
na mgogoro wa ardhi baina yao na kiwanda cha saruji cha Mbeya,
uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wachimbaji na ukosefu wa
maeneo kwa ajili ya uchimbaji wa madini.
No comments :
Post a Comment