Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Selemani Jafo
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
27.9.2018
SERIKALI
imeendelea kutoa kipaumbele katika huduma za afya zenye ubora na
zinazowafikia wananchi wote ili kuboresha afya zao kwa kutambua kuwa
afya bora ni raslimali muhimu kwa maendeleo.
Maendeleo ya
Taifa lolote la duniani yanaletwa na wananchi wenye afya na wenye uwezo
wa
kuzalisha mali na Serikali imeendelea kushirikiana na wadau
mbalimbali kutoa huduma za afya kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.
Kabla ya Uhuru,
huduma za afya nchini zilikuwa zinatolewa zaidi kwenye maeneo ya
shughuli za kiuchumi kama miji na mashamba makubwa na baada ya Serikali
iliweka msukumo zaidi katika kupanua huduma za afya ili kuwafikia
wananchi wengi hasa walioko vijijini.
Ili kufanikisha
azma hii, Serikali iliweka mfumo wa rufaa wa huduma za afya kupitia
mfumo wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za
mikoa, maalum, kanda na taifa zilianzishwa.
Serikali ya Awamu
ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli inaendelea
kuimarisha na kuboresha huduma katika sekta ya afya kuanzia katika
ngazi ya kijiji mpaka Hospitali ya Taifa.
Moja ya mipango
ya haraka inayotarajiwa kufanikishwa kwa ufanisi mkubwa na Serikali ni
pamoja na kuimarisha miundombinu na mahitaji ya watumishi wa kada za
afya kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali ya wilaya na
hospitali ya rufaa ya mkoa.
Katika bajeti ya
Mwaka 2018/19, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), imeliomba Bunge kuiidhinisha kiasi cha Tsh
Trilioni1,458,291,418,500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali
ya maendeleo ikiwemo afya, maji, elimu, barabara n.k
Akiwasilisha
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya mwaka 2018/19, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Selemani Jafo anasema Serikali imeongeza
bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba, chanjo na vitendanishi kutoka Tsh.
Bilioni 31 zilizotengwa Mwaka 2015/16 hadi Tsh. Bilioni 269 zilizotengwa
katika Mwaka 2017/18.
Anaongeza kuwa
katika ya fedha hizo, Tsh. Bilioni 98.08 zimetengwa kwa ajili ya huduma
ya afya ya msingi kwenye Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati
pamoja na ongezeko la upatikanaji wa dawa muhimu kufikia asilimia
92 ikilinganishwa na asilimia 81 katika kipindi kama hicho Mwaka 2016.
Aidha Waziri Jafo
anasema Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya
208 ili kuviwezesha kutoa huduma za dharura za upasuaji kwa ajili ya
kuboresha huduma zote za Vituo vya Afya. Kati ya Vituo hivyo 15 ni vipya
na 14 ni zahanati zilizopandishwa hadhi na vituo vitatu (3) ni maboma
yasiyokamilika.
“Vituo vya Afya
vilivyopo ni 696 sawa na asilimia 15.7 ya lengo la kuwa na Vituo vya
Afya 4,420 ambapo kati ya hivyo, vituo 513 vinamilikiwa na Serikali na
vituo 183 vinamilikiwa na Sekta Binafsi na Mashirika ya Dini” anasema
Waziri Jafo.
Akifafanua zaidi
Waziri Jafo anasema ujenzi wa vituo hivyo utagharimu kiasi cha Tsh.
Bilioni 93.5 hadi kukamilika kwake pamoja na kutenga Tsh. Bilioni
50.2 kwa ajili ya kununulia vifaa tiba pamoja na samani ili kuviwezesha
kuanza kutoa huduma.
Anaongeza kuwa
Ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto zimeandaa mkakati wa pamoja wa kukamilisha
ukarabati na ujenzi wa vituo vyote ili kuboresha huduma za Afya na
kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kupitia wadau wa maendeleo wa Mfuko
wa Pamoja wa Afya.
Sanjari na ujenzi
wa vituo vya afya, Waziri Jafo anasema katika mwaka 2017/18 Serikali
iliidhinishiwa na Bunge Tukufu jumla ya Tsh. Bilioni 35.5 kwa ajili ya
kuendelea na ujenzi wa Zahanati, kipaumbele kikiwa ni kukamilisha ujenzi
wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
“Serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imekamilisha ujenzi wa
nyumba 578 za watumishi wa afya katika vituo vya afya 268 kwenye
Halmashauri 51, lengo ni kuhakikisha kila kituo cha kutolea huduma za
Afya kinakuwa na nyumba angalau mbili ifikapo Mwaka 2020 ili kuboresha
mazingira ya kazi kwa watumishi” anasema Waziri Jafo.
Waziri Jafo
anasema Ofisi yake pia imeanza matumizi ya mfumo wa jazia kwa kutumia
Washitiri (Prime Vendor) katika Mikoa ya Dodoma, Morogoro na Shinyanga
ambao lengo ni kuhakikisha dawa zinakuwepo katika vituo vya kutolea
huduma za Afya endapo zimekosekana katika Bohari Kuu ya Madawa.
Anaongeza kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha mfumo huu unatumika katika Mikoa yote 26 nchini.
Ili kufanikisha
azma ya Serikali kufikia uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda
ifikapo mwaka 2025, ni dhahiri kuwa afya ndiyo mtaji na msingi mkuu wa
mafanikio hayo katika uzalishaji mali katika sekta mbalimbali za
maendeleo.
No comments :
Post a Comment