Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary
Senyamle akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wafanyabiashara
iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kutoa
elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi. Semina hiyo imefanyika
Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi
kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Diana Masalla akitoa
elimu ya kodi wakati wa semina ya wafanyabiashara iliyofanyika Wilaya
ya Same mkoani Kilimanjaro.
Afisa Kodi Mwandamizi kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Shaban Makumlo akiwasilisha
mada kuhusu Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye Malimbikizo ya Madeni ya
Kodi wakati wa semina ya wafanyabiashara iliyofanyika Wilaya ya Same
mkoani Kilimanjaro.
Afisa Maadili Mwandamizi kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Adelaida Rweikiza
akiwasilisha mada kuhusu Mfumo wa Maadili kwa Watumishi wa TRA wakati wa
semina ya wafanyabiashara iliyofanyika Wilaya ya Same mkoani
Kilimanjaro.
Baadhi
ya wafanyabiashara wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa mada
mbalimbali wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika Wilaya
ya Same mkoani Kilimanjaro. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).
Na Veronica Kazimoto
Same
20 Septemba, 2018
Wafanyabiashara
Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wamefurahia elimu ya kodi iliyotolewa
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwa na lengo la kuwaongezea
uelewa juu ya
Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye Malimbikizo ya Madeni ya
Kodi, Mabadiliko ya Sheria za Kodi kulingana na Sheria ya Fedha ya Mwaka
2018 na Mfumo wa Maadili kwa Watumishi wa TRA.
Wakizungumza
mara baada ya kumaliza semina hiyo, wafanyabiashara hao wamesema kuwa,
wamefurahishwa na elimu waliyoipata kutoka TRA na kwamba itawasaidia
katika shughuli zao za kila siku.
“Binafsi
leo nimefurahi sana kupata elimu ya kodi ambayo kwa hapa Same tuna
takribani mwaka mzima bila kupatiwa elimu hii, kwa kweli ninaomba TRA
watupatie semina hizi mara kwa mara ili tuweze kuendesha biashara zetu
kwa ufanisi”, alisema Regina Msuya ambaye ni Mfanyabiashara wa Vifaa vya
Shule na Ofisi.
Msuya
ameongeza kuwa, ni muhimu Mamlaka ya Mapato Tanzania iangalie namna ya
kuongeza muda wa semina hizo ili waweze kuyapata kwa undani masuala yote
yanayohusiana na kodi.
Kwa
upande wake Mfanyabiashara anayemiliki Baa wilayani hapa Tizinga Mbogo,
mbali na kufurahishwa na elimu ya kodi aliyoipata, ameiomba TRA
kushirikiana na ofisi ya Afisa Biashara ili kuondoa changamoto
zinazowakabili ambazo utatuzi wake hutegemea ofisi hizo mbili.
“Kwanza
kabisa naomba elimu hii iendelee maana tumejifunza mambo mengi mazuri
kutoka kwa wenzetu wa TRA, aidha naomba Afisa Biashara ashirikiane na
Mamlaka ya Mapato Tanzania hapa wilayani kwetu kwa ajili ya kututalia
kero ambazo zinategemea maamuzi ya ofisi hizi mbili,” alieleza Mbogo.
Awali
akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Senyamle,
amewahimiza wafanyabiashara wote wenye malimbikizo ya madeni ya kodi
yanayotokana na riba na adhabu kuwahi kutuma maombi ya msamaha pamoja na
kuwataarifu wenzao wenye madeni kama hayo.
Elimu
ya kodi inaendelea kutolewa katika Mikoa ya Kaskazini ambapo baada ya
kumaliza Mkoa wa Tanga, sasa elimu hiyo inatolewa katika Mikoa ya
kilimanjaro, Arusha na Manyara.
No comments :
Post a Comment