Rais Dkt. John Pombe Magufuli
“Wataalamu wasiwe chanzo cha kukwamisha miradi” – Rais Magufuli
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
RAIS Dkt. John
Pombe Magufuli amewataka wataalamu wa kitanzania kutokuwa chanzo cha
kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini yenye
lengo la kuleta maendeleo kwa taifa.
Akizungumza leo
Alhamisi (Septemba 27, 2018) Jijini Dar es salaam, wakati akifungua
rasmi barabara ya juu ya Patrick Mfugale iliyopo katika makutano ya
barabara ya Mandela na
Nyerere, Rais Magufuli alitoa wito kwa wataalamu
wa kitanzania wasiwe chanzo cha kukwamisha miradi mbalimbali kwa kuwa
miradi hiyo ina lengo la kuwasaidia Watanzania.
“Wataalamu wasiwe
chanzo cha kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa, ni
lazima tuweke maslahi yetu kwanza, tusitumike kukwamisha kutekeleza
miradi itakayoasaidia Watanzania” alisisitiza Rais Magufuli
Aidha, Rais
Magufuli alimpongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale na kusema kuwa anamfahamu mhandisi
huyo kama mtu mzalendo, mwaminifu, mwadilifu na mchapakazi.
“Nampongeza
Mtendaji Mkuu Mfugale kwa kubuni, kuandaa mchoro wa barabara hii, ambapo
pia amebuni michoro ya daraja la Mkapa lenye urefu wa km 10, ambalo ni
daraja refu kuliko yote katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati”
alisema Rais Magufuli.
Vilevile, Rais
Magufuli aliishukuru Serikali ya Japan kwa kutoa msaada ulioasaidia
katika ujenzi wa barabara hiyo, na kusema kuwa ni misaada inayolenga
kutatua changamoto yenye kuleta mabadiliko ya kweli.
Aidha, Mtendaji
Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale alisema kuwa barabara hiyo
inayojulikana kama barabara ya juu ya Mfugale yenye urefu wa takribani
kilomita moja, imefanikiwa kupunguza msongamano wa magari kwa asilimia
100 kutoka Airport kuelekea mjini na asilimia 50 kutoka Bandarini
kuelekea Ubungo.
Naye, Mwakilishi
Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA),Toshio Nagase aliipongeza
kampuni za Japan na Tanzania ambazo zimeshirikiana katika ujenzi wa
barabara hiyo kwa kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia kwa wakati na
kutopata ajali yoyote wakati wa utekelezaji wake.
“Najivunia uwepo
wenu katika mradi huu, hii imeonesha ushirikiano na urafiki mkubwa
uliopo kati ya nchi za Tanzania na Japan, pia mmefanikiwa kukamilisha
mradi huu kwa kutumia masaa 2, 100,000 ya ujenzi bila kupata ajali
yoyote na umekabidhiwa kwa Watanzania kama ilivyopangwa” alisema Nagase
Kwa upande wake,
Balozi wa Japan nchini Tanzania, Balozi Masaharu Yoshida alisema kuwa
barabara hiyo imepunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa,
itasaidia ukuaji wa uchumi kwa vile inarahisisha usafirishaji wa watu na
mizigo.
Aidha, aliongeza kuwa mradi huo ni alama muhimu ya urafiki na uhusiano wa kudumu kati ya nchi za Tanzania na Japan.
Mradi wa ujenzi
wa barabara ya juu ya Mfugale ulianza kujengwa mwaka 2016, kwa kutumia
fedha za mkopo wa nchi ya Japan na kiasi kingine kikiwa ni fedha
kilitolewa na Serikali ya Tanzania.
Barabara hiyo
yenye mita 425, imejengwa kwa kutumia nguzo kubwa sita, ina urefu wa
kilomita moja, yenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 180 kwa wakati mmoja.
No comments :
Post a Comment