Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akiwahutubia Wanafunzi wa kidato
cha nne wa shule ya Sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam
wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye skafu) akimkabidhi cheti
mwanafunzi bora katika masomo yote wa kidato cha nne katika shule ya
Sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam, Richard Sagwe
wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye skafu) akiangalia baadhi ya
kazi mbalimbali za Sanaa zinazofanywa na Wanafunzi katika shule ya
sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali
ya kidato cha nne shuleni hapo
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye skafu) akiwa ameongozana na
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Bw. Richard Kayombo
(kushoto) pamoja na uongozi wa shule ya sekondari Misitu iliyopo Kivule
Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
(PICHA ZOTE NA TRA)
……………………………..
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imechangia kiasi cha Shilingi Milioni 25 kwa ajili ya
ujenzi wa maabara
ya Kompyuta katika shule ya Sekondari Misitu iliyopo Wilaya ya Ilala,
jijini Da es Salaam.
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles
Kichere, ametoa mchango huo ikiwa ni sehemu ya kuchangia maendeleo kwa
jamii alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 9 ya kidato cha Nne
katika shule hiyo ambapo wanafunzi 205 wanaotarajia kuhitimu masomo yao
mara baada ya kufanya mtihani wa Taifa mwezi Novemba 2018.
Kamishna Mkuu Bw. Kichere, amesema
kuwa kiasi hicho cha fedha kitachangia ujenzi wa Maabara ya Kompyuta na
kuwafanya wanafunzi kujifunza na kuongeza uelewa zaidi wa masuala ya
Teknolojia.
“Nimesikia katika changamoto
mlizozitaja kuwa mnahitaji jengo la maabara ya kompyuta, uzio pamoja na
jengo la utawala na mimi nimeona vyema nichangie ujenzi wa jengo hilo
ili wanafunzi wapate kujifunza na kuwa na uelewa wa teknolojia kwani
dunia sasa inatumia zaidi teknolojia ya habari na mawasiliano katika
kuleta maendeleo”, alisema Kichere
Aidha, Bw. Kichere aliongeza kuwa,
ujenzi na maendeleo ya shule za serikali unatokana na kodi hivyo
aliwataka wanafunzi, walimu na wazazi kuwa na utamaduni wa kudai risiti
za mashine za kielektroniki (EFD) ili kuchangia Mapato yatakayotumika
kuboresha ujenzi na uboreshaji wa shule pamoja na shughuli mbalimbali za
kijamii.
Bw. Kichere alisisitiza kuwa
matunda ya kodi zinazopatikana pia hutumika kuboresha huduma mbalimbali
za jamii kama vile ununuzi wa vitabu kwa ajili ya maktaba, utoaji wa
mikopo ya elimu ya juu, ujenzi wa madarasa, mabweni, nyumba za walimu na
ununuzi wa vifaa vya maabara na kufundishia.
“Hivyo, natoa wito kwenu wahitimu,
wazazi, walimu pamoja na wanafunzi kwa ujumla kuwa mabalozi wazuri wa
masuala ya kodi na kuifundisha jamii umuhimu wa kulipa kodi popote
mtakapokuwa” alisisitiza Kamishna Mkuu wa TRA.
Kamishna Mkuu pia alifafanua
juhudi za Mamlaka ya Mapato Tanzania kuanzisha Vilabu vya kodi katika
shule za sekondari kuwa ni kuwaandaa walipakodi wa baadaye ambao ni
wazalendo pamoja na mabalozi wa mafanikio ya ulipaji kodi wa hiyari.
“Tunaamini kwa kufanya hivi
tutakuwa na Taifa la watu wazalendo wanaopenda kuchangia maendeleo ya
nchi yao kupitia kodi wanazolipa kwa hiari”, alisema Kichere
Bw.Kichere aliwapongeza wanafunzi
na uongozi wote wa shule kwa juhudi mbalimbali wanazozifanya kuhakikisha
shule hiyo inafanya vizuri mbali na Changamoto za vitendea kazi na
madarasa walizonazo, ambapo shule imeongeza ufaulu kutoka asilimia 50
mwaka 2010 hadi asilimia 63.5 kwa mwaka 2017.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule
Bw. Malima Clement ameishukuru TRA kwa kuchangia ujenzi wa jengo la
maabara ya kompyuta na kuahidi kushirikiana na wajumbe wa Bodi ya shule
pamoja na wazazi kuhakikisha Kompyuta pamoja na vifaa vingine mbalimbali
vinapatikana kwa ajili ya wanafunzi kujifunza pindi jengo
litakapomalizika.
Shule ya Misitu ni moja kati ya
shule zenye Vilabu vya Kodi kwa shule za Sekondari ambapo kwa mwaka huu
2018 ilishika nafasi ya tatu kwa upande wa uwasilishaji mada zinazohusu
masuala mbalimbali ya kodi katika mashindano ya 11 ya vilabu vya kodi
kwa mikoa wa Dares Salaam na Pwani yaliyofanyika katika chuo cha kodi.
No comments :
Post a Comment