Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa kwenye mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akipanda mti kwenye chanzo cha Mtawanya, Mtwara Mjini.
Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa
Mzingira Mtwara (MTUWASA), Mhandisi Mashaka Sita katika Mitambo ya Maji
Mangamba, Mtwara MJini.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wakazi wa Msanga Mkuu, Mtwara Vijijini.
Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa akiinama kwa ajili ya kuonja na kujua ubora wa maji katika mradi
wa Mpapura, Mtwara Vijijini.
……………………..
Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa leo amezindua rasmi Kampeni ya Upandaji Miti kandokando ya
vyanzo vya maji nchi nzima mkoani Mtwara kwa lengo la kuhakikisha vyanzo
hivyo vinatunzwa na kuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo.
Profesa Mbarawa amezindua kampeni
hiyo kwa kupanda miti nane katika chanzo cha Mtawanya kilichopo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mjini na kuzitaka Bodi zote za Mabonde
tisa nchini kuweka mkazo na mipango madhubuti ya kusimamia na kutunza
rasilimali za maji ziweze kuwa endelevu.
Ametoa agizo hilo kutokana na
uvamizi na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji katika maeneo mengi kwa
sasa nchini, hali inayohatarisha kiasi kikubwa cha maji kupungua
kutokana na vyanzo vingi kukauka, hali inayoweza kusababisha ukosefu wa
maji ya kutosha kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa na
Serikali.
Na kutaka vyanzo vyote vya maji
vitunzwe na kulindwa kwa kupandwa miti maalumu inayohifadhi maji na
kuagiza wale wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo waache
tabia hiyo na watakao kaidi wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa
wengine kwa kuwa sheria inaweka bayana kuhusu jambo hilo.
Ametoa tamko hilo kwa kuzingatia
Sheria ya Maji Na, 11 ya Mwaka 2009 inayokataza kufanya shughuli za
kibinadamu katika vyanzo vya maji, na ikieleza shughuli zote za
kibinadamu zifanyike umbali wa mita 6o kutoka chanzo cha maji kilipo na
kutaka maeneo yote yawekewe mipaka na vizuizi kuonyesha ukomo wa watu
kuingia kwenye vyanzo hivyo.
‘‘Hatutaki kupata hasara kwenye
miradi tunayowekeza fedha nyingi, halafu baadae iwe kama magofu kwa
kukosa maji. Imefika hatua kuwa ni lazima tuchukue hatua za lazima
kuinusuru taifa letu na uhaba wa maji. Niwatake wananchi watoe
ushirikiano wa karibu na Serikali kuhakikisha vyanzo vyetu vyote
vinakuwa endelevu kwa kuzalisha maji ya kutosha na kuwa na uwezo wa
kutoa huduma ya uhakika kwa miaka ijayo’’, amezungumza Profesa Mbarawa.
‘‘Kwa kuanza tumepanda miti nane
katika chanzo hiki cha Mtawanya, nataka ifikapo Disemba mwaku huu,
nikute zaidi ya miti 1,000 kwenye chanzo hiki na zoezi hili lifanyike
nchi nzima kwa sababu kama waziri mwenye dhamana ya kusimamia rasilimali
za maji nitalisimamia jambo hili ipasavyo’’, ameonya Profesa Mbarawa.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara
Mjini, Evod Mmanda amesema ni muhimu zoezi la upandaji miti liwe
endelevu lenye kuzingatia upandaji wa miti na kuachana na miti isiyo
rafiki na maji kwa lengo la utunzaji wa maeneo yote yenye vyanzo na
kutaka wananchi wazingatie sheria iliyopo kwa hiari, pasipo kutumika
nguvu na kuonya kuwa hatavumilia uharibifu wa vyanzo vya maji katika
wilaya yake.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya
Maji hivi karbuni imetoa Shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya malipo ya
madai kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya maji katika
Mkoa wa Mtwara, ambapo uzalishaji wa maji kwa siku kwa mji wa Mtwara
umefikia lita milioni 10, huku mahitaji kwa siku ni lita milioni 13.7.
Fedha hizo zimetolewa kwa lengo la
kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati
na kuanza kutoa huduma, ambapo hadi sasa miradi 45 ikiwa imeshakamilika
na mingine 33 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
No comments :
Post a Comment