Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Millanzi ametoa rai
hiyo leo alipokuwa akiwaaga rasmi watumishi wa Wizara ya Maliasili na
Utalii kufuatia kustaafu kwake rasmi Jeshi pamoja na Utumishi wa Umma na
kuwataka watumishi hao kufanya kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya
juu
Meja Jenerali
Millanzi ameelezea kufurahishwa kwake na ushirikiano alioupata kutoka
kwa
watumishi wa Wizara hiyo na kuelezea kuwa, ndio umemwezesha
kuiongoza vema wizara hiyo kwa kipindi alichokuwepo madarakani na
kupelekea mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo Wanyamapori,
Utalii, Misitu na Nyuki na Malikale.
Ameongeza kuwa,
Wizara ya Maliasili na Utalii imepata mafanikio makubwa katika vita
dhidi ya ujangili ambayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopatikana
kutoka kwa watumishi wa Wizara, wananchi, Serikali pamoja na wadau
mbalimbali wa Wanyamapori.
“Katika Kipindi
tulichokuwa pamoja, kuna mambo mengi tumeyakamilisha. Nimefanya kazi
nanyi na kila mmoja wenu alikuwa akinisaidia ili Wizara yetu iweze
kusonga mbele. Hakuna hata mmoja aliyeonyesha kutaka kunikwamisha.
Ninawashukuru sana”Alisema Meja Jenerali Millanzi.
Akizungumza
kwenye hafla fupi ya kumuaga Meja Jenerali Gaudence Millanzi
iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa UDOM jijini Dodoma na
kuhudhuriwa na watumishi wapatao 113 wa Wizara hiyo, Kaimu katibu Mkuu
wa Wizara hiyo Dkt. Aloyce Nzuki, amempongeza Meja Jenerali Gaudence
Millanzi kwa kumaliza salama Utumishi wa Umma na kulitumikia Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kipindi kirefu.
Amesifu Meja
Generali Millanzi kwa umahiri wake katika utendaji hasa namna alivyoweza
kufanya kazi na raia kwa ushirikiano wa hali ya juu wakati yeye ni
mwanajeshi.
“ Umefanya mambo
makubwa kwa kuweka mifumo mizuri pamoja na kubuni mikakati na mbinu za
kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili Wizara kiutendaji na
kuhakikisha
watumishi wanapata utulivu wa akili kwa kujali maslahi ya watumishi na
haki zao na hivyo kuwawezesha kufanya kazi wakiwa na utulivu wa akili
jambo liliongeza ufanisi katika kazi.”ameelezea Dkt. Nzuki.
Akitoa Shukrani
kwa ushirikiano alioupata kutoka kwa Dkt. Nzuki wakati akiiongoza Wizara
hiyo, Meja Jenerali Gaudence Millanzi amesema, amepata ushirikiano
mkubwa kiutendaji kutoka kwa Dkt. Nzuki na kuwaasa watumishi wote
waendelee kutoa ushirikiano mkubwa kwa Kaimu Katibu Mkuu huyo na kwa
viongozi wengine wa Wizara ili kuhakikisha Malengo ya Kitaifa yanafikiwa
katika kukuza uchumi wa nchi.
Ni muhimu sana
kuhakikisha tunamuunga mkono Rais wetu Mhe. John Pombe Magufuli katika
juhudi kubwa anazozifanya kuhakikisha tunapata nyenzo za kutuwezesha
kuongeza idadi ya watalii nchini ikiwemo ununuzi wa ndege ujenzi wa
miundo mbinu ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege na madaraja ya juu kwa
juu (Fly overs) jambo ambalo litarahisisha huduma za usafiri na kuondoa
kero ya foleni kwa raia na wageni na hivyo kuwa chachu ya kuongeza
idadi ya watalii nchini.
Meja Jenerali
Millanzi amesema, pamoja na kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa
watumishi, lakini anaamini kuwa yapo maamuzi aliyoyafanya ambayo
anaamini hayakuweza kumfurahisha kila mmoja lakini yalikuwa mazuri kwa
maslahi ya nchi. Na huu ndio uongozi.
Ameongeza kuwa “
Ninamshukuru MUNGU nimestaafu salama kwani Wizara ya Maliasili na Utalii
ni Wizara Muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na inagusa maslahi ya
wengi. Wakati huo huo jukumu nililopewa na Mhe. Rais ni kusimamia
maslahi ya nchi na si ya mtu mmoja mmoja hivyo naamini kuna maslahi ya
watu yalivurugwa na hivyo mimi kuwa mwiba kwao.”
Naye Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali Watu Bwana Lusius Mwenda amesema, kwa kipindi
kifupi alichofanya kazi na Meja Jenerali Gaudence Millanzi amepata
kujifunza mambo mazuri kutoka kwake akiwa kiongozi Mtendaji wa Wizara
hiyo.
Ameyataja mazuri
hayo kuwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka, uwezo wa
kusikiliza walio chini yake kiumakini na kutoa maamuzi yenye busara
pamoja na kujali maslahi ya Watumishi.
Akizungumza kwa
niaba ya watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mtumishi Eliud Kilo
amemwelezea katibu Mkuu huyo kuwa, alikuwa kiongozi wa watu aliyekuwa
akisikiliza shida za watumishi wake ikiwa ni pamoja na kuzipatia
ufumbuzi wa haraka.”
“Katibu Mkuu tulikupenda sana kwa jinsi ulivyokuwa ukifanya kazi na sisi.” Amesisitiza Mtumishi Eliudi.
Wakielezea namna
walivyofanya kazi na Meja Jenerali Gaudence Millanzi, baadhi ya
Watumishi waliopata fursa ya kutoa maoni yao kuhusiana na Katibu Mkuu
huyo, wamesema, Kwa staili yake ya uongozi, ukiwa hujakamilisha kazi
aliyokuagiza, utajikuta moyo wako unakusuta na kujikuta bila ya
kusukumwa na mtu unabakia ofisini kuhakikisha unakamilisha kazi yako ili
usijikute ukimkwaza kiongozi huyo mahiri aliyewapenda na kuwaheshimu
watu walio chini yake. Tunatamani angeendelea kutuongoza na kukamilisha
malengo tuliyokuwa tumejiwekea kiwizara. Watumishi hao walimuombea kila
la heri katika maisha yake ya Kustaafu.
Meja Jenerali
Gaudence Millanzi aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii mwezi Disemba 2015 na kustaafu Jeshi na Utumishi
wa Umma tarehe 16 Mwezi Septemba mwaka huu.
No comments :
Post a Comment