Na Rhoda James, Geita
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo ameutaka Mgodi wa Geita Gold Mine Ltd kuwalipa fidia wananchi
waliopata madhara ya nyufa katika katika nyumba zao kutokana na
shughuli
za uchimbaji wa madini wa kampuni hiyo.
Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo
tarehe 26 Septemba, 2018 wakati alipofungua Maonesho ya Kwanza ya
Teknolojia ya Uchimbaji na Uwekezaji wa Madini ya Dhahabu mkoani Geita
kwa niaba ya Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.
Alitoa rai kwa Wachimbaji wadogo
wa madini kote nchini kushiriki maonesho hayo yanayoendelea mkoani humo
kwa kuwa yatawanufaisha kwa kupata fursa ya kujifunza kuhusu teknolojia
mbalimbali na namna bora ya uchimbaji, uchenjuaji, ikiwemo kupata elimu
ya kulinda mazingira na kuzalisha kwa tija.
Pia, aliwataka Wakuu wa mikoa yote
nchini pamoja na Wakuu wa wilaya zote kujifunza kutoka kwa Mkuu wa Mkoa
wa Geita, Gabriel Luhumbi ili kuhakikisha kuwa wananchi wao wanafaidika
na rasilimali pamoja na mazao yanayolimwa katika maeneo yao.
“Mkifanya maonesho ya aina hii
katika mikoa yenu kulingana na mazao au rasilimali mlizonazo katika
mikoa yenu wananchi wenu watafaidika,” alisema Naibu Waziri wa Madini
Stanslaus Nyongo.
Vilevile, Naibu Waziri Nyongo,
aliwataka wananchi wa mkoa wa Geita na Kagera pamoja na wadau wa
madini ya dhahabu kujipanga ili kuhakikisha kuwa maonesho hayo
yanafanyika kila mwaka.
Pia, Naibu Waziri Nyongo alisema
kuwa, Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana na uongozi kutoka Mkoa wa
Geita kuhakikisha kuwa wanayatangaza maonesho hayo kwa kiasi kikubwa
ili yaweze kufahamika duniani kote hatimaye wadau wa madini waweze
washiriki kwa wingi.
No comments :
Post a Comment